Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Posted Jumatano,Oktoba30 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumatano,Oktoba30 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Dar es Salaam. Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeibuka na kujibu tuhuma
zilizotolewa katika mitandao ya kijamii na Mwenyekiti wa chama hicho
mkoani Arusha, Samson Mwigamba, zilizosababisha hadi kusimamishwa
wadhifa wake kwa muda usiojulikana, kikieleza kuwa hazina ukweli wowote.
Katika andiko lake kwenye mtandao, Mwigamba
anadaiwa kuwatuhumu viongozi wa juu wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa
Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Wilbrod Slaa kuwa wamechakachua
katiba ya chama hicho kuhusu ukomo wa nafasi za uongozi ili kujinufaisha
binafsi.
Mwigamba alisimamishwa katika Mkutano wa Baraza la
Uongozi la chama hicho Kanda ya Kaskazini siku tatu zilizopita
akituhumiwa kusema uongo, kupotosha taarifa za chama na kuchonganisha
viongozi kupitia mtandao wa kijamii wa Jamii Forums.
Mbali na kujibu tuhuma hizo, chama hicho kimesema
kauli zinazozidi kutolewa na Mwigamba katika vyombo vya habari ni
kinyume na Katiba ya chama hicho ambayo inaeleza kuwa, kama mwanachama
ana jambo au malalamiko anatakiwa kuwasilisha katika vikao vya ndani vya
chama.
Taarifa iliyotolewa na chama hicho jana ilieleza
kuwa, Mwigamba alitoa taarifa mbili zinazokinzana akiwa katika kikao cha
chama hicho mkoani Arusha na wakati akiwa katika mkutano wa baraza
hilo.
“Kwanza alikana kuwa hakuandika chochote katika
mitandao ya kijamii, lakini juzi wakati akizungumza na wanahabari
alikiri wazi kuwa, waraka aliouandika ulikuwa wake,” ilieleza taarifa
hiyo iliyosainiwa na Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa, hakuna kiongozi
yeyote wa chama hicho aliyebadili vifungu vya katiba ya chama hicho na
kwamba katiba hiyo iliandikwa upya mwaka 2006 na haikufanyiwa
marekebisho kama ambavyo amedai Mwagimba.
Imeelezwa kuwa maoni yaliyotolewa na kiongozi huyo
aliyesimamishwa kuhusu katiba kuvunjwa yana maswali mengi, kwa sababu
yametolewa na mtu anayejua kila kinachoendelea ndani ya chama hicho.
Katika hatua nyingine, Diwani wa Kata ya Nyasura
wilayani Bunda kwa tiketi ya Chadema, Zamberi Ngobayi (68) amefariki
dunia usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando Mwanza
alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya kiharusi uliokuwa ukimsumbua kwa muda
mrefu.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI