Kwa ufupi
Tuna muda mfupi sana wa kuzungumza hapa,
tunaomba wote tuelekee Hospitali ya Mount Meru kuaga miili ya marehemu
kwa sababu uwanja huu umezuiwa na polisi.Arusha. Wabunge wanne wa Chadema, Said Arfi (Mpanda Mjini), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Mustapha Akunaay (Mbulu) na Joyce Mukya (Viti Maalumu) wamekamatwa wakituhumiwa kuhusika na mkusanyiko usio halali kwenye Uwanja wa Soweto jana.
Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul
Chagonja alisema jana kwamba pamoja na wabunge hao pia wamewakamata watu
wapatao 60 kutokana na vurugu zilizozuka jana baada ya Polisi
kuwatawanya kwenye uwanja huo waliokuwa wamekusanyika kuomboleza vifo
vya watu watatu; Judith Moshi, Ramadhan Juma na Amir Ally waliofariki
kwenye mlipuko wa bomu uliotokea kwenye uwanja huohuo, Jumamosi
iliyopita.
Mbali ya viongozi hao, alisema wanawasaka Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
“Tunawasaka wabunge ili tuwajumuishe na watu hawa
kwa kosa la kuhusika na mkusanyiko usiokuwa halali. Hadi sasa
tumefanikiwa kulinasa gari la Mbowe,” alisema Chagonja.
Pia kamatakamata hiyo imemkumba Mpigapicha wa
Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Ashraf Bakari. Polisi
walilazimika kutumia nguvu kuwatawanya waombolezaji hao.
Awali, Kamishna Chagonja alisema jana asubuhi kuwa
wamelazimika kuzuia viwanja hivyo kutumika baada ya wamiliki wake, AICC
kuzuia shughuli za Chadema kwenye eneo lao.
Kamishna Chagonja aliwaonyesha waandishi wa habari
barua aliyosema imeandikwa na uongozi wa AICC kuzua Chadema kuendelea
kuutumia Uwanja wa Soweto.
Mabomu yarindima
Dalili za kuzuka kwa vurugu zilianza kuonekana
asubuhi baada ya polisi kuzingira uwanja huo na kuzuia watu waliokuwa
wameanza kufurika katika eneo hilo kuanzia saa moja kuingia kwa ajili ya
maombolezo.
Wakati Polisi wakiwa uwanjani, wananchi walijaa nje ya uwanja na kuonekana kama wamewazingira.
Viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mbowe
waliwasili uwanja hapo yapata saa nane mchana na kukuta zuio hilo na
kuanza kuzungumza na wananchi ingawa FFU walikuwa wakiwataka watu
kutawanyika. Mabomu yalianza kurindima wakati Arfi aliposimama na
kuwahimiza wananchi kuelekea Hospitali ya Mount Meru kwa ajili ya kuaga
miili ya marehemu.
“Tuna muda mfupi sana wa kuzungumza hapa, tunaomba
wote tuelekee Hospitali ya Mount Meru kuaga miili ya marehemu kwa
sababu uwanja huu umezuiwa na polisi,” alisema Arfi kabla ya kukatishwa
na milipuko ya mabomu.
Awali, Lissu ambaye pia ni Mwanasheria wa Chadema alitoa msimamo
wa chama hicho kuwa Mwenyekiti wao, Mbowe na Lema hawatatoa ushahidi wa
tukio la bomu wala kujisalimisha polisi kwa sababu hawana imani na
jeshi hilo.
“Namtaka Chagonja atangulie mahakamani, tutakutana
hukohuko. Mbowe na Lema hawatatoa ushahidi wala kujisalimisha
polisi...” alisema Lissu na kuongeza:
“Kisheria haiwezekani polisi ambao ndiyo watuhumiwa ndiyo wadai kukabidhiwa ushahidi ili wauharibu.”
Mapema Kamishna Chagonja aliwataka Mbowe na Lema
kutoa ushahidi wa polisi kuhusika na tukio la kurusha bomu kwenye
mkutano wa Chadema la sivyo polisi watatumia sheria kuwalazimisha
kufanya hivyo.
Hekaheka
Baada ya polisi kuanza kutupa mabomu saa 8.45
mchana, wabunge, viongozi waandamizi wa Chadema na watu waliokuwa
wamekusanyika walilazimika kutimua mbio.
Watu walioshuhudia tukio lile wanasema viongozi
hao akiwamo Mbowe na mwenzake Lissu walikimbilia kwenye magari yao. Lema
alilazimika kukimbilia kwa wachoma nyama ya nguruwe, (kitimoto) kwenye
maeneo ya Kaloleni.
Kabla ya polisi kurusha bomu mahali alipokuwapo Lema, mbunge huyo alisikika akisema:
“Jaribuni kuvumilia, tunajaribu kuwasiliana
Serikali ya Mkoa, ili watupe kibali cha kuleta miili ya wapendwa wetu
hapa, kuweni wastaarabu kwa sababu mbele yetu kuna wana usalama ambao
wanalinda amani, ingawa kufa ni kufa tu, wenzetu wameshakufa na sisi ipo
siku tutakufa, lakini kila anayetangulia lazima tumzike kwa heshima
zote.”
Kauli hiyo iliwachefua polisi ambao walishatangaza
amri ya watu kutawanyika katika viwanja hivyo na kwamba hakutakuwa na
suala la kuaga miili ya watu hao katika eneo hilo. Ghasia hizo
zilisababisha kusimama kwa shughuli za biashara na kijamii kwa muda
jijini Arusha huku watu waliokuwa katika nyumba zilizokuwa karibu na
maeneo yalikorushwa mabomu wakilazimika kutoka nje kupata hewa safi
baada ya nyumba hizo kujaa hewa ya mabomu.
Polisi waliokuwa wakirusha mabomu waliwakimbiza
wananchi hadi maeneo ya Sakina huku wakiendelea kufyatua mabomu kila
walipoona mkusanyiko wa watu.
Katika eneo la Kaloleni, mkabala na Ofisi ya
Mtendaji wa Kata hiyo baadhi ya wafuasi wa Chadema walichoma matairi
barabarani na kusababisha ifungwe. Pia walichoma matairi katika eneo la
Mianzin
Katika eneo la Tanki la Maji, Barabara ya kwenda Moshi, baadhi
ya wafuasi wa Chadema walipanga mawe barabarani na kusababisha
msongamano wa magari.
Katikati ya jijini Arusha barabara zilikuwa hazipitiki kutokana na nyingine kufungwa na kusababisha usumbufu mkubwa.
Waandishi nao matatani
Katika vurugu hizo, baadhi ya waandishi wa habari
walishambuliwa na polisi. Hao ni pamoja na Mwandishi Mwandamizi wa
Gazeti dada la The Citizen, Zephania Ubwani ambaye kabla ya kuchomoka
katika mikono ya askari, alikuwa akiwaonyesha kitambulisho chake cha
kazi.
Hata hivyo, askari hao walimtishia kumtandika na kisha kumwambia aondoke katika eneo hilo kwa kuwa haijalishi yeye ni nani.
Mwingine ni mwandishi wa gazeti la Nipashe,
Cnythia Mwilolezi ambaye alilazimika kuacha viatu na vitendea kazi vyake
katika Uwanja wa Soweto na kukimbilia kwenye moja ya nyumba zilizopo
jirani na eneo la tukio.
Katibu Msaidizi wa Klabu ya Waandishi wa Habari
Mkoa wa Arusha, Moses Kilyinga alipigwa na polisi baada ya kuonekana
akichukua maelezo.
Kilyinga ambaye alishambuliwa na askari hao
alisema mara baada ya askari hao kumkamata, alijitambulisha lakini
hawakumwelewa na wakaendelea kumchapa kabla ya kufanikiwa kuchomoka.
Polisi wavamia hospitali
Wakati baadhi ya majeruhi wakidai kushuhudia
polisi wakiwapiga risasi watu waliokuwa wakimkimbiza mtu aliyerusha bomu
katika tukio la Jumamosi, askari hao juzi walifika katika Hospitali ya
Seliani saa mbili usiku wakitaka kumchukua mmoja wa majeruhi kwa
mahojiano kuhusiana na tukio hilo. Hata hivyo, hawakufanikiwa baada ya
mgonjwa kutokomea kusikojulikana baada ya kupata taarifa za kutaka
kuhusishwa na tukio hilo.
Ingawa si polisi wala Chadema waliokuwa tayari
kumtaja mgonjwa huyo, inaelezwa kwamba majeruhi anayesakwa ni Abdallah
Alila aliyekaririwa na vyombo vya habari jana na juzi akidai kumshuhudia
aliyerusha boma akiondoka kwenye moja ya magari ya polisi.
Hata hivyo, Kamishna Chagonja jana alisema kwamba jeshi lake linapenda kushirikiana na raia kupata taarifa na si kutumia nguvu katika kukusanya ushahidi wake.
Chanzo : mwananchi newspaper
Hata hivyo, Kamishna Chagonja jana alisema kwamba jeshi lake linapenda kushirikiana na raia kupata taarifa na si kutumia nguvu katika kukusanya ushahidi wake.
Chanzo : mwananchi newspaper