Monday, 28 October 2013

Kauli ya JK kuhusu CCM yaibua mengi

28th October 2013

Rais Jakaya Kikwete
Kauli  ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, kwamba chama hicho kina wakati mgumu kushinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kutokana na kushamiri kwa rushwa, imeibua mjadala miongoni mwa jamii.

Akifunga mafunzo maalumu ya watendaji hao wa CCM wa wilaya na mkoa mjini Dodoma wiki iliyopita, Rais Kikwete alisema tatizo la rushwa lisipodhibitiwa ndani ya chama hicho, hakitashinda katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 au ule wa 2020.

PROFESA BAREGU

Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa toka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut), Profesa Mwesiga Baregu, alisema kauli aliyoitoa Rais Kikwete ni ya kijasiri.

“Kwa sababu kama kuna mtu anayekijua chama chake ni Mwenyekiti, na kwa hali hiyo Rais Kikwete si kwamba ameiona tu rushwa ilivyo ndani ya chama chake, bali pia ameiishi ndani ya chama hicho,” alisema.

Alisema Rais Kikwete alishawahi kusema huko nyuma kuwa wale wanaoitabiria CCM kufa kutokana na rushwa, watatangulia wenyewe.

Alisema kwa hali hiyo, ya Rais Kikwete kujitokeza hadharani sasa na kukiri wazi wazi kuwa rushwa inaweza kuiondoa CCM madarakani, ni kitendo cha kishujaa ingawa muda uliobakia kabla ya uchaguzi ni mfupi.

Akizungumzia hatua ya Rais Kikwete kukasimu madaraka kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Tanzania bara, Philip Mangula, ya kushughulikia suala la rushwa ndani ya chama hicho, Profesa Baregu alisema hicho ni kitendo cha kutapatapa.

“CCM walikuja na zoezi la kujivua gamba ambalo lilikuwa likisimamiwa na huyu huyu Mangula akisaidiana na Nape Nnauye, ambao waliahidi ndani ya miezi sita, matokeo yangeonekana, lakini haikuwa hivyo,” alisema.

Alisema kwa Rais kusema CCM itaanguka isipoweza kubadilika, ni lugha ya kiuongozi zaidi kwa kuwa kwa hali ilivyo ndani ya CCM, rushwa haiwezi kumalizika ndani ya kipindi kifupi kilichobakia, kabla ya uchaguzi,” alisema.

MHADHIRI UDSM

Naye Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally, alisema kauli hiyo ya Rais ni ya msingi, lakini ina mtizamo finyu, kwa kuwa inaangalia kuanguka kwa CCM, badala ya kuangalia mustakabali wa nchi.

“Kwangu mimi sina tatizo la rushwa kuiangusha CCM na nchi ikabaki salama, lakini tatizo ni kwamba, hali ya rushwa ilivyo hivi sasa haiiweki tu CCM shakani, bali nchi nzima,” alisema.

Alisema rushwa kwa sasa nchini imeshapenya katika mwili mzima wa nchi kiasi kwamba hakuna sehemu iliyo salama, si polisi, mahakamani, ardhi na kwingineko.

Alisema mjadala unapaswa kujikita si kwa kuangalia kusambaratika kwa chama, au madhara ya rushwa na kushindwa kwa chama, bali unapaswa kuangalia chanzo cha rushwa na kwa nini taifa limeshindwa kuiondoa.

“Tujadili chanzo cha rushwa na ni akina nani wako nyuma ya rushwa nchini, kwamba pamoja na juhudi zote zilizofanyika za kupambana na rushwa, kama kutunga sheria, lakini bado rushwa ipo,” alisema.

Alisema kama taifa limefanya mengi, kama kutunga sheria mbalimbali ikiwamo ile ya fedha wakati wa uchaguzi, kuanzisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) na asasi mbalimbali dhidi ya rushwa, lakini bado imejikita.

Alisema mjadala unapaswa kuangalia kitu hasa kilichosababisha rushwa ishindikane kuondolewa, na si rushwa kuiondoa CCM madarakani, kwa sababu kama rushwa itaendelea kuwapo hata baada ya CCM kuondoka, itaendelea kuwapo hata chama kingine kikiingia madarakani.

RAIS TLS

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stolla, alisema kauli iliyotolewa na Rais Kikwete si ngeni kwa sababu hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alishawahi kuitoa.

“Mwalimu aliwahi kuwaonya CCM kule Dodoma kwamba wasipowatumikia wananchi ipasavyo, rais anaweza kutoka upinzani,” alisema.

Alisema hata alichoonya Rais Kikwete ni kile kile cha madhara ya rushwa, kwamba rushwa ni adui wa haki na ikiendelea kuachwa inakuwa tatizo kwenye huduma za jamii zilizo na uhusiano wa moja kwa moja na wananchi.

Alisema wananchi wakichoshwa na rushwa, wataangalia chama mbadala na hivyo kuinyima kura CCM.

KUGA MZIRAY
Baraza la Vyama vya Siasa nchini, limeitaka Takukuru kumsaidia Rais Kikwete kupambana na rushwa ndani ya CCM.

Mwenyekiti wa baraza hilo, Peter Mziray, alisema kutokana na kauli hiyo ya Rais Kikwete, Takukuru wachukue hatua ya kuwashughulikia viongozi na wanachama wa CCM wanaojihusisha na rushwa kwa kuanza na wanachama walionza kampeni kabla ya wakati.

“Baraza linampongeza Rais Kikwete kwa kuwa mkweli katika suala hili, watu wengine wanaweza kumlaumu kwa kuwa ametoboa siri,” alisema.

Mziray ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha APPT-Maendeleo, alisema Watanzania watambue kuwa mtu yeyote anayeshinda uongozi kwa rushwa, ni hatari hawezi akapambana na rushwa katika serikali atakayoiunda.

MCHUNGAJI

Askofu wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of God Tanzania, Daniel Awet, alisema kuwa kutokana na viongozi wa CCM kujihusisha na rushwa, ufisadi na ubinafsi, kuna kila sababu ya kuwa na hofu ya kushindwa katika uchaguzi wa mwaka 2015.

Alisema hali hiyo inatokana na viongozi wengi kutokuwa na ujasiri wa kukemea ufisadi na rushwa.

Aliongeza kuwa chama hicho kitashindwa kutokana na viongozi wengi kuhusishwa na tuhuma za ufisadi.

MHADHIRI UDOM

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Paul Loisulie, alisema: “Kauli aliyoitoa Rais Kikwete ni sahihi kabisa na wana-CCM wanatakiwa kutoipuuza ila waitafakari kwa undani zaidi.”

Alisema vitendo vya  rushwa, ubabe na kutowajibika, ndivyo vinavyowaondolea imani wananchi kwa chama hicho.

“Binafsi nakubaliana nayo kauli hiyo kwa asilimia 100…mfano mzuri ni ubabe na vitisho vya wana-CCM juu ya mchakato wa Katiba na matokeo yake watu wengi wanaungana na wapinzani.

“Mimi nashangaa alikuwa wapi, nani hajui kwamba asilimia 80 kama siyo 90 ndani ya CCM waliingia kwa rushwa?. Anakumbuka shuka kumekucha,” alisema Jonathan Bahweje, mkazi wa jijini Tanga.

Bahweje alidai kuwa kauli hiyo si ya msingi ndani ya CCM  kwani haiwezi kutekelezeka kwa kuwa wenye mamlaka ya kufanya hivyo ni miongoni mwa viongozi walioingia kwa njia za mizengwe na kwamba wengi wao hawakubaliki kwa kuwa siyo changuo la wanachama.

Alisema kauli hiyo inatia shaka na kwamba inalenga kukisafisha chama hicho na kuwataka wana-CCM  kuchukua tahadhari kwa  kuwataka viongozi wala rushwa kujivua gamba kwa kuwa wanafahamika.

Mkazi mwingine wa jijini Tanga, Sabitina Mbwana, alisema CCM kitavuna kilichopanda kutokana na ukweli kwamba kauli ya Rai Kikwete ndiyo kilio cha wanachama wa chama hicho nchi nzima na kuongeza kuwa kilikosa msimamiazi na wa kuchukua hatua badala yake wanachama walipuuzwa na yakajengeka matabaka ya kulindana.

Nuru Rajab, alibainisha kuwa kauli hiyo ni ishara kwamba CCM imepoteza mwelekeo na kwamba haiaminiki tena katika kusimamia na kutenda haki kama inavyotarajiwa na wengi.

“Kimekiuka misingi ya upatikanaji wa viongozi na hivyo kupata viongozi wabovu, wala rushwa …jambo hili limeendana na kauli ya Baba wa Taifa kuwa chama kikiwa legelege kitaunda serikali legelege,” alisema Rajab, mkazi wa jijini Tanga.

Moses Kyemberei, muasisi wa CCM kutoka Arumeru, alisema ameshangazwa na kauli ya Mwenyekiti wa CCM hadharani kuwa Chama kipo katika hali mbaya.
“Huyu ndiye kiongozi mkuu wa Chama kama anaweza kutamka mambo haya tena hadharani, ninapata shaka. Nchi imekuwa ni ya watu kulalamika tu, yeye kama kiongozi anachukua hatua gani?” Alihoji.

Christina Soud, wa Chuo Kikuu cha Mount Meru, jijini Arusha, alisema Mwenyekiti huyo amefanya vyema kueleza hadharani kuhusu hali ilivyo ndani ya CCM, lakini alipaswa kuchukua hatua ili kuonyesha kuwa yeye ni kiongozi na siyo mtu wa kulalamika.

Imeandikwa na Raphael Kibiriti, Thobias Mwanakatwe, Dar;  Jacqueline Massano na Peter Mkwavila, Dodoma; Dege Masoli, Tanga na Charles Ole Ngereza, Arusha.
CHANZO: NIPASHE