Thursday, 31 October 2013

Waziri: Mashambulizi ya tindikali ni ya kisiasa


Na Mwinyi Sadallah,Mwananchi

Posted  Alhamisi,Oktoba31  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi

Waziri huyo aliongeza kuwa, mashambulizi haya yameleta taswira mbaya kwa Wazanzibari wenyewe na Tanzania kama nchi kwani yanailenga jamii moja ambayo siku jamii hiyo ikiishiwa uvumilivu taifa linaweza kuingia katika machafuko na kuathiri kwa kiasi kikubwa amani, mshikamano wa kitaifa na utulivu visiwani hapa.


Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ), imesema mashambulizi ya kutumia tindikali dhidi ya viongozi wa dini na Serikali visiwani hapa ni utekelezaji wa mipango ya kisiasa na si sehemu ya chuki za kidini.
Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed wakati wa mahojiano maalumu na gazeti hili ofisini kwake eneo la Vugha, Zanzibar jana.
“Mashambulizi haya ya kutumia tindikali yanatokana na chuki za kisiasa na kamwe siyo dini kwani Wazanzibar kwa muda mrefu wamekuwa na tofauti za kidini lakini hapakuwahi kutokea choko choko na mashambulizi kama haya,” alisema waziri huyo.
Akizungumza kwa uchungu amesema, wanaotekeleza mashambulizi haya ni watu waovu wenye nia ya kuleta vurugu na kuivunja nchi katika vipande na tayari katika hii wanaelekea kufanikiwa kwa kuitia doa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Waziri huyo aliongeza kuwa, mashambulizi haya yameleta taswira mbaya kwa Wazanzibari wenyewe na Tanzania kama nchi kwani yanailenga jamii moja ambayo siku jamii hiyo ikiishiwa uvumilivu taifa linaweza kuingia katika machafuko na kuathiri kwa kiasi kikubwa amani, mshikamano wa kitaifa na utulivu visiwani hapa.
Amesisitiza hadi sasa tathmini ya awali inaonyesha chanzo kikuu ni kuibuka kwa vikundi vya dini vilivyojikita katika mambo ya siasa hali inayosambaratisha amani na umoja wa kitaifa uliokuwa umeanza kuimarika tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar Novemba, 2010.
Alisema baadhi ya viongozi wa dini wanaofanya kampeni za Zanzibar kujitenga katika Muungano bila ya kuangalia athari zake kwa pande zote mbili.
Waziri huyo alionya iwapo Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar utavunjika basi wanaotoka visiwani hawatabaki salama kama Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alivyowahi kuonya siku za nyuma. Waziri huyo alibainisha kuwa,faida za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni nyingi kuliko kero zinazolalamikiwa. Alizitaja faida hizo kuwa ni pamoja na fursa ya kumiliki ardhi, soko la watu milioni 40 la bara, kuishi na kufanya kazi upande wowote.

SOURCE: MWANANCHI