Na Sharon Sauwa na Habel Chidawali,Mwananchi
Posted Jumatano,Oktoba30 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumatano,Oktoba30 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
“Inashangaza sana kuwa wale wanaotajwa hawachukuliwi
hatua, lakini wananchi wanazidi kuteseka… Mathalani, zipo taarifa kuwa
wakuu wa polisi katika mikoa inayopakana na Mbuga ya Serengeti ndio
waratibu wa shughuli za ujangili, lakini hatujasikia hao wakichukuliwa
hatua,”
Dodoma. Wabunge jana
walichachamaa na kushinikiza kutolewa kwa orodha ya vigogo
wanaojihusisha na ujangili wakati wa kikao cha kwanza cha mkutano wa 13
wa Bunge unaofanyika mjini Dodoma.
Wabunge hao walitaka kutajwa kwa majina ya mawaziri, viongozi wa Serikali na wabunge wanaojihusisha na biashara hiyo.
Baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na
majibu, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, aliomba mwongozo,
akiitaka Serikali kuwataja hadharani na kuwachukulia hatua viongozi wake
na wanasiasa, wakiwamo mawaziri na wabunge, ambao wanatajwa kuhusika na
vitendo vya ujangili nchini.
Lugola aliomba mwongozo wa Naibu Spika baada ya
kutoridhishwa na jibu lililotolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa
Kahama (CCM), James Lembeli.
Katika jibu hilo, Nyalandu alilieleza Bunge kuwa
Operesheni Tokomeza inayolenga kukomesha vitendo vya ujangili nchini
bado inaendelea, lakini alishindwa kulieleza Bunge ni nani hasa
wamebainika kuhusika na vitendo hivyo.
Lugola, hata hivyo, aliitaka Serikali kuwasilisha ripoti bungeni kuhusiana na utekelezaji wa operesheni hiyo.
“Tangu Aprili tumekuwa tukipewa majibu mepesi kuhusiana na operesheni hii, wakati suala hili si la masihara,” alionya Lugola.
Lugola alisema kuwa taarifa zimewataja watu
wanaohusika na vitendo hivyo wakiwamo viongozi serikalini, mawaziri
pamoja na wabunge, lakini tangu operesheni hiyo ilipoanza hakuna yeyote
miongoni mwa hao wanaotajwa ambaye amekamatwa isipokuwa wananchi wa
kawaida.
Alisema operesheni hiyo imekuwa ikiendeshwa kwa
unyama kwani wanaokamatwa hupigwa na kuteswa bila ya ushahidi
unaoonyesha kuhusika kwao na vitendo vya ujangili.
“Inashangaza sana kuwa wale wanaotajwa
hawachukuliwi hatua, lakini wananchi wanazidi kuteseka… Mathalani, zipo
taarifa kuwa wakuu wa polisi katika mikoa inayopakana na Mbuga ya
Serengeti ndio waratibu wa shughuli za ujangili, lakini hatujasikia hao
wakichukuliwa hatua,” alisema.
Kabla ya Naibu Spika kutoa majibu ya mwongozo
ulioombwa na Lugola, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisimama na kukiri kuwapo kwa
vitendo vya utesaji wa watu wanaokamatwa katika operesheni hiyo.
Alitolea mfano tukio la kukamatwa kwa msaidizi
wake jimboni ambaye alipigwa na kuteswa na askari hao kabla ya kuachiwa
baada ya kushikiliwa kwa siku moja, huku akionyesha kuwa ushahidi wa
tukio hilo anao kwenye simu yake.
SOURCE: MWANANCHI
Serikali yakiri tatizo
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi
Vuai Nahodha akizungumza bungeni kwa niaba ya Waziri Mkuu, alikiri
kuwapo fununu za wanasiasa ambao wamekuwa wakijihusisha na biashara hiyo
na kusema Serikali italifanyia kazi jambo hilo.
Nahodha aliwataka Watanzania kuwa watulivu wakati
vyombo vya Ulinzi na Usalama vinaposhughulika na kusafisha tatizo hili
na kuonya wanasiasa kuacha kutoa shinikizo kwa kutumia nguvu zao za
kisiasa.
SOURCE: MWANANCHI