Kwa ufupi
Serikali inao maofisa wa elimu katika kila kata
nchini ambao wangetumika kabisa kukusanya kero za elimu na Serikali kuu
kuzifanyia kazi.Kinachoonekana sasa ni kama mpango mwingine wa
kuendeleza porojo kwa kufanya vikao vinavyotumia fedha nyingi badala ya
kuboresha elimu.
Bukombe/Dar: Hali ya elimu nchini inaonekana kuendelea kuwa mbaya licha ya ahadi nyingi za Serikali kuiboresha.
Mojawapo ya sababu za kuwepo kwa hali hiyo mbaya,
inaelezwa ni mazingira duni ya kufundishia, uhaba wa vifaa na walimu
kutoridhishwa na malipo kwa kazi wanazofanya.
Agosti 15, mwaka huu Serikali ilizindua
utekelezaji wa mkakati wa ‘Matokeo Makubwa Sasa’ katika elimu nchini,
huku sekta hiyo ikionekana kudidimia.
Elimu ni miongoni mwa sekta sita zilizochaguliwa
katika Mpango wa Serikali hivi karibuni wa kuleta Matokeo Makubwa Sasa.
Sekta nyingine ni Nishati, Maji, Miundombinu, Kilimo na Fedha. Sekta
hizi sita zimechaguliwa ziwe za mwanzo katika kutekeleza Mpango huu wa
Serikali ili kuiletea nchi matokeo makubwa kwa haraka.
Sekta hizi zinabeba msingi wa kufungulia fursa za
ukuaji uchumi wa nchi kwa ujumla na kuchochea ustawi wa maisha bora kwa
Watanzania wote.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru
Kawambwa aliyezindua utekelezaji huo, Jijini Dar es Salaam, anasema
katika sekta ya elimu, washiriki 34 kutoka taasisi 31 zikiwemo za
Serikali na zisizo za Serikali, washirika na wadau wa maendeleo ya elimu
walikutana kati ya 25 Februari hadi 05 Aprili, 2013, kutafakari kwa
kina changamoto zinazoathiri sekta ya elimu.
Changamoto kubwa iliyoainishwa ni kiwango cha
uandikishaji wa wanafunzi kimeongezeka, ubora wa elimu umeshuka, hususan
kuporomoka kwa kiwango cha ufaulu katika Elimu ya Msingi na Sekondari.
Kuboresha elimu ni kichocheo muhimu katika kuleta maendeleo nchini.
Ingawa ufaulu siyo kiashiria pekee cha ubora wa elimu, kwa sasa ni
muhimu kutumika kupima ubora wa elimu nchini kwetu.
Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne yalivyokuwa
Asilimia 60 ya watahiniwa walipata alama sifuri yaani walifeli.
Mchanganuo ni kama hivi;
Matokeo ya kidato cha nne 2012: Alama 1 (0.4%) Alama 2 (1.6%) Alama 3 (3.9%) Alama 4 (26.0%) Alama 0 (60.1%).
Baadhi ya wananchi wanasema huenda ikawa ni
mipango mizuri, cha msingi ni itekelezwe kwa vitendo. Hata hivyo baadhi
wana hofu kwamba hakuna chochote cha maana kinaweza kutokea kwa sababu
kwa staili ya sasa walimu hupatikana kutokana na waliofeli.
“Wengi wanaokwenda kusomea ualimu ni wale waliofeli. Kwa maana
hiyo hawana uwezo wa elimu na ndiyo sababu wanashindwa kufaulisha,”
anasema Mwandi Kimbwe, mkazi wa Arusha.
Mfano wa hali ya Geita
Kuna maelfu ya watoto wasiopata elimu stahiki katika vitongoji viwili vya Kijiji cha Namalandula, Bukombe mkoani Geita.
Hali hiyo imesababisha wananchi kuamua kujenga shule mbili katika vitongoji vya Ilyamchele na Mtukula.
Wanaotoa taarifa za kweli hunyanyaswa na wakubwa
Agosti 15, mwaka huu, gazeti hili liliripoti kuhusu suala hili la kutokuwepo kwa shule.
Hata hivyo ilibanika baadae kuwa uongozi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe umeanza kuwafuatilia watu waliotoa
taarifa za kuwapo kwa shule hizo huku zisizo na hadhi ukihoji “aliyetoa
ruhusa kwa waandishi wa habari kuingia katika maeneo hayo na kuandika
taarifa za shule husika”.
Wanafunzi zaidi wanufaika
Shule ya Ilyamchele ambayo sasa ina wanafunzi 600
ilianzishwa 2004 wakati shule ya Mutukula yenye wanafunzi 354
ilianzishwa 2008, zikiwa ni jitihada za kuwawezesha watoto zaidi ya 3000
waliopo katika vitongoji hivyo kupata mahali pa kusoma.
Licha ya kwamba mazingira ya shule hizo siyo
mazuri, lakini wananchi wa vitongoji hiyo wanasema walau malengo yao ya
kuwawezesha watoto kujua kusoma, kuandika na kuhesabu yanafanikiwa.
Mkazi wa Kitongoji cha Mutukula, Suzy William
anasema watoto wake wawili; Isaya William anayesoma darasa la tano na
Eliza William anayesoma darasa la tatu katika shule waliyoianzisha wana
uwezo wa kusoma, kuandika na kuhesabu tofauti na walipokuwa hawasomi.
Mkazi mwingine Elizabeth Leonard anasema kwa
kutambua umuhimu wa elimu, wamekuwa wakichanga kiasi cha Sh20,000 kwa
ajili ya kuwezesha ujenzi wa madarasa mapya tofauti na vibanda vilivyopo
sasa.
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Namalandula, Jackson
Bwire shule iliyopo katika kijiji hicho ina wananfunzi 1,300 lakini ina
upungufu wa vyumba vya madarasa 19 na walimu 11.
Kimsingi wananchi katika vitongoji hivyo
wanailalamikia Serikali kwamba imeshindwa kuwasaidia kukamilisha majengo
wealiyoanza na badala yake imekuwa ikikimbilia kufunga shule hizo
ambazo kimsingi haikuzianzisha.
Msimamo wa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Bukombe ni kwamba shule hiyo ifungwe kwani haistahili kutoa elimu
kutokana na kutokuwa na vigezo husika, lakini uongozi huo hautaki
kueleza hatma ya kielimu kwa maelfu ya watoto wa shule hizi. Ofisa Elimu
wa shule za msingi katika wilaya hiyo, Shadrack Kabanga kwa upande
mmoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bukombe, Liliani Matinga
kwa upande mwingine ni kama wanajivua wajibu kuhusu suala hilo kwa kuwa
tu hakuna shule zilizosajiliwa katika vitongoji hivi.
source: Mwananchi news paper
source: Mwananchi news paper