Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Posted Jumatatu,Oktoba28 2013 saa 10:38 AM
Posted Jumatatu,Oktoba28 2013 saa 10:38 AM
Kwa ufupi
Kiongozi huyo wa UVCCM, alisema watu wa
Tanzania Bara wanaoishi Zanzibar, si wakimbizi kwa mujibu wa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Wanasema Serikali inatumia fedha nyingi
kugharimia matibabu ya kiongozi huyo nje ya nchini, kinyume na ahadi
yake ya kutotibiwa nje.
Zanzibar. Mwenyekiti wa Umoja wa
Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamis amesema baadhi
ya viongozi ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wameshindwa
kutekeleza wajibu wao.
Amesema wajibu huo ni pamoja na kushindwa
kutatua kero za madaktari na kusababisha kuzorota kwa huduma za afya
visiwani humo. Sadifa aliyasema hayo jana alipokuwa akihutubia mkutano
wa hadhara katika Uwanja wa Vuga katika Mkoa wa Mjini Magharibi,
Unguja.
“Serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa
kumhudumia kwa matibabu, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharrif
Hamad, itakumbukwa aliwahi kuwaahidi wananchi wa Zanzibar kuwa akiwa
kiongozi atahakikisha anatibiwa hapa hapa badala ya kusafirishwa nje ya
nchi,” alisema.
Wabara waishio Zanzibar
Kiongozi huyo wa UVCCM, alisema watu wa Tanzania
Bara wanaoishi Zanzibar, si wakimbizi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Sadifa alisema wapinzani wanaohoji uhalali wa watu
hao kuishi na kufanya kazi Zanzibar, hawafahamu haki ya kila mtu
kikatiba kwa maana ya kuwa huru kuishi na kufanya kazi katika sehemu
yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alisema ibara ya 11 na 26 ya
katiba imeweka wazi kwa kila Mtanzania ana haki ya kuishi sehemu atakayo
ndani ya Jamhuri ya Muungano.
Huku akishangiliwa na wanachama wa CCM alisema
sera za ubaguzi hazitasaidia kujenga amani na umoja wa kitaifa baada ya
kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Novemba mwaka 2010.
Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Shaka Hamdu
Shaka, alisema umoja huo umeamua kuchunguza kikundi cha watu wenye asili
ya India ambao wamekuwa wakipinga misingi ya Mapinduzi na Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar.
Alisema ni jambo la kushangaza kuona watu hao
wakiwa katika mstari wa mbele kuhoji uhalali wa Muungano wa Tanganyika
na Zanzibar, wakati hakuna muafrika anayeweza kwenda kuhoji uhalali wa
harakati za ukombozi wa India au Iran kama hali ilivyojitokeza visiwani
Zanzibar.
Alisema kitendo hicho hakikubaliki.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI