Wednesday 19 June 2013

Serikali yanyooshea kidole wanasiasa mlipuko wa Arusha


“Sote tunajiuliza kwa nini wananchi waliwashambulia na kuwazuia askari wasitimize wajibu wao, badala ya kuwasaidia ili wamkamate mhalifu. Je, ilitokea kwa bahati mbaya au ilipangwa?” Waziri William Lukuvi 
Na Waandishi Wetu  (email the author)

Posted  Jumatatu,Juni17  2013  saa 20:30 PM
Kwa ufupi
  • Ni kuhusu mlipuko wa bomu uliotokea katika mkutano wa kuhitimisha kampeni za Chadema mjini Arusha.


Dodoma. Serikali imetoa kauli yake ya awali jana, kuhusu mlipuko wa bomu uliotokea katika Kata ya Soweto, mkoani Arusha wakati wa mkutano wa Chadema wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani mkoani humo.
Shambulio hilo lilipoteza maisha ya watu wawili na wengine zaidi ya 70 kujeruhiwa.
Tamko la Serikali kuhusu kadhia hiyo, lilitolewa jana bungeni na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi baada ya kipindi cha maswali na majibu.
Katika tamko hilo, Serikali imevinyooshea kidole baadhi ya vyama vya siasa, taasisi za kijamii na watu binafsi (bila kutaja majina) kuwa vinahusika.
Lukuvi alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mlipuko huo ulikuwa wa bomu la kurushwa kwa mkono na kwamba aina ya urushaji wa bomu hilo hautofautiani na mbinu iliyotumika katika shambulio la Mei 5 mwaka huu katika Kanisa la Olasiti jijini Arusha.
Serikali pia imetangaza zawadi ya Sh100 milioni kwa watakaowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa na mtandao wao.
Zawadi hiyo inakuja huku Serikali ikiunda timu ya wataalamu wa kuchunguza tukio hilo.
Timu hiyo itaongozwa na Kamishna Paul Chagonja wa polisi ikishirikisha pia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
“Katika siku za karibuni, zimekuwepo jitihada za makusudi za baadhi ya vyama vya siasa, makundi ya kijamii na watu binafsi kupandikiza chuki kwa raia dhidi ya vijana wetu wa Jeshi la Polisi, kuwafanya raia wawachukie askari, kuwafanya raia wasiwaamini askari, kuwafanya raia wasiwape ushirikiano askari na hatimaye kuwa na taifa ambalo halitawaliki,” alisema Lukuvi.
Alisema mlipuko huo ulikuwa wa bomu la kurushwa kwa mkono na kwamba lilirushwa kutoka upande wa Mashariki kuelekea Magharibi kulikokuwa na gari aina ya Fuso lililokuwa linatumika kuhutubia.
Kuhusu kutoroka kwa mtuhumiwa aliyerusha bomu hilo, Lukuvi alisema ni matokeo ya uchochezi unaofanywa kwa makusudi na baadhi ya wanasiasa dhidi ya Serikali na polisi. “Sote tunajiuliza kwa nini wananchi waliwashambulia na kuwazuia askari wasitimize wajibu wao, badala ya kuwasaidia ili wamkamate mhalifu. Je, ilitokea kwa bahati mbaya au ilipangwa?”alihoji waziri huyo.
Alisema shambulio hilo la Soweto limehama kutoka kanisani (Olasiti) kwenda kwenye mikutano ya kisiasa ikiwa na nia ya kuwafanya Watanzania wachukiane, wapigane na taifa liparaganyike.

Alisistiza kuwa baadhi ya wanasiasa kwa bahati mbaya au kwa kujua na kushiriki mpango huo wamekuwa wakitoa kauli mfululizo za kuendeleza chuki za kijamii wakidhani wanajiimarisha kumbe wanapanda mbegu ya uharibifu kwa taifa.
“Serikali imepania kuwasaka na kuwatia mbaroni wahusika wa shambulio hilo la watu waovu. Kupitia Bunge hili nataka niwaambie wahalifu hao kuwa njama zao za kutugawa kwa misingi ya dini, makabila rangi, rasilimali na itikadi za vyama kuwa zitashindwa.
“Tutapambana nao usiku na mchana, kwa silaha zote tulizonazo mpaka tutakapowashinda na kuwafikisha mbele ya mikono ya sheria,” alisema.
Wabunge waomba mwongozo
Baada ya Lukuvi kuwasilisha kauli hiyo ya Serikali, wabunge wanne wa vyama vya upinzani, Kombo Khamis Kombo (CUF), David Kafulila, Felix Mkosamali na
Moses Machali wa NCCR-Mageuzi waliomba Mwongozo wa Spika. Katika mwongozo wake, akitumia kanuni ya 47 Machali aliomba Bunge liruhusiwe kujadili suala hilo akieleza kuwa kwa mujibu wa mitandao ya kijamii inaonekana kuwapo kwa malumbano kati ya vyama vya CCM na Chadema vikitupiana mpira kuhusu tukio hilo.
Alikwenda mbali zaidi na kutaka
kufanyika kwa uchunguzi na chama kitakachobainika kuhusika Msajili wa Vyama vya Siasa akifute.
Kwa upande wake, Kafulila alisema kauli ya Lukuvi inaashiria kwamba anajua sababu za tukio hilo.
Kombo aliitaka Serikali itoe maelezo kuhusu matukio kama hilo yaliyotokea Zanzibar, akisema ukimya wa Serikali unawafanya wananchi kutoielewa.


Spika Makinda
Hata hivyo baada ya wabunge hao kuomba mwongozo, Spika wa Bunge Anne Makinda alisema kuwa kutokana na uzito wa tukio hilo ameitisha kikao cha Kamati ya Uongozi kujadili suala hilo.

Chanzo: Mwanachi newspaper