Posted Jumatatu,Juni17 2013 saa 21:51 PM
Kwa ufupi
Nchi yetu imeandika tena historia mbaya katika
masuala ya usalama kutokanana mlipuko wa bomu uliotokea jijini Arusha
Jumamosi iliyopita, wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
kilipokuwa kikihitimisha kampeni zake za uchaguzi mdogo wa udiwani
katika Viwanja vya Soweto jijini humo.
Taarifa zinasema watu kadhaa wamepoteza maisha
hadi sasa japokuwa idadi yao bado haijafahamika kutokana na mamlaka
mbalimbali kutoa taarifa zinazokinzana huku watu kwa makumi nao
wakijeruhiwa, miongoni mwao vibaya.
Bomu hilo lililipuka muda wa jioni yapata saa 12
muda mfupi kabla ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kumaliza
kuhutubia mkutano huo na kusababisha taharuki kubwa na baadaye
sintofahamu miongoni mwa wakazi wa Arusha na Tanzania nzima kwa ujumla.
Itakumbukwa kwamba hili ni tukio la pili katika
kipindi cha mwezi mmoja na nusu kutokea jijini Arusha katika mkusanyiko
wa watu, kwani Mei 5 mwaka huu bomu lililipuka katika Kanisa Katoliki la
Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasit jijini Arusha na kuua
watu watatu na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Kwanza tunawapa pole wale wote ambao wameguswa kwa
namna moja au nyingine na tukio hili; wale walioondokewa na wapendwa
wao, waliojeruhiwa na uongozi wa Chadema.
Ni tukio baya, linalosikitisha ambalo linapaswa
kulaaniwa na kila mpenda amani wa nchi yetu. Kwa mara nyingine amani ya
nchi yetu imetiwa doa.
Tafsiri ya tukio hili ni kwamba usalama wetu sasa
kama Watanzania uko shakani. Ilitarajiwa kwamba baada ya tukio la
mwanzoni mwa mwezi jana, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vingefanya
kazi kubwa ya kuchunguza na kubaini chimbuko la uhalifu huu wenye sura
ya ugaidi na kuudhibiti kabla haujaathiri watu wengi zaidi!. Lakini
jambo la kushangaza ni kwamba umetoekea mlipuko mwingine katika muda
mfupi tangu utokee wa kwanza katika mji huo huo na katika mazingira
yanayofanana na yale ya awali kwa maana ya mkusanyiko mkubwa wa watu.
Hapa kuna maswali mengi yanayohitaji majawabu
sahihi kwamba vyombo vyetu vya usalama vimelifanyia kazi kwa kiasi gani
tukio la Mei 5 mwaka huu, kwa lengo la kupata taarifa za kuwezesha
kuchukua hatua za kiusalama kwa wakazi wa Arusha?
Kutokea tena kwa mlipuko Jumamosi jioni, ni
dhahiri kwamba Wanausalama wetu wameshindwa kuwalinda wakazi wa Arusha
na huu ni udhaifu mkubwa katika mifumo ya usalama wa nchi yetu na watu
wake.
Tunasema hivi tukirejea matukio kadhaa ya uhalifu
ambayo Jeshi la Polisi liliyaundia tume kwa ajili ya kuyachunguza ili
kuwezesha hatua kuchukuliwa. Lakini ni dhahiri kwamba tume hizi ama
zimeshindwa kufanya kazi yake na kutoa taarifa zenye tija au kama
taarifa zake zipo basi hazifanyiwi kazi.
Tume hizi ni kama hazina tija na badala yake zinaongeza mzigo wa gharama kwa walipakodi.
Katika mazingira haya ni dhahiri tunahitaji
mabadiliko makubwa (reforms) katika utendaji wa polisi na vyombo vingine
vya usalama. Vyombo hivi vinapaswa kufahamu kwamba vina dhamana ya
kuhakikisha wananchi wanakuwa salama. Hiyo ndiyo kazi yake na jukumu
lake kubwa na siyo kin