Monday, 17 June 2013

CCM yazoa viti vingi vya udiwani

                  
Nassari 


Posted  Jumatatu,Juni17  2013  saa 8:21 AM
Kwa ufupi
Nassari alivamiwa, kupigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali mwilini na watu wanaodaiwa kuwa viongozi na wafuasi wa CCM.
Chaguzi ndogo za udiwani zilizofanyika sehemu mbalimbali ziligubikwa na vurugu wakati hali ilikuwa mbaya zaidi huko Makuyuni mkoani Arusha ambako Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari alipigwa na wafuasia wa CCM na kulazimika kulazwa hospitalini.
Pamoja na vurugu hizo, CCM iliendelea kudhihirisha umwamba wake katika ulingo wa siasa baada ya kujizolea viti vingi vya udiwani wakati wa chaguzi ndogo zilizofanyika sehemu mbalimbali nchini.
Wafuatiliaji wa mambo ya kisiasa walikuwa wanafuatilia kwa kina chaguzi hizo ili kupima joto la kisiasa nchini.
Uchaguzi uliokuwa unasubiriwa kwa hamu ni ule wa Makuyuni wilayani Monduli ambako Mbunge wake ni mwanasiasa maarufu Edward Lowassa.
CCM iliibuka kidedea huko Makuyuni na kufanya maneno ya Rais Jakaya Kikwete kuwa Lowassa ana misuli ya kuifanya CCM ishinde huko Monduli.
Lowassa alikuwa na kibarua cha kukabiliana na Chadema waliokuwa wanataka kujipenyeza Monduli ambako hawajahi kuwa na kata tangu mfumo wa vyama vingi uanzishwe.
Hata hivyo, bado CCM haijapata dawa ya ushindi Pemba kwani kilishindwa vibaya na CUF kwenye uchaguzi wa ubunge wa Chambani.
Chadema kwa upande wake kilitoa changamoto kwa CCM katika chaguzi hizo za kata na hata kujizolea kata mbili za Iyela huko Mbeya na wilayani Hanan’g huko mkoani Manyara.
Nassari apata kichapo Makuyuni
Nassari alivamiwa, kupigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali mwilini na watu wanaodaiwa kuwa viongozi na wafuasi wa CCM, akiwa katika harakati za uratibu wa shughuli za upigaji kura za udiwani katika Kata ya Makuyuni, wilayani Monduli.
Nassari aliyekuwa wakala mkuu wa Chadema katika kata hiyo alivamiwa na kundi la watu zaidi ya 30 waliomshambulia kwa fimbo na
Tukio hilo lilitokea jana kati ya Saa 3:00 na 4:00 katika kituo cha kupigia kura cha Kwa Zaburi wakati mbunge huyo alipofika kuangalia maendeleo ya zoezi la kura.

“Mara nilipofika kwenye kituo kile nilikutana na kundi kubwa la vijana wa CCM waliokuwa wamejifunika mashuka ya Kimaasai wakiwa na fimbo mikanoni ambao walinizuia kuingia kituo cha kura, lakini askari na wasimamizi wakaniruhusu baada ya kuwaonyesha kitambulisho cha wakala mkuu,” alisema Nassari
Akizungumza kwa njia ya simu akiwa hospitali ya Seliani Jijini Arusha alikokimbizwa kwa matibabu, Nassari alisema vijana hao wa CCM walimsubiri nje ya kituo na kumvamia mara alipotoka nje na kuanza kumshambulia kwa fimbo na marungu kila sehemu ya mwili.
“Kama siyo kukabiliana nao na kupata upenyo wa kukimbilia bastola yangu niliyoiacha kwenye gari, nadhani ningekuwa marehemu sasa. Nimetokwa na damu nyingi puani na mdomoni. Pia nasikia maumivu makali ya kichwa na kifua,” alisema Nassari
Pamoja na Nassari, kiongozi mwingine wa Chadema aliyeshambuliwa na vijana wa CCM hadi kuokolewa na polisi ni katibu wa chama hicho Wilaya ya Monduli aliyejulikana kwa jina la Thomas Kipese.
Makuyuni (Arusha)
Mgombea wa CCM, Goodluck Lekurunya alipata kura 1547 wakati Josephat Sironga wa Chadema alipata kura 302.
Iyela (Mbeya)
Mgombea wa Chadema, Charles Mkela naye aling’ara kwenye uchaguzi wa kata ya Iyela baada ya kujizolea kura 1918, Richard Shangwi wa CCM alifuatia baada ya kupata kura 1163, Kapaga Mwakibete (NCCR) kura 17, Amosi Mwambagi (DP) kura 20
Dongobesh (Manyara)
Mgombea wa Chadema, Ernest Jorojik aliibuka mshindi baada ya kujizolea kura 1,500 akifuatiwa na Josep Barabojika wa CCM (900), Amon Akonaay wa CUF(123). Walikuwa wawania kuchukua nafasi ya Daniel Siasi aliyefariki dunia.
Bashneti (Manyara)
Msimamizi wa uchaguzi, Julius Lawi alitangaza mgombea wa Chadema, Lawrence Surumbu Tara, alipata kura 2008, Nicodemus Gwandu wa CCM alipata 1,130 na Alloyce Gwandu wa NCCR (253).

Ibugugile (Dodoma)
Leonard Eliya Kagoa (CCM) alichaguliwa kuwa diwani mpya wa katia ya Ibubugile baada ya kupata kura 733 akifuatiwa na Julius Francis Chawenda (Chadema) kura 170 na Aman Madagadi (APPT-Maendeleo) kura sita.
Stesheni (Mtwara)
Msimamizi msaidizi wa uchaguzi, Hassan Masoud alitangaza kuwa CCM imetetea kiti hiki cha Stesheni kilicho wilayani Nachingwea baada ya kura 806 na waliomfuatia ni Ally Luhundu (Chadema) kura 327, Athumani Msauna (CUF) kura 480 na Zawadi Ligawa (ADC) kura 48.
Genge (Tanga)
Steven Mlaguzi wa CCM ameshinda baada ya kupata kura 347, Joseph Komba (Chadema) kura 326, Oledi Abdulrahman (CUF) kura saba.
Tingeni (Tanga)
Aisha Mohamed wa CCM aliibuka kidedea baada ya kupata kura 362, Omar Salim (Chadema) kura 244 na Ramadhan Yahya wa CUF kura nne.
Mimeta (Morogoro)
Athumani Kapati (CCM) alishinda udiwani baada ya kupata kura 1154 na kumshindi wa Michael Madili wa Chadema alipata kura 1004.
Mbalamaziwa (Iringa)
CCM iliibuka kidedea baada ya kupata 1642 na yule wa Chadema aliambulia kura 185.

Iseke (Singida)
Emmanuel Jingu wa Chadema aliibuka kidedea kwenye uchaguzi wa kata hiyo.
chanzo : mwananchi news paper