* Asema yeye kuwa Waziri wa Katiba na Sheria anajiona kama samaki aliyetumbukizwa majini
Wakazi
wa Jimbo la Nachingwea mkoani Lindi, wana kila sababu ya kujivunia
bahati ya wabunge wao kuteuliwa na Rais kuongoza wizara mbalimbali hapa
Tanzania. Edgar Maokola-Majogo, aliyeliongoza jimbo hilo kwa kipindi cha
miaka 30, pamoja na wizara nyingine, alipata kuwa Waziri wa Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, kitengo
cha Kupunguza Umaskini na Kuratibu Mashirika yasiyo ya Kiserikali na
Waziri wa Nishati na Madini.
Baada ya Maokola-Majogo kustaafu siasa mwaka 2005, Mathias Meinrad
Chikawe, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Katiba na Sheria, alishika hatamu
ya kuliongoza jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kilichomshawishi Chikawe
Katika mahojiano maalum na JAMHURI
Dar es Salaam wiki iliyopita, Waziri Chikawe ambaye kitaaluma ni
mwanasheria, anasema alianza kunusa siasa mwaka 1999 wakati akifanya
kazi katika Tume ya Marekebisho ya Sheria Tanzania (TLRC).
“Nikiwa
pale kwenye tume [TLRC] ndiyo nikashawishika kujihusisha na siasa kwa
vitendo, na Kikwete [Jakaya Mrisho Kikwete] alipoanza kusikika ndipo
nami nikashawishika. Nilikutana naye akanitia moyo,” anasema Chikawe na
kuendelea:
“Mwaka
2000 nilikwenda kuwania ubunge wa Nachingwea, lakini nikashindwa katika
kura za maoni [ndani ya CCM], ila kura nyingi nilizopata zilinitia
moyo. Hata Maokola-Majogo aliyenishinda alitikisika.
“Baada
ya hapo ndiyo nikasema kumbe hili jambo linawezekana, na wananchi
wakawa wananitia moyo, si kwamba Maokola-Majogo ni mbaya, lakini kwa
sababu walikuwa wamemchoka.”
Kitendo
cha kuungwa mkono na wananchi wengi kilimwongezea Chikawe ujasiri kiasi
cha kujitosa tena kwenye kinyang’anyiro cha ubunge wa Nachingwea katika
Uchaguzi Mkuu mwaka 2005.
Mwaka
huo, pengine baada ya kusoma alama za nyakati, Maokola-Majogo
alitangaza kung’atuka siasa, hivyo hakujitokeza kuomba kuteuliwa na CCM
kugombea ubunge katika jimbo hilo. Hatua hiyo ilimpatia Chikawe nafasi
nzuri zaidi ya kutwaa ushindi.
“Katika
uchaguzi ule [wa 2005] nilishinda kwa kupata asilimia 85 za kura za
jumla, nikaingia [bungeni] nikiwa na nguvu,” anasema Chikawe na
kuongeza:
“Kuanza
tu [ubunge] Rais [Rais Kikwete] akaniteua kuwa Naibu Waziri wa Katiba
na Sheria chini ya Waziri kamili, Dk. Mary Nagu. Baadaye Rais akafanya
mabadiliko na kuniteua kuwa waziri kamili wa wizara hii.
“Mwaka 2010 nikarudi kugombea [ubunge], wananchi wakasema bado wana imani na mimi, wakanichagua kwa kura nyingi.
“Niliporudi
bungeni Rais akaniteua kuwa Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, (Utawala
Bora), nikawa pale Ikulu na yeye, tukaendelea vizuri hadi mwaka 2012
aliponitoa pale akanirudisha tena Wizara ya Katiba na Sheria wakati
vuguvugu la mabadiliko ya Katiba limeshaanza.”
Lengo lake kisiasa
Waziri
Chikawe anasema lengo kuu la yeye kujiingiza katika siasa ni kutafuta
ufumbuzi wa matatizo ya huduma duni za umeme, maji, barabara na umaskini
yaliyokuwa yanawakabili wakazi wa Jimbo la Nachingwea.
“Kabla
sijaenda kugombea ubunge, kila nilipopata nafasi ilikuwa lazima
niondoke Dar es Salaam kwenda Nachingwea kusalimia wazazi wangu, ndipo
nikawa ninashuhudia kero zinazowakabili wananchi kule.
“Umeme
ulikuwa kero, unakatika ovyo, maji ni shida, watu walikuwa wanachota
maji machafu kwenye visima, nilikerwa pia na hali ya umaskini wa
wananchi. Nikasema labda ninaweza kufanya kitu kikaleta mabadiliko
kule,” anaeleza.
Mafanikio anayojivunia jimboni
“Mafanikio
ni makubwa. Mwaka 2005 nilipochaguliwa kuwa mbunge, Nachingwea yenye
wakazi 187,000 ilikuwa na shule za sekondari tatu, hospitali mbili,
vituo vya afya viwili, umeme ulikuwa ni mjini tu na barabara zote
zilikuwa za vumbi,” anasema Chikawe na kuendelea:
“Lakini
mpaka sasa mradi wa maji uliogharimu Sh bilioni 31 umekamilika, watu
wanatumia hayo maji, tatizo la uhaba wa maji limepungua Nachingwea.”
Anafafanua
kuwa mradi huo umewezesha mji wa Nachingwea na vijiji tisa kuwa na
uhakika wa huduma ya maji safi ya bomba na kwamba Rais Kikwete ameahidi
kwenda kuuzindua wakati wowote akipata nafasi.
“Ninajivunia
juhudi zangu hizo na ninamshukuru Rais kwa kunisaidia kutafuta ufumbuzi
wa tatizo la uhaba wa maji Nachingwea. Pia ninamshukuru Mwandosya
[Profesa Mark James Mwandosya] naye alinisaidia sana kufanikisha mradi
huo,” anasema Waziri Chikawe.
Kikwete
alipata kuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Nachingwea. Profesa Mwandosya
ambaye kwa sasa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Asiye na Wizara
Maalum, alipata kuwa Waziri wa Maji.
Pia
tumefanikiwa kuchimba mabwawa matano ya maji, kila moja linahudumia
vijiji vinne na tumechimba visima virefu saba vya maji,” anaongeza
Chikawe.
Kuhusu umeme, Waziri Chikawe anasema amejitahidi kupunguza kwa kiwango kikubwa tatizo lililokuwapo.
“Siku
hizi kule Nachingwea unaweza kukaa wiki nzima bila kuona umeme
umekatika na wananchi wengi, hasa vijana wanatumia fursa hiyo kuanzisha
na kuendesha miradi mbalimbali ya uzalishaji mali,” anasema.
Kwa
mujibu wa waziri huyu, chanzo cha umeme huo ni gesi inayovunwa katika
Mkoa jirani wa Mtwara. Akizungumzia barabara, Chikawe anasema, “Sasa kwa
mara ya kwanza, wananchi wa Nachingwea wanaona lami, tumejenga barabara
ya lami yenye urefu wa kilomita tano.”
Kwa
upande wa sekta ya afya, mbunge huyu wa Nachingwea anasema ameweza
kuishawishi Serikali kwa kushirikiana na wananchi hadi kufanikisha
ujenzi wa zahanati 28 katika kata 28, na kwamba juhudi zinafanyika
kuwezesha ujenzi wa zahanati nyingine nne katika kata nne zilizosalia.
Sekta
ya elimu, kwa mujibu wa Chikawe, nayo haijaachwa nyuma katika Jimbo la
Nachingwea. “Tumefanikiwa kujenga shule ya sekondari katika kila kata na
jitihada za kuboresha zaidi elimu zinaendelea,” anasema.
Mtazamo
wa Waziri Chikawe ni kwamba uboreshaji wa huduma za jamii ni chanzo cha
kupiga vita umaskini miongoni mwa wakazi wa Jimbo la Nachingwea.
Mafanikio anayojivunia wizarani
Chikawe
anaelezea pia kuridhishwa kwake na jinsi anavyomudu majukumu katika
Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na viongozi wengine.
“Ninamudu
majukumu vizuri, nina Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Jaji Mkuu na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wote tunashirikiana vizuri, tunajivunia
tunachokifanya,” anasema.
Waziri
huyu anataja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika wizara hiyo
kutokana na juhudi zake kwa kushirikiana na viongozi wengine kuwa ni
kuongezwa kwa bajeti ya sekta ya sheria.
“Kwa
mfano, Mahakama na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali vimeboreshewa
incentive (marupurupu). Pia tumeanzisha Law School (Shule ya Sheria)
jijini Dar es Salaam na Rais anatarajiwa kuizindua hivi karibuni,”
anathibitisha.
Anaongeza
kuwa Wizara ya Katiba na Sheria chini ya uongozi wake imefanikiwa
kuwezesha ujenzi wa Mahakama Kuu katika mikoa ya Kagera na Shinyanga.
“Mwaka
huu pia tumejipanga kuanzisha ujenzi wa Mahakama Kuu katika mikoa
mitano, bajeti ipo na imeshapitishwa, tunaishukuru ofisi ya Hazina
inatuelewa. Tunataka kila mkoa uwe na Mahakama Kuu.
“Pia
sisi kama Wizara ya Katiba na Sheria tunasimamia mchakato wa mabadiliko
ya Katiba. Tume ya Warioba [Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba –
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba] inaendelea vizuri,” anasema.
Ataja changamoto
Waziri
Chikawe anataja changamoto kuu zinazomkabili kama mbunge wa
Nachingwea kuwa ni kuongeza juhudi za kuboresha huduma za jamii kama
vile elimu, maji, afya, umeme na barabara.
“Kuna
changamoto nyingine ninaiona, unaweza ukawajengea wananchi barabara na
shule, lakini kama hujawapa pesa baadhi ya wananchi wanaweza
wasiridhike. Lakini mimi ninaamini kuwa kazi ya mbunge ni kutafuta
maendeleo ya umma, si ya mtu binafsi,” anasema na kuongeza:
“Pia
kiwango cha rushwa kinakatisha tamaa, ni kikubwa, kwa sababu ukitaka
ardhi mtu anaomba rushwa, ukitaka shule mtu anaomba rushwa. Hata kule
mahakamani mambo hayoko very clean (shwari sana). Lakini mapambano
yanaendelea.
“Tumewaongezea
watu wa Mahakama marupurupu ili wafanye kazi vizuri. Tunaendelea
kupambana kuwezesha uboreshaji wa bajeti za sekta zote zilizo chini ya
Wizara ya Katiba na Sheria.”
Kwa
upande mwingine, Waziri Chikawe anasema kitendo cha Rais kumteua kuwa
Waziri wa Katiba na Sheria kinamfanya afarijike zaidi kwa kuwa kitaaluma
yeye ni mwanasheria.
“Mimi
ni mwanasheria, ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ninajisikia
vizuri, niko kwenye sekta yangu, mimi kuwa hapa [Wizara ya Katiba na
Sheria] ni kama umemtumbukiza samaki kwenye maji. Ninajivuna kuwa
nimefanya something (kitu fulani) kwa ajili ya maendeleo ya sekta yetu,”
anaeleza.
Ndoto yake
“Mimi
ni mwanasiasa, ndoto ya mwanasiasa siku zote ni kuendelea mbele. Maisha
ya mwanasiasa yanatawaliwa na vitu vitatu. Kwanza ni matakwa yako
mwenyewe, pili ni matakwa ya watu unaowaongoza na tatu ni majaliwa ya
Mwenyezi Mungu.
“Ninaweza nikataka mimi, wananchi wakakataa, wananchi wanaweza kutaka Mungu akakataa. Ukikubali hali hiyo hakuna shida.
“Kwa
hiyo, mimi kama mwanasiasa ni mtu wa kwenda mbele. Ndoto yangu ni
kuendelea for at least ten years (kwa angalau miaka kumi), bado nina
nguvu na moyo wa kuwatumikia wananchi,” anaeleza Waziri Chikawe.
Wito wake
Kiongozi huyu wa Wizara ya Katiba na Sheria anatumia nafasi ya mahojiano na JAMHURI pia kutoa wito kwa viongozi na wanachama wa CCM kuboresha ushirikiano na kujiimarisha katika sera na hoja za kisiasa.
Kwa
upande mwingine, anatoa wito kwa viongozi na wanachama wa vyama vya
siasa vya upinzani dhidi ya CCM kujenga utamaduni wa kuchangia mawazo
yatakayoiwezesha Tanzania kusonga mbele katika suala zima la maendeleo.
“Wapinzani
wasaidie kujenga kuliko kubomoa,” anasisitiza Waziri huyu wa Katiba na
Sheria. Kadhalika, anasema Serikali haina budi kuendelea kujitambua
kuwa ipo kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania walioikabidhi madaraka.
“Mfano,
minister (waziri) ni servant (mtumishi), viongozi sisi kazi yetu ni
kuwatumikia wananchi, Serikali nayo kazi yake ni kuwahudumia wananchi
wake. Serikalini si mahali pa kwenda kutafuta fedha, na viongozi tusiwe
mabosi bali tuwe watumishi,” anasisitiza.
Anaiambia
nini jamii? “Wito wangu kwa jamii nzima ni kwamba kila mtu anapoamka
afanye yanayowezekana kwa siku hiyo na ayafanye vizuri ayamalize, kwa
sababu jana haipo na kesho haipo, ipo leo na leo ndiyo siku ya kufanya
kila kitu. Nchi yetu itaendelea tukifanya hivyo, mimi ninafanya hivyo.”
Chikawe alikosoma
Mathias
Meinrad Chikawe anasema alizaliwa mwaka 1951. Alipata elimu ya awali
(chekechea) katika Shule ya St. Josephs Convent ya jijini Dar es Salaam
mwaka 1958.
Alipata
elimu ya msingi shuleni hapo kati ya mwaka 1959 na 1965 kabla ya
kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule hiyo hiyo mwaka
1966 hadi mwaka 1969 alipohitimu kidato cha nne.
Kati
ya mwaka 1970 na 1971 alipata elimu ya sekondari ya juu (kidato cha
tano na cha sita) katika Shule ya Mkwawa iliyopo mkoani Iringa. Mwaka
1972 alijiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Ruvu, kabla ya
kuchaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi mwaka 1975
alipohitimu digrii ya sheria.
“Mwaka
huo huo wa 1975 mara baada ya kuhitimu chuo kikuu niliajiriwa katika
ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, huku nikipata mafunzo ya vitendo
pia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Shirika la Sheria Tanzania
na Chuo cha Siasa Kivukoni hadi mwaka 1976 nilipohitimu nikaajiriwa
rasmi na kupangiwa kazi katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,”
anasema Chikawe.
Baadaye
alihamishwa kwenda kuwa Mwanasheria wa Wizara ya Kilimo, akiwasaidia
John Malecela na Joseph Mungai katika kipindi cha miaka 10 kabla ya
kuhamishiwa Ikulu ambako alifanya kazi kati ya mwaka 1985 na 1998, kabla
ya kuanza kujitosa kwenye siasa mwaka 1999. Huyu ndiye Mathias Meinrad.
SOURCE: JAMHURI MEDIA
|