Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Posted Jumatatu,Oktoba14 2013 saa 9:10 AM
Posted Jumatatu,Oktoba14 2013 saa 9:10 AM
Kwa ufupi
Katika tukio hilo linalodaiwa kufanywa na mzazi
mwenzake, Anthery Mushi ambaye alijiua baadaye, pia anadaiwa kumuua mama
yake Ufoo, Anastazia Saro.
Kibaha/Dar es Salaam. Mwandishi wa Kituo cha
Televisheni cha ITV, Ufoo Saro amejeruhiwa vibaya baada ya kupigwa
risasi mbili jana alfajiri huko Kibamba, Dar es Salaam.
Katika tukio hilo linalodaiwa kufanywa na mzazi
mwenzake, Anthery Mushi ambaye alijiua baadaye, pia anadaiwa kumuua mama
yake Ufoo, Anastazia Saro.
Ufoo alipigwa risasi moja tumboni na kutokea
kwenye mbavu na nyingine ilipita kifuani hadi kwenye ziwa lake la kulia
na kutokea kwenye mkono wa kulia.
Baada ya tukio hilo, Ufoo alipelekwa katika
Hospitali ya Tumbi, Kibaha kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili ambako alifanyiwa upasuaji.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Kamishna Suleiman Kova alithibitisha kutokea kwa tukio hilo
lililosababisha vifo hivyo na kumjeruhi mwandishi huyo.
Kova alimtaja Mushi, ambaye alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Saro akidai kuhusika na tukio hilo.
“Mushi alimpiga risasi za kifuani mama yake Ufoo,
ambaye alifariki palepale. Pia alimpiga risasi mwandishi huyo na baadaye
alijiua kwa kujipiga risasi chini ya kidevu, risasi ambayo ilifumua kwa
kiasi kikubwa eneo la juu la kichwa chake.”
Kova aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa katika Hospitali ya Muhimbili kuwa, vifo hivyo vimetokana na wivu wa mapenzi.
Mashuhuda wa tukio
Akizungumzia tukio hilo, mdogo wa mwandishi huyo,
Goodluck Saro alisema dada yake Ufoo na shemeji yake Mushi walikwenda
nyumbani kwa mama yao huko Kibamba saa 12.00 asubuhi na kwamba baada ya
kufika huko walikuwa na mazungumzo na mama yao ambayo hata hivyo,
hakuyafuatilia kwa kuwa alikuwa amelala.
Goodluck alisema, muda mfupi baadaye alisikia sauti ya mama yake, ikimwita; “Goodluck nakufa... Goodluck nakufa.”
Alisema alitoka chumbani na kwenda sebuleni ambako alimkuta Ufoo akiwa ameanguka chini huku akichuruzika damu.
“Ufoo aliponiona aliniagiza nirudi chumbani mara moja. Niliporudi chumbani, Mushi akaanza kupiga risasi ovyo,” alidai Goodluck.
Goodluck alisema alikuwa chumbani na ndugu zake
Jonas Saro na Abel Innocent, ambao walilazimika kupanda darini ili
kuokoa maisha yao.
Alidai kuwa baada ya Mushi kuona amewakosa ndugu
zake Ufoo alikusanya nguo zote na kuziweka karibu na mtungi wa gesi,
ambao aliupiga risasi na kusababisha kuwaka moto.
“Tukiwa darini tulizidiwa na moshi tukalazimika kupasua paa na kuruka nje ya nyumba,” alisema Goodluck.
Baada ya kutoka nje alisema walipiga simu polisi
na ilipotimu takriban saa tatu asubuhi polisi mmoja alifika lakini
baadaye waliongezeka na hivyo kupata ujasiri wa kuingia ndani ya nyumba.
Mtuhumiwa akutwa na tindikali, kamba na shoka
Goodluck alidai kwamba walimkuta shemeji yao akiwa
amejiua huku akiwa ameketi kwenye kiti na kichwa chake kikiwa
kimefumuka jambo ambalo alisema wanaamini kuwa alijipiga risasi.
Goodluck alisema baada ya ukaguzi, askari
walimkuta akiwa na kitu kinachoaminika kuwa ni tindikali, shoka, mifuko
ya plastiki, kompyuta ndogo, kamba, pingu na risasi nane.
“Tunahisi alikuwa na risasi kama 17 hivi kwani alitumia tisa hivi wakati wa tukio hilo na zikabaki nane,” alisema Goodluck.
Baadhi ya majirani walisema walisikia milio ya
risasi na wakati wakiulizana kulikoni, alitokea mtoto anayeishi kwenye
nyumba ya marehemu na kuwaomba msaada akisema kulikuwa na ugomvi.
“Tulipokwenda tulichungulia na kuona damu
zimetapakaa chumba kizima, pembeni tuliuona mwili wa mama yake Ufoo Saro
ukiwa umelala chini. Nyumba ilikuwa imejaa moshi mzito, tulipiga simu
polisi kutoa taarifa,” alisema mmoja wa majirani, Bobroy Ngowi.
Licha ya kuwa katika maumivu makali, hadi polisi wanafika, Ufoo alikuwa ameshatoka katika eneo la tukio mwenyewe.
Ufoo aelezea mkasa mzima
Akizungumza kwa taabu wakati akiwa kwenye gari la
wagonjwa kutoka Tumbi kuelekea Muhimbili, Ufoo alisema alijivuta kutoka
nje na kutembea mwenyewe hadi barabarani.
Alisema baada ya madereva wa Boda Boda kumwona anavuja damu nyingi, walimpakia na kumpeleka Tumbi.
Hata hivyo, alipofika Tumbi, anasema hakuchukuliwa
vipimo kutokana na kutokuwepo kwa mtaalamu wa x-ray ndipo ilipoamuliwa
kuwa apelekwe Muhimbili.
Akiwa amefuatana na Mwandishi Wetu, Julieth Ngarabali Ufoo licha ya kuwa na maumivu makali, alisimulia kilichomsibu.
Ilikuwa baada ya kufika Kibaha mizani Ufoo
alipomwita mwandishi wetu: “Julieth naomba uiname nikusimulie kitu...
Unajua aliyefanya haya ni Baba Alvin (Mushi). Amempiga risasi mama na
mimi mwenyewe.”
Baada ya kusema hivyo, alinyamaza na kuanza kububujikwa na machozi.
Baada ya kufika Kibamba alipata nguvu na kusimulia
kuwa mama yake alikuwa amefariki katika tukio hilo... Huku akilia,
alisema kuwa alipewa taarifa hizo na polisi.
“Masikini mtoto wangu Alvin sijui itakuwaje, baba
yake amejiua, amemuua mama yangu na babu yake alishafariki... sijui
atabakia na nani, maana sijui kama nitapona,” alisema huku akilia.
Ufoo ambaye alitoka katika chumba cha upasuaji saa
12 jioni, alisema atakapopata nafuu ataweka hadharani mkasa mzima
uliosababisha mauti na majeraha hayo.
Mushi ni nani?
Mushi alikuwa mfanyakazi kitengo cha mawasiliano
cha Umoja wa Mataifa huko Darfur, Sudan na alikuwa na uhusiano wa
kimapenzi na Ufoo kwa zaidi ya miaka 10.
Pia aliwahi kufanya kazi ITV na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), akiwa mpigapicha wa televisheni.
Baada ya kuondoka kwenye fani ya habari alijiunga
na Mahakama ya Kimataifa inayoshughulikia kesi za Rwanda (ICTR), kabla
ya kwenda Sudan.
Ofisa wa Kitengo cha Habari cha Umoja wa Mataifa
huko Darfur, Said Msonda alisema kuwa Mushi alikuwa amehamishwa kutoka
kituo cha El-Jenina na kupelekwa kile cha Al-Fasha.
“Tulikuwa tumepanga kumwandalia tafrija ya kumuaga baada ya kurudi kutoka Tanzania na haya ndiyo yametokea,” alisema.
Kaka mkubwa wa marehemu, Silva Mushi alisema mdogo wake alikuwa Moshi kabla ya kuja Dar es Salaam.
“Nilikuwa sijawasiliana naye siku nyingi na nilikuwa sijawahi kusikia kama alikuwa na matatizo yoyote na Ufoo,” alisema.
Mazishi ya mama wa Ufoo
Msemaji wa familia ya kina Saro, Iddi Lema alisema
kuwa mazishi ya mama yake Ufoo yamepangwa kufanyika Ijumaa katika
Kijiji cha Mashari, Machame mkoani Kilimanjaro.
Lema alisema msafara wa kuelekea huko utaondoka
Dar es Salaam Alhamisi na kwamba ndugu, jamaa na marafiki watakutana
kesho saa 10.00 kwenye Ukumbi wa Urafiki kwa ajili ya kufanikisha
taratibu hizo.
Imeandikwa na Julieth Ngarabali, Aidan Mhando, Fidelis Butahe, Pamela Chilongola na Sanjito Msafiri.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI