Na Emmanuel Rubagumya, Mwananchi
Posted Ijumaa,Oktoba11 2013 saa 11:59 AM
Posted Ijumaa,Oktoba11 2013 saa 11:59 AM
Kwa ufupi
- Jopo la madaktari bingwa wa upasuaji wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) wakishirikiana na wenzao ( MNH) walifanikisha upasuaji huo wa mtoto aliyezaliwa akiwa ameungana na mwenzake sehemu ya chini ya uti wa mgongo.
- Kinamama waanze kutumia madini ya folic acid pale wanapojitayarisha kubeba mimba, maana haya yanasaida katika kujenga viungo vya mtoto tumboni.
Upasuaji wa kuwaokoa pacha pengine
unadhaniwa kuwa ni jambo linalowezekana nchi za nje pekee. Lakini hata
hapa nchini, inawezekana.
Agosti 30, 2013 ulifanyika upasuaji wa kihistoria
kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambapo mtoto aliyezaliwa
ameungana na mwenzake kwa sehemu ya chini ya uti wa mgongo
alitenganishwa na mwenzake ambaye hata hivyo hakuwa amekamilika viungo
vyake.
Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji wa Watoto, MNH Dk
Zaitun Bokhary anaeleza mengi kuhusu tukio hilo na masuala mengine
yanayohusu umahiri wa MNH katika kukabiliana na aina hiyo ya tatizo
katika jamii pamoja na pia kutoa ushauri.
Anasema tukio hilo limeandika historia nyingine kwenye tasnia ya kitabibu nchini na kuonyesha kuwa Watanzania wanaweza.
Jopo la madaktari bingwa wa upasuaji wa Taasisi ya
Mifupa Muhimbili (MOI) wakishirikiana na wenzao ( MNH) walifanikisha
upasuaji huo wa mtoto aliyezaliwa akiwa ameungana na mwenzake sehemu ya
chini ya uti wa mgongo.
Licha ya kuwa na uhai, kiwiliwili cha mtoto huyo
mwingine hakikuwa na viungo muhimu kama kichwa na macho. Pia, hakikuwa
pia na moyo, figo, tumbo na maini, ila kilikuwa na uti wa mgongo.
Mtoto huyo ambaye amepewa jina la Kudra
alifikishwa MNH akitokea Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, Zanzibar
alikozaliwa na mama yake, Pili Hija (24), Agosti 18, 2013.
Kwa kuona uwezo wao, madaktari wa Mnazi Mmoja
waliamua kumhamishia MNH mtoto na mama yake kwa upasuaji mkubwa zaidi
ili kumwokoa.
Ushuhuda wa Dk Bokhary
Upasuaji kama huo wa kutenganisha watoto pacha walioungana si wa kwanza kufanyika katika hospitali hiyo na hapa nchini.
Anasema mwaka 1994, Profesa Joseph Shija, gwiji wa
kwanza Mtanzania mtaalamu wa upasuaji wa watoto aliwahi kufanya
upasuaji kama huo. Hata hivyo, tofauti na Kudra, watoto wale
waliofanyiwa upasuaji na Prof Shija walikuwa wamekamilika, waliungana
tumboni (omphalopagus), kila mmoja akiwa mtu kamili. Mmoja wao alipona,
mwingine alikufa.
Upasuaji mwingine wa kutenganisha pacha ni ule
uliofanywa na bingwa mwingine, Dk Petronila Ngiloi mwaka 2009 kwa pacha
waliokuwa wameungana sehemu ya chini ya uti wa mgongo (ischiopagus).
Kwa bahati mbaya, hao walifariki muda mfupi baada ya upasuaji wao.
Profesa Shija na Dk Ngiloi, wote kwa sasa ni wastaafu, ingawa wanaendelea na shughuli za tiba.
Dk Bokhary anasema kwamba baada ya kufanya vipimo
mbalimbali na uchunguzi wa kina, Kudra na kitegemezi chake, timu ya
wataalamu waliona kuwa ni kazi wanayoweza kuifanya.
“Tuliona kuwa ni ‘case’ (suala) tunayoweza kuifanya kama pakiwa na matayarisho mazuri na kujituma,” anasema Dk Bokhary.
Pamoja naye (Dk Bokhary), mabingwa wengine
waliohusika na upasuaji huo ni Dk Ngiloi (aliyekaribishwa), Dk Robert
Mhina (mifupa), Profesa Karim Manji (bingwa wa watoto), Dk Karim Khalid
(dawa ya usingizi), Dk Hamis Shaaban (mishipa ya fahamu na uti wa
mgongo) na Dk Bashir Nyangasa (moyo na mishipa ya damu).
Ingekuwa vipi kuwatenganisha watoto pacha wawili ambao wamekamilika?
Swali hilo analijibu Dk Bokhary akisema kuwa mara
nyingi huwa ni changamoto kubwa zaidi. Ugumu huo hutokana na jinsi
pacha hao walivyoungana.Anaongeza kuwa huhitajika wataalamu wengi zaidi
na wa aina tofauti, teknolojia na vyombo vya kisasa.
Kwa mfano anaeleza tukio la watoto pacha, Eliud na
Elikana Erick Mwakyusa waliopokelewa katika hospitali hiyo ya rufaa
wakitokea mkoani Mbeya mapema mwaka huu. Hao anasema walikuwa wameungana
kwenye njia ya haja kubwa na wakiwa na sehemu moja ya kiume.
Kwao, haikuwezekana kutenganishwa nchini na
ililazimu kupata ufadhili wa kuwapeleka India kwa sababu ilihitaji
vipimo vya kisasa na utaalamu mkubwa ambao bado haupatikani nchini.
Kwa mfano, anasema pacha hao wanaoendelea na
matibabu India ikiwa ni matayarisho ya upasuaji mkubwa wa
kuwatenganisha, watahitaji wataalamu bingwa wa upasuaji wa watoto
waliobobea na wale wa njia ya mkojo, ambao bado hawapo nchini.
Pia, kama moja ya matayarisho, watoto hawa wanafanyiwa utaalamu unaojulikana kitaalamu kama ‘tissue expansion.’
Huduma hii, Dk Bokhary anaeleza kuwa bado haipo
hapa nchini na wataalamu wake wajulikanao kama ‘pediatric plastic
surgeons’ bado hawapo. Kitu kingine kinacholeta changamoto hadi
kufikia kupeleka watoto kama hawa nje ni kukosekana kwa huduma maalumu
baada ya upasuaji.
Dk Bokhary anafafanua kuwa uangalizi baada ya upasuaji wa aina hiyo huhitaji chumba maalumu cha uangalizi wa hali ya juu na wataalamu/wauguzi waliofunzwa maalumu kwa ajili ya kazi hiyo.
Dk Bokhary anafafanua kuwa uangalizi baada ya upasuaji wa aina hiyo huhitaji chumba maalumu cha uangalizi wa hali ya juu na wataalamu/wauguzi waliofunzwa maalumu kwa ajili ya kazi hiyo.
Chumba hicho kinajulikana kama ‘Neonatal Intensive Care Unit’ (NICU), ambacho hakipo katika hospitali hiyo na nyingine nchini.
“Huwezi kupeleka watoto wachanga kwenye ICU ya
watu wazima baada ya upasuaji kwa ajili ya uangalizi ni hatari na
haikubaliki kitaalamu,” anasema mtaalamu huyo na kuongeza kuwa bado hii
ni changamoto kubwa inayotakiwa kufanyiwa kazi.
Anasema wakati mwingine huwa anapata homa pale
ambapo anatakiwa kufanya upasuaji mkubwa huku akijua kabisa kuwa hakuna
Neonatal ICU katika hospitali hiyo, chumba ambacho husaidia sana
kufuatilia maendeleo kwa karibu na kwa kitaalamu huduma baada ya
upasuaji kufanyika.
Anasema Kudra amekuwa akiendelea vizuri kwa
ushirikiano mkubwa wa timu ya wataalamu waliomshughulikia kila mmoja
akimfuatilia kwa karibu kuhakikisha kila kitu kinakwenda vyema.
“Kusema kweli palikuwa na ushirikiano wa hali ya juu baina yetu,” anasema.
Sababu za kuzaliwa wakiwa wameungana
Anasema kuwa hadi sasa hakuna sababu maalumu inayojulikana kisayansi.
Dk Bokhary anasema pacha walioungana huwa ni
matokeo ya kushindwa kukamilika kwa mchakato wa yai kugawanyika na
hatimaye kila upande uanze kujenga viungo vyake ili wapatikane pacha
wanaofanana.
Mchakato huu hutakiwa kufanyika kati ya wiki ya
tano na wiki ya nane ya ujauzito. Hata hivyo, kwa sababu ambazo bado
hazijajulikana, mchakato huo hugoma kukamilika katika kipindi hicho na
kusababisha kuzaliwa kwa pacha walioungana.
Anasema kuwa tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa
kuna vihatarishi vinavyoweza kusababisha yai lishindwe kutengana sehemu
mbili kama inavyotakiwa. Anazitaja sababu hizo hatarishi kwa wazazi wote
wawili kunywa pombe kupindukia, kuvuta sigara kupita kiasi, mtindo wa
vyakula visivyofaa kama mafuta mengi, unene kupita kiasi na kutofanya
mazoezi.
“Tunadhani vihatarishi hivi vinaweza kusababisha mtu kuzaa mtoto asiye na afya au pacha walioungana,” anasema.
Pia, anashauri mama kuanza kutumia madini ya folic acid pale ambapo anajitayarisha kubeba mimba.
“Kinamama waanze kutumia madini haya pale wanapojitayarisha
kubeba mimba, maana haya yanasaida katika kujenga viungo vya mtoto
tumboni,” anaeleza.
Kwa mujibu wa daktari huyo bingwa, tafiti
zinaonyesha kuwa tatizo la watoto pacha kuzaliwa wakiwa wameungana ni
mara chache kutokea duniani ambapo kati ya kila watoto 100,000
wanaozaliwa, ni tukio moja huwa ni la pacha walioungana.
Pia, wingi wa kuungana huku hutofautiana ambapo
pacha walioungana tumboni ndio wanaoongoza kuzaliwa kwa asilimia 47; uti
wa mgongo (asilimia 26); na pacha wanaozaliwa wakiwa wameungana sehemu
ya kichwa ni asilimia 2.
Mapacha wanazaliwa huku mmoja akiwa hajakamilika viungo vyake au Conjoined Tetrapus Parasyticus Twins ni nadra zaidi kutokea.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI