Posted Alhamisi,Juni20 2013 saa 21:55 PM
Kwa ufupi
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare, amesema mfumo wa
kuwatafuta wahalifu ndani ya Jeshi la Polisi ni dhaifu kwani pamoja na
kutuhumiwa kwa ugaidi matukio hayo yameendelea kuitikisa nchi katika
maeneo mbalimbali.
Akiwahutubia wananchi wa mjini Bukoba juzi katika
Uwanja wa Mashujaa, Lwakatare alidai kuwa aliwaeleza maofisa wa polisi
kuwa amegundua udhaifu wa kuhoji ili kubaini watuhumiwa na kutaka
salamu hizo zimfikie Mkuu wa Jeshi hilo Saidi Mwema.
Kwa mujibu wa Lwakatare jeshi hilo bado lina safari ndefu ya kuwapata watuhumiwa sahihi wa makosa ya ugaidi.
Alisema udhaifu uliopo ndiyo unaosababisha matukio hayo yaendelee kutokea na watu kupoteza maisha.
Alisema siku 92 alizoishi gerezani zimemfundisha
mambo mengi na kuwa atatumia siku zote atakazokuwa huru kutoa ushuhuda
wa mambo mbalimbali aliyoshuhudia.
Pia Lwakatare alimsifu kiongozi wa Jumuiya za
Kiisalamu, Shekhe Issa Ponda kuwa ni kiongozi shupavu aliyemfundisha
kuwa jasiri na mtu wa kumwomba Mungu baada ya kuishi naye gerezani kwa
siku kadhaa.
Akizungumzia hatima yake kisiasa, kiongozi huyo
alisema hana uhakika kama atagombea nafasi ya ubunge lakini alisema
hayuko tayari kung’oka Chadema badala yake ataendelea kupambana na
maadui waliomzunguka.
Lwakatare aliwasili mjini Bukoba kwa staili mpya
baada ya wananchi waliokuwa wamesubiri uwanja wa ndege tangu asubuhi
kutangaziwa kuwa kiongozi huyo angewasili kwa gari akitokea Mwanza.
Alipoulizwa kama mabadiliko hayo ya ghafla ilikuwa
ni kukwepa hujuma ambayo ingeweza kutokea wakati wa mapokezi yake,
Mwenyekiti wa Chadema Bukoba Mjini, Victor Sherejei alisema kuwa
Lwakatare alikosa ndege baada ya kufika Mwanza na hivyo kutumia gari ili
kuwahi mkutano.