Na Julieth Kulangwa, Mwananchi
Kwa ufupi
Nilishuhudia wasichana zaidi ya 35 wakitiwa mbaroni
usiku wa Septemba 27 karibu na Baa ya Kimboka, lakini nusu saa baadaye
kundi la wasichana wengine nikaliona likiwa limejipanga kuendelea na
kazi.
Sehemu ya kwanza tuliona jinsi biashara
inavyoendeshwa katika madanguro, leo simulizi inaendelea kuuelezea
mtandao wake na jinsi watu wengine wanavyoitumia kama fursa ya
kujinufaisha.
Katika sehemu ya kwanza nilisimulia wanaume ambao
huonekana nje katika nyumba hizo wakinywa pombe za aina mbalimbali
mchana kutwa.
Swali la kwanza nililojiuliza inakuaje mwanamume
mzima anakaa katika vibanda na kunywa pombe mchana kutwa. Je anapata
wapi pesa za kunununulia pombe au kuitunza familia yake?
Jibu nililopata ni kuwa wanaume hawa wengi ni
madalali, ambao huwatafutia wasichana wateja pia huwatafutia wasichana
wazuri wateja wa kiume.
Yaani hawa wanaume wanaweza kuingia mkataba na
wanawake au wasichana wa kuwatafutia wanaume, na wao hupata kitu kidogo
na hapa ndiyo hupata pesa za kunywa pombe.
Pia mwanamume anapokuja na kutaka mwanamke mzuri
na mwenye usalama huwatumia madalali hawa. Wanasema hufanya hivi
kujihakikishia usalama kwa kuwa wanawake wengine huwaibia wateja wao na
ikitokea hivyo basi mteja humfuata dalali ambaye humsaidia kuvipata vitu
vyake, kwa kuwa wao wanawajua wasichana wote wanaofanya biashara hiyo.
Mwanamke mmoja anayejiuza katika maeneo ya
Buguruni Madenge, anasema wanaume hawa ni kiungo muhimu katika biashara
hiyo hasa wakati wa mchana.
“Wanaume wengi huwa wanahitaji usalama zaidi
wakati wa mchana kwa sababu ni lazima muingie ndani, sasa huwa wanaogopa
labda tunaweza kuwabadilikia ndiyo maana huwa wanawatumia hawa ili wawe
na uhakika,” anasema mwanamke huyo.
Anasema madalali wameingia katika biashara hiyo
baada ya kukithiri vitendo vya kuwasingizia wateja, ambavyo hufanywa na
makahaba kama vile kuwasingizia hawajawalipa hata kabla ya kufanya tendo
lenyewe.
Anaongeza kuwa wakati wa usiku biashara hiyo
inaweza kufanyika ‘chapchap’ hata katika vichochoro au kwenye gari
lakini mchana ni lazima watafute faragha.
Aidha, anasema usipokuwa na uhusiano mzuri nao
wanaweza kukuharibia kwa mteja wako, pale watakapokukuta naye kwa
kumwambia maneno mabaya ili akuache amchukue mtu wanayemtaka wao.
Buguruni usiku
CHANZO: MWANANCHI
Mitaa hii hasa karibu na Barabara ya Mandela na Uhuru, wanawake
hawa wanaonekana pembeni wakiwa wamejipanga kila mmoja kwa ‘pozi’ lake.
Tofauti na wale wanaojiuza katika ‘Club za Usiku’
na makasino ambao huvalia nadhifu na nusu utupu, hawa huvalia kawaida,
wengine chini wamejifunga vitenge au khanga.
Wasichana wa chini ya miaka 15 na wanawake wenye
zaidi ya miaka 35 wakiwa na nywele zisizo na matunzo na mavazi
yasiyovutia, wanaonekana katika barabara hizi wakijiuza.
Nyumba za kulala wageni katika mitaa hii ambazo
zipo mpaka zenye vyumba vitatu zinafurika, siyo wageni wa kulala bali
wale wa ‘chapchap’ na wengine wanaonekana kwenye foleni wakisubiri
wengine watoke ili na wao waingie.
Wamiliki wa nyumba hizo za kulala wageni huwatoza
kiasi cha Sh2,000 kwa muda wa dakika kumi, zikiisha mgeni hugongewa
atoke au aongoze pesa nyingine ili aendelee kwa dakika kumi zaidi.
Pia simulizi ya leo inaelezea upande mwingine wa
biashara hii, kwa wale ambao wanajitegemea kwa kupanga katika makazi ya
kawaida au nyumba za kulala wageni.
Siyo kuwa wanawake wote wanaojiuza Buguruni
wanaishi kwenye madanguro, wengine wamepanga katika makazi ya kawaida na
wengine wanaishi katika nyumba za kulala wageni.
Wenye nyumba wanasema siyo rahisi kujua anayekuja
kupanga kama anafanya biashara hiyo au la, lakini pia wanasema si rahisi
kuthibitsha hilo kwa kuwa hawawaleti wateja wao katika nyumba
walizopanga.
Mmiliki mmoja wa nyumba maeneo ya Buguruni kwa
Mnyamani (Jina tunalihifadhi), anasema siyo rahisi kujua kazi anayofanya
mpangaji wako na hata hivyo anachoangalia ni pesa yake ya pango tu.
“Kama mtu anafanya biashara hiyo na hawaleti
wateja wake nyumbani kwangu, mimi nina sababu gani ya kukataa kodi yake
wakati mimi ninachotaka ni mpangaji tu,” anasema mwanamke huyo.
Hata hivyo, wapo wanaokerwa na tabia za wenzao
wanaowapangisha wanawake wanaojiuza, wakisema kuwa wanashusha hadhi ya
maeneo wanayoishi.
Wengine wanaichukulia biashara hii kama fursa ya
kujinufaisha kwa kuwapangisha huku wakiwapa sharti la kulipa kodi kwa
siku, kitu ambacho wanasema kinalipa tofauti na yule anayelipia pango
kwa mwezi.
“Wasichana hawa kwa kuwa wengi hawana uhakika wa maisha yao,
hupendelea nyumba za kulipia pango kila siku, huwa tunawatoza Sh3,000
mpaka Sh4,000 kwa siku, hii inatulipa kuliko mpangaji anayetaka akulipe
kodi ya mwezi ambayo haizidi elfu ishirini,” anasema mwanamume mmoja
anayemiliki nyumba katika eneo la Buguruni Madenge.
Aidha, anasema hii inawaondolea adha ya kusumbuana
na wapangaji wanaolipia kodi ya mwezi, kwani huwa hawana uhakika
ukilinganisha na wapangaji wa aina hii.
Zainab Zubeir anasema kukithiri kwa wanawake
wanaojiuza katika maeneo wanayoishi, kumeshusha na kuwatia doa wanawake
wote wa eneo hilo.
“Mimi leo hii ninaona aibu kumwambia mtu ninatokea
Buguruni kwa sababu ukimtajia mtu hivyo moja kwa moja anakuhusisha na
biashara ya ukahaba, natamani ningekuwa na uwezo wa kuwaondoa watu hawa
huku,” anasema Zainab.
Hata hivyo mara kwa mara serikali imekuwa ikifanya
jitihada za kuwakamata na kuwaondoa wanawake hawa katika eneo hili,
kutokana na kuwa na mtandao mkubwa juhudi hizo zimeshindwa kuzaa
matunda.
Nilishuhudia wasichana zaidi ya 35 wakitiwa
mbaroni usiku wa Septemba 27 karibu na Baa ya Kimboka, lakini nusu saa
baadaye kundi la wasichana wengine nikaliona likiwa limejipanga
kuendelea na kazi.
CHANZO: MWANANCHI