Tuukubali ukweli, kuwa katika kilichoanishwa hapo juu, ni vigumu kuzungumzia Muungano wa Serikali MBILI badala ya MOJA au TATU.
Haiyumkini kuwa Majaji wetu na tume zao, kuanzia
Jaji Nyalali, Kissanga na sasa Warioba, wameliona tatizo ambalo halipo
na kuwa mapendekezo yao hayastahili kupewa uzito na kufanyiwa kazi.
Ikumbukwe, kuwa Tume ya Jaji Warioba inaundwa na
watu wenye hekima na busara nyingi akiwamo Mzee Salim Ahmed Salim na
Jaji Mstaafu Augustine Ramadhani. Ni juzi tu Mwanasheria Mkuu wa
Serikali wa zamani, Jaji Mark Bomani ameweka hadharani, kuwa muda wa
kuwa na Serikali Tatu umefika.
Naam, umefika wakati wa kuukubali ukweli, kuwa kwa
muundo huu wa Muungano tulio nao sasa, siku zote kutakuwa na
manung’uniko. Kuukataa ukweli huu ni sawa na kufagilia takataka chini ya
jamvi. Iko siku jamvi lazima liinuliwe na uchafu huo utaonekana tu.
Majuzi tu, Balozi Augustine Mahiga ambaye ni
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa UN nchini Somalia alizungumzia Rasimu ya
Katiba kama jitihada za ubunifu katika kufikia mwafaka wa mazungumzo
kuhusiana na kero za Muungano.
Balozi Mahiga anasema, kuwa ingawa Serikali Tatu
zina gharama zake, lakini kisiasa ina manufaa yake kutokana na mijadala
ya muda mrefu kuhusiana na muundo wa Muungano. Balozi Mahiga anazidi
kunukuliwa akisema, kuwa iwapo Rasimu hiyo itapitishwa na Watanzania, ni
wazi kwamba Tanzania itakuwa imerekebisha kasoro za Muungano unaotimiza
miaka 50 mwakani, kwa njia ya mazungumzo. ( Mwananchi, Jumapili, Juni
9, 2013, Uk 2)
Tafsiri yangu?
Aliyoyasema Balozi Mahiga yana uzito mkubwa sana.
Ni maneno yaliyojaa hekima na busara nyingi kutoka kwa Mtanzania na
Mwanadiplomasia mzoefu. Mahiga kwenye mazungumzo yake ametanguliza
masilahi mapana na ya muda mrefu ya taifa.
Nakubaliana na Balozi Mahiga kwenye usahihi wa njia ya Jaji Warioba na Tume yake kuhusiana na Serikali Tatu.
Maana, njia ni ile ile tuliyokuwa tukihangaika
kuifuata huku kukiwa na kero nyingi za njiani. Ni kwa vile njia ilikuwa
nyembamba mno, alichofanya Warioba na Tume yake ni kuipanua njia hiyo
ili hata malori yaweze kupita.
Katiba Mpya ina maana pia ya Mabadiliko Makubwa. Ninachokiona
mimi ni hofu ya mabadiliko kwa baadhi yetu. Kwa wengine ni hofu
inayotokana na sababu binafsi zenye kuambatana na kupoteza fursa hata
nafasi za kimamlaka katika mabadiliko yanayokuja. Hivyo, ni sababu za
kibinafsi zaidi na pengine hata kimakundi.
Ni hulka ya mwanadamu pia kuogopa mabadiliko
yanapotokea. Hata kwenye nyumba yako tu. Siku ukirudi nyumbani ukakuta
mfanyakazi wako wa ndani kapangua fenicha na kuziweka katika utaratibu
mpya , basi, utaanza kwanza kuyaogopa mabadiliko yale. Huenda akili yako
isitulie pia. Kidogo kidogo utaanza kuyazoea.
Hili la Serikali Tatu kwa historia tu inabidi
tupumue kwa akina Jaji Warioba kuja na ubunifu huu. Maana, imekuwa ni
kero sugu iliyoundiwa hata Wizara. Hatuwezi kuendelea na hali hiyo mwaka
hadi mwaka.
Maana, hata mimi binafsi, ningeulizwa mwaka 2000
juu ya muundo wa Muungano, basi, chaguo langu la kwanza lilikuwa
Serikali Moja, pili, Serikali Mbili na tatu Serikali Tatu.
Lakini, miaka 13 baadaye na kwa kusoma alama za
nyakati. Ukiniuliza leo swali hilo, jibu langu liko wazi kabisa, kuwa
tuwe na Serikali Tatu; Ya Muungano, Zanzibar na Tanzania Bara
(Tanganyika). Hii si heshima tu tutakayoipata kimataifa, bali,
itachangia kwa watu wa pande mbili hizi za Muungano kuheshimiana na
kushirikiana zaidi.
Tusisahau historia, kuwa Kamati ya Jaji Robert
Kissanga mwaka 2000 ilikuja na mapendekezo kama haya ya Serikali Tatu.
Nakumbuka Rais Mkapa pale Diamond Jubilee akiongea na Wazee wa Dar es
Salaam alionyesha dhahiri kuwa Serikali haikuyapenda mapendekezo yake.
Kukawa na hata mjadala kama Kamati inaweza kuja na
mapendekezo au la, maana, ikasemwa kuwa ya Kissanga haikuwa Tume. Rais
Mkapa akawashambulia pia wanahabari kwa kutaka kuishinikiza Serikali
kuyakubali mapendekezo hayo. Kitu ambacho hakiwezekani, maana, Serikali
hata siku moja haiwezi kushinikizwa na wanahabari kama haikubaliani na
inachoshinikizwa nacho. Lakini huo ulikuwa ni mwaka 2000 na sasa ni
2013. Wakati umebadilika.
Naam na tuendane na wakati unaobadilika. Tusiwe
watumwa wa historia. Tuwe na ujasiri wa kuzipa mgongo fikra za ukale.
Katiba Mpya inaweza pia kuchangia tuondokane na mambo ya ovyo ovyo na
yenye kutuvunjia heshima kama taifa.
0754 678 252, http://mjengwablog.com