Na Kalunde Jamal, Mwananchi
Posted Jumapili,Oktoba13 2013 saa 11:29 AM
Posted Jumapili,Oktoba13 2013 saa 11:29 AM
Kwa ufupi
Gazeti hili lilishuhudia daktari huyo akimwelekeza
mmoja wa madaktari wa MNH namna ya kumsaidia mgonjwa wake. Kwa mujibu wa
mazungumzo yao, hali ya mgonjwa husika ilimchanganya daktari huyo,
hivyo kutaka kupata msaada kwa Dk Kishiwa.
Dar es Salaam. Huwezi kuamini lakini huu ndio
ukweli, kwamba watu kadhaa wamekuwa wakimiminika kupata msaada wa tiba,
ushauri wa kitabibu na wengine masomo ya udaktari kwa mtu ambaye
imethibitika kwamba hivi sasa ana matatizo ya akili.
Huyu si mwingine bali ni Mark Paulo Kishiwa
ambaye kitaaluma ni daktari, aliyewahi kufanya kazi Hospitali za Kasulu,
mkoani Kigoma na Bugando mkoani Mwanza, lakini sasa mvua na jua
humwishia akiwa maeneo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Ukimwona mara kadhaa utamkuta akiimba nyimbo
zisizo rahisi kuzielewa kutokana na hali anayonekana kuwa nayo ya
matatizo ya akili, lakini anapokuwa sawa, hugeuka kuwa msaada kwa wengi;
madaktari wa MNH ambao huomba ushauri kwake, wanafunzi wa Chuo Kikuu
cha Sayansi za Tiba Muhimbili (MUHAS) na wagonjwa ambao hutaka ushauri
pia.
Dk Kishiwa anasema: “Naikumbuka Aprili 26, 1981,
ilikuwa Jumatatu ya Pasaka, ndipo nilianza kuugua. Nilijikuta nikifanya
vitu visivyo vya kawaida.
Nilimwaga maji ovyo ndani, nilimwaga nguo na vitu
mbalimbali, kila kitu kilikuwa ovyo. Baada ya muda niligundua kufanya
vitu siyo vya kawaida…Hivyo ndivyo nilivyoanza kuchanganyikiwa na hali
hii imenitokea mara kwa mara.”
Aliongeza: “Yaliponitokea hayo, nilikuwa nikifanya
kazi mkoani Kigoma katika hospitali iliyopo wilayani Kasulu (hakuitaja
jina) ndipo kilikuwa kituo changu cha kazi.”
Pamoja na Dk Kishiwa kuwa na matatizo ya akili,
imethibitika kuwa baadhi ya madaktari wa MNH wamekuwa wakikimbilia kwake
kupata ushauri, lakini kubwa ni lile la kufundisha masomo ya ziada kwa
baadhi ya wanafunzi MUHAS.
Pia amekuwa akifuatwa na watu wanaomfahamu hasa
wanawake wakimwomba ushauri hata kuwaandikia dawa kutokana na maradhi
waliyonayo. Mwandishi wa habari hii ni mmoja wa waliopata ushauri wa
kitabibu kutoka kwa Dk Kishiwa.
Tiba na ushauri
Uchunguzi wa wiki kadhaa katika eneo la MNH,
nyumbani kwake Chamazi na hata katika familia yake, umethibitisha kwamba
Dk Kishiwa licha ya kuwa mgonjwa wa akili bado ni msaada mkubwa kwa
watu wengi.
Gazeti hili lilishuhudia daktari huyo akimwelekeza
mmoja wa madaktari wa MNH namna ya kumsaidia mgonjwa wake. Kwa mujibu
wa mazungumzo yao, hali ya mgonjwa husika ilimchanganya daktari huyo,
hivyo kutaka kupata msaada kwa Dk Kishiwa.
Uchunguzi pia ulibaini kuwa wakati fulani, Dk
Kishiwa anakuwa katika hali ya kawaida na kuweza kutoa ushauri, hata
kutibu kwa kuwaandikia dawa wagonjwa akiwa eneo hilo la Muhimbili.
Jioni moja gazeti hili lilishuhudia wanawake wawili waliobeba
watoto mgongoni wakiwa na Dk Kishiwa, aliyekuwa akiwaandikia kitu kwenye
karatasi. Baada ya tukio hilo mwandishi aliwauliza iwapo wanamfahamu,
na walijibu; “Tunamfahamu, ni daktari alikuwa akituandikia dawa.”
Hata hivyo, uchunguzi ulibaini kuwa mambo
yanapobadilika, Dk Kishiwa huwa mkali asiyetaka kuwa karibu na mtu au
kuzungumza naye, huku akifanya vioja vinavyothibitisha hali yake ya
matatizo ya akili. Hali hiyo ilimlazimisha mwandishi kuendelea
kumfuatilia kwa siku kadhaa katika eneo hilo la MNH na kufanikiwa
kuzungumza naye.
Kwa mujibu wa watu wanaomfahamu hasa madereva
teksi wa eneo hilo, walisema Dk Kishiwa hushinda hapo na kwamba pamoja
na kuwepo kwa wafanyabiasha na madereva wengi, daktari huyo humsikiliza
dereva mmoja anayepatana naye na mara nyingi hutekeleza anayomweleza.
Kwa msaada wa dereva huyo, Dk Kishiwa anaeleza
historia ya maisha yake kuwa alizaliwa Desemba 25, 1954, alipata elimu
katika Shule ya Msingi Tumbi mkoani Tabora hadi darasa la nane na
kuendelea na masomo kupitia shule kadhaa ikiwemo Sekondari ya Busonga na
Sekondari ya St Mary’s ya Tabora.kwamba katika elimu ya sekondari
alipata daraja A kwa masomo yote 11.
“Sikuwahi kufeli, nilipata daraja A katika masomo
yote 11 niliyosoma yakiwemo kemia, baolojia, hisabati na civics. Baada
ya hapo nilijiunga na jeshi kwa mujibu wa sheria kwa miezi sita katika
kambi ya Mafinga,” anasema Kishiwa bila kutaja miaka aliyosoma.
Anakumbuka kuwa 1974 ndipo alijiunga na Chuo cha
Tiba Muhimbili, ambapo alisoma kwa miaka mitano na kumaliza 1979, bila
kufeli somo hata moja na baada ya hapo alipangwa kwenda Hospitali ya
Bugando, Mwanza kikiwa ni kituo chake cha kazi cha kwanza.
Anasema alikaa Bugando kwa mwaka mmoja tu na mwaka
uliofuata akapelekwa Wilaya ya Kasulu, Kigoma kama Mganga Mfawidhi na
huko ndipo lilipoanzia tatizo alilonalo hadi sasa.
Itaendelea Jumapili ijayo…..
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI