Na Aidan Mhando, Mwananchi
Posted Alhamisi,Oktoba31 2013 saa 24:0 AM
Posted Alhamisi,Oktoba31 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Ni kauli ya aliyekuwa mchumba wa marehemu Luteni Rajabu, aliyeuawa nchini DRC .
Dar es Salaam. Mchumba wa
askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), aliyeuawa kwa
kupigwa risasi akiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Luteni Asia
Hussein aliyekuwa naye kabla ya kuuawa mchumba wake amesema, marehemu
alimwomba amwombee arudi salama kutoka kwenye mapigano.
Pia, alisema kauli hiyo ndiyo ya mwisho kuisikia
kutoka kinywani mwa mchumba wake huyo aliitoa baada ya kutolewa amri ya
kijeshi kwamba anatakiwa kwenda kuwasaidia wenzake waliokuwa kwenye
mapigano na askari wa waasi wa M23.
Askari huyo wa(JWTZ), Luteni Rajab Ahmed Mlima,
aliuawa akiwa kwenye uwanja wa mapambano na vikosi vya askari wa waasi
wa M23 katika milima ya Gavana, karibu na Goma, DRC wakati akitekeleza
jukumu la ulinzi wa amani.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti
hili jana nyumbani kwake, Luteni Asia alisema, “Ninachokumbuka
walitakiwa kwenda kuwasaidia wenzao waliokuwa kwenye mapigano kwa muda
mrefu, tayari walikuwa wamezidiwa nguvu na askari wa waasi wa M23,
ukweli hali ilikuwa mbaya na mimi nilimkataza asiende kwa kuhofia
usalama wake,” alisema Luteni Asia huku akibubujikwa machozi.
Alisema wakati akimsihi asiende alimjibu kwamba ni
lazima aende kuwasaidia wenzao, kwani kazi waliyotumwa kuifanya ni
pamoja na hiyo hivyo asingeweza kuacha kwenda.
Aidha, Luteni Hussein alibainisha kuwa baada ya
kwenda kutoa msaada na kufanikiwa kuwadhibiti waasi, muda mfupi baadaye
alipata taarifa kuwa Luteni Mlima amefariki kwa kupigwa risasi jambo
lililomshtua kiasi cha kuishiwa nguvu kabisa.
Alisema kwa kuwa kazi ya Mungu haina makosa, yeye
anamwombea huko aliko apumzike kwa amani kwani amefariki akiwa
anawatetea wananchi wa DRC na kuiwakilisha nchi yake.
Mipango ya harusi
Akielezea mipango yao ya harusi, Luteni Asia
alisema Desemba 28, mwaka huu walipanga kufunga ndoa na kwamba taratibu
zote zilikuwa zimekamilika ikiwa pamoja kutolewa mahari.
“Kwa kweli jambo linalo niuma sana na siwezi
kusahau ni kwamba, tulikuwa tumebakiza muda mfupi tufunge ndoa na kila
kitu kilikuwa kimeshakamilika hadi ukumbi wa kufanyia sherehe ya harusi
yetu tulishaulipia,” alisema Luteni Hussein huku akibubujikwa na
machozi.
Kaka wa marehemu
Akizungumza na gazeti hili, kaka wa marehemu Dk
Aziz Mlima alisema ndugu yao atazikwa leo Alhamisi saa 10 kwenye
makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.
JWTZ yatoa tamko
Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ), Meja Erick Komba alisema mwili wa Luteni Rajab Ahmed Mlima
ulitarajiwa kuingia jana saa moja jioni na kuhifadhiwa kwenye kambi ya
Jeshi Lugalo. Alisema taratibu za kuuaga mwili huo zitafanyika kijeshi
kwenye kambi hiyo kuanzia leo saa tatu asubuhi na mazishi yatafanyika
kwenye makaburi ya Kisutu Dar es Salaam.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI