Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Posted Jumatatu,Oktoba14 2013 saa 8:50 AM
Posted Jumatatu,Oktoba14 2013 saa 8:50 AM
Kwa ufupi
Mzee Kisumo alitoa onyo hilo wiki iliyopita katika
mazungumzo maalumu aliyofanya na Mwananchi nyumbani kwake Dar es Salaam
kuhusu kumbukumbu ya miaka 14 ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere
inayoadhimishwa leo.
Dar es Salaam. Mwanasiasa na kada mkongwe wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Peter Kisumo ameonya kuwa chama hicho
kinaweza kuondolewa madarakani kutokana na kunyamazia vitendo vya
ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za umma vinavyotokea nchini.
Mzee Kisumo alitoa onyo hilo wiki iliyopita katika
mazungumzo maalumu aliyofanya na Mwananchi nyumbani kwake Dar es Salaam
kuhusu kumbukumbu ya miaka 14 ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere
inayoadhimishwa leo.
Alisema tatizo kubwa la chama hicho ni kwamba
kimemeendelea kuwa chama dola kikikaa mbali na wananchi, huku
kikishindwa kuidhibiti rushwa na kuwajibisha wahusika wa vitendo hivyo.
“Chama kimebaki kuwa cha walalamikaji, kila mtu
amekuwa mlalamikaji. Hata Waziri Mkuu amegeuka mlalamikaji. Sijaona watu
wanaowajibishwa kwa ufisadi,” alisema Kisumo na kuongeza:
“CCM haiwezi kujivunia ufisadi unaoonekana nchini.
Siwezi kusema imeukumbatia, lakini nasema imekuwa CCM bubu, hata
kuukemea ufisadi haiwezi. Utamaduni huu enzi za Mwalimu Nyerere
haukuwapo.”
Alisema kutokana na udhaifu huo wa CCM, kuna
uwezekano mkubwa wa chama cha upinzani, na hasa Chadema kutumia mwanya
huo kuwashawishi wananchi na kushinda uchaguzi.
Kisumo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini wa CCM, alisema ingawa Chadema haijaonyesha wazi mambo
kinayoyapigania, kinaweza kutumia agenda ya ufisadi na matumizi mabaya
ya rasilimali za umma kuwavutia wananchi na kuchaguliwa.
Alitoa mfano wa tuhuma za baadhi ya viongozi wa
Serikali kuficha mabilioni ya shilingi kwenye benki za Uswisi, kuwa
zinaweza kuwa kete muhimu ya kuwaingiza Chadema madarakani, iwapo
Serikali ya sasa haitawashughulikia wahusika.
“Wakijitokeza na kuwataja majina wahusika,
wakasema fulani na fulani ndiyo wenye mabilioni haya Uswisi, na Serikali
ikasita kuwachukilia hatua, wakasema tukiingia madarakani tutawakamata,
wananchi wanaweza kuwaamini na kuwachagua,” alisema na kuongeza:
“Wakishinda uchaguzi hata kwa viti vichache tu, watakosa nguvu bungeni,
lakini kwa wananchi watakuwa na nguvu sana.
Hii inaweza kuwasaidia kwa miaka mitano ya kwanza.
Wanaweza kupata ushindi mkubwa zaidi kwa mara ya pili na wakiingia
madarakani watawafunga viongozi wa zamani kweli.”
Mzee Kisumo anasistiza, “Hili linawezekana.
Anayesema uwezekano wa CCM kushindwa haupo, anajikana mwenyewe. CCM
inabidi ijihami na majibu ya jinsi inavyotumia rasilimali za nchi.”
Alionya kuwa si vizuri kuishia kujinadi kwa mambo
mengi mazuri iliyofanya huko nyuma, akitolea mfano kuwa hiyo ni sawa na
nguo nyeupe ambao ikiingia doa moja tu inakuwa haitamaniki tena.
“Sisemi kwamba hawajafanya kitu, yapo mengi mazuri
waliyoyafanya, lakini ufisadi ni sawa na doa kwenye shati jeupe ambalo
huwa linaonekana kuliko weupe na ung’avu wa shati hilo,”alisema Kisumo.
Alisema katika siku za karibuni ufisadi umekuwa
jambo la kawaida, hadi umegeuzwa kuwa wa kitaasisi, ambapo aligusia hata
Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ulioanzishwa na Bunge kuwa ni sehemu ya
ufisadi.
Alihoji iweje fedha za umma zitumike kumsadia mtu mmoja kujiimarisha kisiasa, akisema hiyo ni ‘Built in Corruption’.
Mzee Kisumo pia alizungumzia mvutano ambao umekuwa
ukijitokeza kati ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) na Mkurugenzi
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwamba
msingi wa mvutano huo ni kuwapo tabaka la wahalifu wasioweza kuguswa na
sheria.
“Unapokuwa na mvutano huo una maana mbili, kwanza
ni hali kwamba huyo mmoja anajua sabababu za watuhumiwa kutochukuliwa
hatua, lakini pili ni kwamba huenda tuna watu wawili katika nafasi hizi,
lakini wana nia mbili tofauti,”alisema Kisumo na kuongeza:
“Ni hatari sana unapokuwa na mfumo kwenye nchi
ambao unawalinda baadhi ya wahalifu, unakuwa na wahalifu wanaoguswa na
wengine hawaguswi, watu wanasubiri pengine itokee siku waone mtu
wasiyemtarajia anafikishwa mahakamani na hapo watajua kwamba kweli nchi
imeamua kupambana na rushwa na ufisadi.”
…Aonya Zanzibar
Mzee Kisumo pia alizungumzia mchakato wa
mabadiliko ya Katiba Mpya na kwamba mvutano kuhusu muundo wa Muungano ni
matokeo ya upande wa Zanzibar kuachiwa kufanya vitendo vingi
vinavyoashiria kutafuta uhuru kamili kama nchi nje ya Muungano huo.
Vitendo hivyo kwa mujibu wa kada huyo ni
mabadiliko ya kumi ya Katiba ya Zanzibar ambayo yalitamka kuwa Zanzibar
ni nchi, kurejesha bendera yake, wimbo wake wa taifa na mambo mengine.
“Katika hatua sasa Zanzibar wanajiona kwamba
wamekaribia kutimiza azma yao, kuelekea katika ‘uhuru’ kamili, nasema
whoever (yeyote) aliyefumbia macho vitendo hivi akiwa Rais, alifanya
makosa makubwa,”alisema Mzee Kisumo na kuongeza:
“Ukitafakari hali hiyo, kama tukiwa na mfumo wa
Serikali Tatu, ni kitu gani kitawazuia Tanganyika nao wasidai kuwa na
Katiba sawa na ile ya upande wa pili? Ikifika hapo mimi sioni Muungano
kuwapo.”
Hata hivyo, alionya kuwa masuala yote yanayohusu
Muungano ikiwa ni pamoja na lile la mabadiliko ya kumi ya Katiba ya
Zanzibar, yanapaswa kufanyiwa uamuzi wa busara kwani historia inaonyesha
kuwa kuvunja Muungano wowote ule lazima damu imwagike.
“Muungano wa States (nchi) za Marekani uligharimu umwagaji damu,
United Kingdom (Uingereza) pia damu ilimwagika, kwa hiyo lazima
tujifunze kwamba ikiwa tutafikia hatua ya kuvunja Muungano wetu,
hatuwezi kupita salama katika hili,” alisema.
Alisema kinachotokea sasa kuhusu Zanzibar kuwa na
mwelekeo wa kujitenga, ilianza katika chaguzi zilizopita, pale ambapo
Mzanzibari aliyekaa nje ya visiwa hivyo kwa zaidi ya miaka mitano
anakosa haki ya kupiga kura kwa kukosa sifa ya ukaazi.
“Hili nalo ni tatizo kubwa, Mzanzibari ambaye
ameamua kuishi Moshi, Morogoro au kwingineko nchini uhalali wake wa kuwa
Mzanzibari unawekwa shakani, kwani hawezi kupiga kura kama hajaishi
Zanzibar mfululizo kwa kipindi hicho,” alisema Mzee Kisumo na kuongeza:
“Ukiangalia kwa Mtanzania wa Bara, hakutani na
kadhia hii, yeye ataishi popote hata kama nje ya nchi kwa muda wowote,
lakini akirudi nyumbani haambiwi eti si mkaazi, kama ni Tabora atakwenda
kwao au Mbeya”.
Mzee Kisumo alisema kutokana na hali hiyo kuna
kundi kubwa la Wazanzibari ambalo linajikuta katika hatari ya kukosa
haki zao na kwamba ikiwa kutakuwa na mfumo wa Serikali Tatu na upande wa
Tanzania Bara kuanzisha utaratibu kama wa Zanzibar, watajikuta kwenye
utata wa uraia wao.
“Tukiwa na Tanzania moja iliyoungana, ambayo watu
wake hawana mwelekeo wa kuangalia masilahi yao zaidi, haya mambo
hayawezi kutokea. Kimsingi mtu yeyote ambaye ni raia wa Tanzania
anapaswa kujivunia uraia wake kama Mtanzania na hapaswi kuishi kwa
vikwazo vya aina hii,”alisema Kisumo na kuongeza:
“Kwa hiyo mimi nasema haya mambo lazima… Lazima
tuyatizame kwa upana wake….Maana hawa watu wapo wanaathirika, sihitaji
kutaja majina ya watu hapa, lakini wapo, wanafahamika na wengine ni
wafanyabiashara wakubwa sana nchini, wametoka Zanzibar na wameishi
Tanzania Bara kwa miaka mingi.”
Kisumo alionekana kukerwa zaidi na pendekezo la
kuwapo kwa Serikali ya mkataba na kusisitiza kuwa wanaotoa mawazo ya
aina hiyo wanakusudia kuvunja Muungano kwa masilahi yao binafsi.
... Asema Nyerere alijaa katika mioyo ya Watanzania
Wakati taifa leo linatimiza miaka 14 tangu
kufariki kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Kisumo anasema kuwa
kiongozi hiyo alikuwa na sifa nyingi ambazo zilimfanya kujaa mioyoni mwa
wa Watanzania.
Akizungumzia sifa za Nyerere kabla na baada ya
uhuru wa Tanganyika iliyokuja kuwa Tanzania baadaye , Kisumo anaeleza
kiongozi huyo alikuwa na uzalendo wa hali ya juu kwa nchi yake na Bara
la Afrika kwa jumla.
Kisumo, ambaye alifanya kazi na kiongozi huyo
kabla na baada ya uhuru, alisema sifa nyingine ya Mwalimu Nyerere
ilikuwa uwezo wake wa kushawishi na kuongoza.
“Nyerere pia aliamini katika umoja wa taifa na uongozi wa pamoja
na ndio maana alifanikiwa katika nyanja nyingi,” anasimulia Kisumo,
ambaye alianza siasa kupitia kwenye vyama vya wafanyakazi akiwa na
Waziri Mkuu wa zamani, Rashid Kawawa na Marehemu Michael Kamaliza katika
miaka ya 1950.
Kisumo anasema bila ya kificho kuwa marais
waliomfuatia Nyerere wameshindwa kufikia sifa ya Mwalimu hasa linapokuja
suala zima la sifa za uongozi.
Alitoa mfano kitendo cha Nyerere kwa kutumia lugha
ya Kiswahili na kuunganisha watu wa Tanganyika kupigania uhuru bila ya
kumwaga damu kutoka kwa Waingereza.
“Alipigania uhuru bila ya kuwa na jeshi au silaha
unaweza mwenyewe ukamfikiria mwenyewe Mwalimu alikuwa ni kiongozi wa
aina gani?
“Nyerere aliunganisha machifu waliokuwa na nguvu
sana katika kipindi kile ingawa alipingwa na baadhi yao kama Chifu
Thomas Marealle wa Moshi.
“Huyu Chifu Marealle alikwenda mbali zaidi na hata
kwenda kwenye Umoja wa Mataifa nchini Marekani na kueleza kuwa
Tanganyika haikuwa tayari kujitawala, lakini alishindwa kwa hoja za
Mwalimu,” aliongeza Kisumo, ambaye alishika nyadhifa mbalimbali wakati
wa uongozi wa Nyerere zikiwamo za Uwaziri na Ukuu wa Mkoa.
Kisumo anaeleza kuwa Mwalimu aliwazidi kete Waingereza kwani alipenya katika asasi mbalimbali za Watanganyika.
“Mwalimu alitumia michezo kudai uhuru, alikuwa
karibu sana na klabu ya Yanga pia hata vikundi vya muziki wa dansi na
taarabu,” aliongeza Kisumo.
Kisumo anasimulia kuwa baada ya Tanganyika kupata
uhuru bado Nyerere alisaidia mataifa mengine katika harakati zao za
kupigania uhuru wao na alitaka Umoja wa Afrika na ndio maana akaasisi
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.
Ukombozi wa Afrika
Alisema Nyerere alikubali Kamati ya Ukombozi ya
iliyokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) iweke makao makuu yake
jijini Dar es Salaam.
“Kilikuwa kitendo cha hatari kwani mataifa mengi
wakati ule hayakukubali kupokea wapigania uhuru kwa kuhofia usalama wa
nchi zao.
SOURCE: MWANANCHI
“Vyama mbalimbali kutoka nchi za Afrika Kusini, Angola, Msumbiji
na Namibia vilileta watu wao kwa mafunzo ya kijeshi, jambo ambalo
lilitutisha wakati ule,” anaongeza Kisumo.
Kisumo alisimulia kuwa Nyerere alisimamia umoja na
ukombozi wa Bara la Afrika na kumfanya ajizolee sifa sawa na marais
wengine kama Gamal Abdel Nasser wa Misri, Ben Bella wa Algeria na Kwame
Nkrumah wa Ghana.
Kisumo alisema kuwa Mwalimu hakuishia kuunga mkono
wapigania uhuru wa Afrika pia aliunga mkono harakati za Wapalestina
kujikomboa kutoka kwa Israel, ambayo katika miaka ya mwanzo wa Uhuru
ilikuwa kati ya wafadhili wakubwa wa Tanzania.
“Nakumbuka Kiongozi wa Chama cha Ukombozi cha
Palestina (PLO), Yasser Arafat alialikwa katika moja ya mikutano ya
chama cha TANU iliyofanyika jijini Dar es Salaam,” anaongeza Kisumo.
Sera za uchumi
Kisumo anasema kuwa Nyerere alikuwa anaamini kuwa Tanzania itaendelea kiuchumi kama itawekeza vya kutosha katika kilimo.
“Ndio maana katika miaka ya mwanzo baada ya uhuru
tulikuwa na sera ya `Siasa ni Kilimo’ na baadaye `Kilimo cha Kufa na
Kupona’,” alisema Kisumo.
Kisumo alisema kuwa baada ya kampeni ya kilimo,
Nyerere aliona umuhimu wa kujenga viwanda ili kutumia malighafi
iliyotoka katika kilimo.
“Ndio maana ukaona tukajenga viwanda vya nguo
katika Miji ya Dar es Salaam, Arusha, Musoma na Mwanza pia kiwanda cha
nyuzi pale Tabora,” alisema.
Pia Kisumo alisema kuwa Mwalimu aliweka mkazo katika elimu ya kujitegemea ili kumwandaa kijana wa Kitanzania.
“Hivi majuzi nilisikitika sana baada ya kusikia
ikiwa shule moja huko Kigoma imepokea msaada wa vyoo vya shimo kutoka
kwa Wachina! Hivi kweli imefika mahali wanafunzi wetu wanashindwa
kuchimba vyoo?” alihoji Kisumo kwa masikitiko.
Kisumo alisema kuwa mambo yalibadilika katika
miaka ya 1990 wakati Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Margareth
Thatcher alipoanzisha sera za ubinafsishaji na utandawazi.
“Hapo ndio yakabadilika ambapo mataifa makubwa yakazidi
kuzikandamizia nchi changa kupitia misaada ya Benki ya Dunia na Shirika
la Fedha la Kimataifa (IMF),” alisema Kisumo.
Kisumo alisema Mwalimu alipambana na mataifa hayo
makubwa na kutaka kuacha kukandamiza nchi changa. Alipambana na mataifa
kupitia Tume ya Kusini 1986, taasisi ambayo ilitokana na uliokuwa Umoja
wa Nchi zisizofungamana na upande wowote (NAM).
Imeandikwa na Neville Meena, Samson Mfalila na Regnald Miruko
SOURCE: MWANANCHI