Na Goodluck Eliona, Mwananchi
Posted Jumapili,Oktoba27 2013 saa 7:52 AM
Posted Jumapili,Oktoba27 2013 saa 7:52 AM
Kwa ufupi
Mwenyekiti wa Umoja wa Watendaji Wakuu wa
Makampuni Tanzania (CEOrt), Ali Mufuruki, anasema hatua iliyochukuliwa
na serikali itawaathiri wananchi pamoja na kampuni za kigeni ambazo
zilikuwa tayari kushirikiana na wafanyabiashara wa ndani.
Dar es Salaam. Wadau wa gesi
nchini wameendelea kupinga uamuzi wa Serikali kuwaweka kando kushiriki
kwenye uchimbaji wa gesi, badala yake kuwakilishwa na Shirika la
Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC).
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti
wa Umoja wa Watendaji Wakuu wa Makampuni (CEOrt), Ali Mufuruki alisema
hatua iliyochukuliwa na serikali itawaathiri wananchi pamoja na kampuni
ya kigeni ambayo yalikuwa tayari kushirikiana na wafanyabiashara wa
ndani.
“Hata wale watu wa nje ambao walikuwa wameanza
kuwahusisha watu wa ndani watakuwa wameanza kujiuliza kuhusu uamuzi wao
kwamba hivi tulifanya uamuzi wa busara kuwa husisha hawa, mbona viongozi
wao wanasema hawafai? Hii si sawa,” alisema Mafuruki na kuongeza:
“Hakuna nchi duniani ambayo imesimama na kusema kuwa watu wa ndani wasihusike kwasababu hawana uwezo, pesa na ni mafisadi.”
Kauli ya watendaji hao inakuja siku chache baada
ya Mwenyekiti wa Mfuko wa Sekta Binafsi (TPSF), Dk Reginald Mengi
kupinga msimamo wa serikali kuwa wafanyabiashara wa ndani hawana uwezo
wa kuchimba gesi kutokana na kuwa na mitaji midogo.
Pia Mafuruki alipinga ufafanuzi uliotolewa juzi na
Rais Jakaya Kikwete kuwa sekta binafsi itafuata masharti sawa na
wawekezaji wa nje na kusema kuwa hatua hiyo inalenga kuwakandamiza
wazawa.
“Haiwezekani sera ambayo inasimamia uendelezwaji
wa hii sekta ikawa inasema kwamba wawekezaji wa nje na ndani wawe sawa,
hakuna kitu kama hicho,” alisema.
Alisema utafiti unaonyesha kuwa nchi za Saudi
Arabia, Marekani, China, Nigeria, Malaysia na Norway zinatoa kipaumbele
na ulinzi kwa wawekezaji wa ndani katika sekta ya madini na nishati
kutokana na umuhimu wake katika kukuza uchumi wa nchi.
Mwenyekiti huyo alisema TPDC haina uwezo wa
kushiriki uchimbaji wa gesi, ila imepewa nafasi hiyo kwa kuwa ni shirika
la umma na kwamba sheria inataka iwe hivyo.
“Kwa nini Serikali ibague, au kwasababu TPDC ni
shirika la umma? Sawa wao washiriki lakini na sekta binafsi waruhusiwe…
kutumia kampuni moja ni kujiweka kwenye hatari, kwa sababu linaweza kufa
na hakuna ambaye anaweza kuniambia haiwezi kufa,” aliongeza.
Alipendekeza kuwepo kwa sheria za upendeleo kwa wazawa katika sekta mbalimbali ili kuwanufaisha wadau wengi zaidi.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt, Santina
Benson alisema lazima serikali ijifunze kutokana na makosa kwa kuangalia
sera ya madini ambayo imeshindwa kuwanufaisha Watanzania wote.
“Hatuwezi kuiacha historia ijirudie yenyewe. Tunahitaji
kuangalia nyuma miaka 20 iliyopita wakati sera ya madini ilipokuwa
inatungwa.
Watanzania hawajanufaika nayo huku wengi wakiwa bado wanaishi chini ya mstari wa umaskini,” alisema na kuongeza kuwa:
“Ni ukweli uliowazi kwamba sera ya madini
ilishindwa kulinda rasilimali za Watanzania kwa hiyo safari hii lazima
tuhakikishe tunafanya vizuri.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI