Kwa ufupi
Tido Mhando ni miongoni mwa watangazaji wa radio
wakongwe Afrika ya Mashariki. Tangu mwishoni miaka ya 1960, jina la Tido
Mhando limekuwa maarufu katika kanda hii kama mtangazaji wa muziki,
michezo na baadaye habari na matukio.
Tido Mhando ni miongoni mwa watangazaji wa radio
wakongwe Afrika ya Mashariki. Tangu mwishoni miaka ya 1960, jina la
Tido Mhando limekuwa maarufu katika kanda hii kama mtangazaji wa muziki,
michezo na baadaye habari na matukio. Ndani ya simulizi zake hizi za
kila Jumapili, Tido anasimulia baadhi tu ya mambo aliyokutana nayo
katika kipindi chake hicho. Jumapili iliyopita aliendelea kusimulia
kuhusu maandalizi yake ya safari ya kwenda New Zealand kwenye michezo ya
Nchi za Jumuiya ya Madola ya 1974. Maandalizi ambayo yaliingia dosari
kiasi wakati ilipofahamika kwamba isingewezekana kwa RTD kutuma
watangazaji wawili kwenye michezo hiyo kama ilivyokuwa imetarajiwa. SASA
ENDELEA…
Haikuwa rahisi kupokea kauli ile ya Naibu
Mkurugenzi, Sammy Mdee, kwamba kwa sababu ya uhaba wa fedha imelazimika
mimi pekee niende kwenye michezo hiyo ya New Zealand badala ya
kuambatana na mtangazaji mwenzangu Abdul Omar Masoud.
Tulikaa kimya kwa muda, lakini hatimaye, Masoud
alinishika mkono na kunitakia kila la kheri. Tulijaribu kutafakari
kuhusu uamuzi huo na tukakubaliana kwamba bila ya shaka uamuzi wa
kunichagua mimi ulitokana na ukweli ya kwamba Masoud, mbali ya mchezo wa
mpira wa miguu, alikuwa si mzoefu sana kwenye michezo mingine kama vile
riadha na ngumi, tofauti na mimi.
Wakati tulipokuwa tukifanya mipango ya safari kwa
pamoja tulikuwa tumezungumza mengi, siyo tu kuhusu jinsi ambavyo
tungetangaza michezo hiyo, bali hata ambavyo tungevinjari pamoja huko
Christchurch. Sasa yote haya yakawa yamesukumwa pembeni. Ikanibidi
nianze kujipanga upya mwenyewe.
Nilipobakia peke yangu, niliwaza na kumsikitikia
mwenzangu Masoud. Nilifahamu ni kwa jinsi gani tungeweza kuusisimua umma
wa Watanzania kwa matangazo yetu ya pamoja, kwani sote tulikuwa
wabunifu na wachangamfu. Lakini nikajisemea mwenyewe: “Yote kwa yote,
lazima mambo yaendelee, tena kwa kasi ile ile.” Nikapania kufanya
vizuri, japo peke yangu.
Kwa kweli, niliwashukuru sana viongozi wangu kwa
kuwa na imani nami, hivyo nikadhamiria kutowaangusha hata kidogo. Lakini
zaidi, nilimshukuru Mwenyezi Mungu maana kama uamuzi ungekuwa tofauti,
ndoto yangu ya kuitumia safari hii kwa matayarisho ya harusi yangu
ambayo ilikuwa imepangwa kufanyika mara tu baada ya kurejea, ingeingia
dosari.
Hii ni kwa vile, katika kujipanga kwa maandalizi
hayo, nilikuwa nimeiona safari hii kuwa nafasi nzuri ya kujinunulia vitu
muhimu vya harusi, hasa mavazi yangu na ya mke wangu mtarajiwa.
Tulikuwa tumekubaliana na wazazi wangu kuwa pamoja
na mambo mengine, wao wangelipa mahari ambayo yalikuwa ni Sh2,000
(Shilingi elfu mbili), kiasi cha kadiri sana hasa siku hizo, hasa kwa
vile baba mkwe, Mzee Amos Mwaipopo ambaye alikuwa mzee mtaratibu sana,
hakutaka makuu ya mahari makubwa na kwamba, mimi nami ningechuku gharama
nyinginezo hasa hizo za mavazi yetu.
Kwa hiyo, nilipania kwenda kununua nguo za nguvu
huko New Zealand, hasa za bi harusi, kwa kuwa pia nilikuwa tayari
namfahamu vyema Mwangaza kwamba alikuwa mtu wa kupenda mavazi ambayo
kwayo yalikuwa yakimkaa vizuri sana.
Katika desturi za mila za Kibondei, ilikuwa
vilevile ni wajibu wangu mimi kama bwana harusi kuhakikisha ya kwamba
namvalisha bi harusi, kwani wakati wa sherehe za kimila, tungetakiwa
kutoka nje mara tatu, tukiwa tumevaa mavazi tofauti, na huku watu
wakimwangalia zaidi bi hurusi. Kwa sababu hiyo, nilitarajia kuitumia
safari hii vizuri kwa lengo hilo.
Kwa hakika siku zilikuwa zikienda haraka haraka
sana na ghafla tukajikuta tumeingia kwenye mwaka mpya wa 1974,
ikimaanisha ya kwamba siku za safari zilikuwa zimekaribia mno.
Kikosi cha wanamichezo wa Tanzania kilichokuwa
kinakwenda kwenye michezo hii kilikuwa kikubwa kiasi. Kulikuwa na
wanamichezo wengi wa riadha akina Suleiman Nyambui, Mwinga Mwanjala,
Nzael Kyomo, Norman Chihota na nyota Filbert Bayi na wengine wengi
wazuri sana.
Pia walikuwamo wachapa masumbwi wazuri tu kama vile Habibu
Kinyogoli na Emmanuel Mlundwa. Hata tulikuwa na waendeshaji wa baiskeli
waliokuwa na uhodari wa kushindana kwa kiwango cha juu kwenye mashindano
kama haya ya kimataifa ikiwa ni pamoja na George Mulamula.
Halikadhalika tulikuwa na wachezaji wa mpira wa meza (table tennis). Kwa
kweli ilikuwa timu iliyosheheni vyema.
Wote hawa walipewa nafasi nzuri ya kufanya mazoezi
ya kweli kweli huku Serikali ikiwa mstari wa mbele wa kugharimia
maandalizi haya vyema. Vilevile, wale wote ambao tulikuwa kwenye safari
hii, ikiwa ni pamoja na sisi waandishi wa habari, tulipatiwa sare
maalumu za kupendeza. Mwandishi mwingine wa habari kwenye safari hii
alikuwa ni Stephen Rweikiza aliyekuwa akiandikia gazeti la Daily News.
Tuliondoka sote kwa pamoja kuelekea New Zealand
kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Mshariki (East African
Airways) hadi Port Luis, Mauritius. Tulilala kwenye kisiwa hiki maarufu
kwa zao la miwa kwa usiku mmoja.
Nakumbuka sana wakati tulipokuwa tukielekea kwenye
hoteli hiyo tuliyopangiwa kulala tukipita kwenye ekari na ekari za
mashamba makubwa sana ya miwa, huku tukipishana na viberenge vingi
vilivyobeba malundo ya miwa iliyokatwa kupelekwa kwenye vinu vya
kutengenezea sukari.
Tuliondoka Mauritius mapema asubuhi sana kwa ndege
kubwa zaidi ya Shirika la Ndege la Qantas kwa safari ndefu ya saa kumi
na ushei kuivuka Bahari ya Pacific. Ilikuwa vizuri kwamba tulikuwa
kwenye kundi la watu wengi maana tuliweza kuchangamshana kwa kucheza
michezo kadhaa midogo midogo mle ndani ya ndege kama vile karata, ili
kupitisha muda maana hii ilikuwa safari ya kuchosha sana hii.
Tuliwasili mji wa Perth, Australia, kiza kikiwa
kimeingia. Tulikuwa tumesimama kwa muda tu hapo kubadilisha ndege ya
kutupeleka Christchurch. Nikiwa kiwanjani hapo nilianza kuona hali ya
maisha ilivyo tofauti. Niliona maendeleo makubwa ya miundombinu ya
kisasa zaidi.
Baada ya muda wa saa mbili hivi, tuliondoka Perth
na ndege ndogo kiasi ya shirika hilo hilo la Qantas kwa mkondo wa mwisho
wa safari yetu hii, tukawasili New Zealand kiasi cha saa tano usiku
tukiwa tumechoka sana.
Hata hivyo nilifurahi hatimaye kuwasili nchini New
Zealand, kwani baada ya miezi kama miwili ya kusubiri na kufanya
maandalizi mbalimbali sasa nikawa nimetua kwenye hii ya nchi ya mbali
sana. Maili elfu kadhaa kutoka nyumbani Tanzania. Kwa kweli sikuwa
nimetarajia kwamba siku moja ningeweza kufika mahali kama huko, na
mapema kiasi hicho kwenye maisha yangu ya kikazi.
Lakini pia nilifahamu kwamba nilikuwa nakabiliwa
na changamoto pamoja na kazi kubwa mbele yangu na hasa kwa kuwa sasa
nilikuwa peke yangu. Kabla ya kuondoka, nilikuwa nimefanya maandalizi
mazuri ili kuhakikisha kuwa natekeleza kazi yangu kwa kiwango cha juu.
Nilihakikisha ya kwamba nilikuwa nimekusanya kila
kitu ambacho kingeniwezesha kutoa habari kwa usahihi mkubwa. Nilisoma
vitabu na majarida mbalimbali kuhusu Michezo ya Jumuiya za Madola.
Nilifanya juhudi za kuwafahamu wanamichezo mbalimbali maarufu
watakaokuwepo kwenye michezo hiyo na kuhakikisha nawafahamu vizuri sana
wanamichezo wetu.
Halikadhalika, nilipata maelezo na maelekezo ya
kutosha ya jinsi nitakavyokuwa ninatuma habari za michezo hiyo. Tayari
kulikuwa kumefanyika mawasiliano ya kutosha baina ya RTD na wasimamizi
wa matangazo ya radio ya mashindano haya ambapo nilikuwa nimepangiwa
muda na studio maalumu wa kurusha matangazo yangu hayo.
Nilikuwa nimepangiwa kutuma kipindi maalumu cha
muda wa dakika 15 kila siku za majuma mawili ya michezo hiyo,
nikifahamisha yote yale muhimu na ya kusisimua ambayo yangekuwa
yametokea siku nzima kwenye viwanja mbalimbali.
Ili kutia ladha katika matangazo yangu hayo, nilitafuta wimbo
wangu maalumu, (signature tune) ambayo ningekuwa ninaicheza kila wakati
wa kufungua na kufunga kwa ripoti hizo. Niliutafuta wimbo huo kwa
umakini mkubwa, nikishinda kwa muda mrefu kwenye maktaba hadi
nilipofanikiwa kupata wimbo mzuri wa ala tupu uliokuwa wa kusisimua,
wenye mahadhi ya ngoma za kienyeji, uliokuwa umepigwa na bendi ya Jeshi
la Tanzania.
Kwa hakika, nilikuwa nimejipanga vizuri. Lakini
sasa tukiwa bado hapo kwenye uwanja wa ndege, baaada ya kukamilisha
taratibu zote za uhamiaji ambazo zilifanyika kwa haraka sana kwa sababu
tulikuwa wageni mashuhuri, hali ya taharuki ikanitokea baada ya kukosa
kulipata sanduku langu.
Kama desturi ya safari za ndege, nakumbuka hii
ilikuwa safari yangu ya kwanza ndefu, nililitoa sanduku hilo pale uwanja
wa ndege wa Dar na kama wengine wote tukafahamishwa ya kwamba tusiwe na
shaka yoyote tungepata masanduku yetu hayo mwishoni kabisa mwa safari.
Sasa wakati wenzangu wote walifanikiwa kupata
masanduku yao, miye langu halikupatikana hata baada ya wasimamizi wa
ndege na uwanja kufanya juhudi kubwa ya kulitafuta. Kikawa kisanga
kingine. Nikawa nawaza na kuwazua, Nikaona hii balaa.
Hata hivyo maofisa wa ndege wa Qantas walinitoa
shaka kwa kunifahamisha ya kwamba wangenipatia kiasi kizuri tu cha fedha
kuweza kununua nguo chache za kutumia huku wao wakiendelea kulitafuta
sanduku hilo.
Nilifarijika na kuondoka na wenzangu wote kuelekea
hoteli tuliokuwa tumepangiwa kufikia sisi waandishi wa habari wakati
wachezaji na viongozi wao walikuwa wanapelekwa kwenye kijiji maalumu cha
wanamichezo.
Tulipita maeneo mengi mazuri ya mji huo wa
Christchurch nikavutiwa nao sana. Mji ulikuwa umepangwa na kupangika
ukiwa na vivutio vingi vinavyokufanya upende kuishi humo. Lakini pamoja
na yote hayo, nilijua sasa kazi ndiyo imeanza.
INAENDELEA JUMAPILI IJAYO...
source: Mwananchi
source: Mwananchi