Sunday 16 June 2013

Habari Kuu : Ugaidi tena Arusha, bomu lajeruhi na kuua

                   
                       


Mama akikimbizwa hospitali kupata matibabu 
Na Mussa Juma na Moses Mashala, Mwananchi  (email the author)

Posted  Juni15  2013  saa 23:36 PM
Kwa ufupi
Bomu hilo lililipuka jana saa 11:50 dakika chache kabla ya Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe kumaliza kuhutubia mkutano huo uliofanyika katika Viwanja vya Soweto mjini Arusha na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.

Arusha. Mkutano wa Chadema wa kumaliza kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani mjini Arusha, jana ulivunjika baada ya bomu kulipuka na kuua watu wanne na wengine kujeruhiwa.
Bomu hilo lililipuka jana saa 11:50 dakika chache kabla ya Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe kumaliza kuhutubia mkutano huo uliofanyika katika Viwanja vya Soweto mjini Arusha na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.
Hilo ni tukio la pili la bomu kulipuka katika mkusanyiko wa watu, Mei 5 mwaka huu bomu lililipuka katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasit mjini Arusha na kuua watu watatu na wengine kujeruhiwa.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru Frida Mokiti alisema katika hospitali yake kuna maiti moja ya mtoto na majeruhi 11.
Habari zingine zilisema katika hospitali ya Misheni ya Selian kuna maiti za watu wawili, waliokufa kutokana na shambulio hilo na majeruhi ambao idadi yao haijafahamika.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema katika tukio hilo watu wawili wamepoteza maisha, mwanamke na mwanamume na kwamba idadi ya majeruhi bado haijafahamika kwa kuwa wametawanywa katika hospitali mbalimbali mkoani humo.
Watu walioshuhudia tukio hilo waliliambia gazeti hili kuwa bomu hilo lililipuka karibu na jukwaa walilokuwa wamekaa viongozi wa Chadema, wakati Mbowe na Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema wakiwa katika hatua za kumaliza kuhutubia.
Taarifa zilidai kuwa kuna mtu alionekana akirusha kitu kinachodaiwa bomu kwenye eneo la jukwaa karibu na gari la matangazo la chama hicho, lakini alipokuwa akifuatiliwa baada ya kutokea mlipuko huo, polisi nao walikuwa wameanza kudhibiti watu kwa kulipua mabomu ya kutoa machozi na kupiga risasi za moto hali iliyozidisha taharuki.
Baada ya tukio hilo watu waliokuwa katika mkutano huo walitawanyika wakikimbia kuokoa maisha yao huku wakimwacha Mbowe na Lema na viongozi wengine wakiwa bado wako jukwaani.
Hali hiyo ilifanya barabara zote za mji wa Arusha kujaa watu waliokuwa wakikimbia ovyo.
Hali hiyo ya watu kukimbia ovyo kuliwafanya askari polisi wengi kuingia mitaani kudhibiti watu na hivyo nao kulazimika kutumia mabomu ya machozi hali ambayo ilizidisha taharuki.
Baadhi ya watu waliojeruhiwa walikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru na wengine katika Hospitali ya Seliani na wafuasi wa Chadema na watu wengine waliokuwa katika eneo hilo.


Miongoni mwa watu waliojeruhiwa katika tukio hilo la mlipuko wa bomu ni Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa ambaye amelazwa katika hospitali ya Selian.
Mbowe akizungumza katika hospitali ya Selian jana aliwataka wanachama wa chama hicho watulie kwa sababu tukio hilo ni kubwa na lina mambo mengi ndani yake.
Alisema wanachofanya sasa ni kuhakikisha kuwa watu waliojeruhiwa katika tukio hilo wanapata matibabu kwanza.
Mbowe aliwataka watu wote waliopotelewa na ndugu kufika katika hospitali zote za mji wa Arusha kutambua ndugu zao waliojeruhiwa.
Alisema Chadema itagharimia matibabu ya watu wote waliojeruhiwa katika tukio hilo.
Mbowe alisema chama chake kwa sasa hakiwezi kutoa tamko lolote kuhusiana na tukio hilo la bomu kwa sababu wanafuatiliwa na baadhi ya askari polisi na maofisa wa Usalama wa Taifa.
Katika hospitali ya Selian, Mganga wa zamu, Dk Ekenywa alisema kuwa hospitali hiyo imepokea majeruhi 25 ambao wanaendelea kupatiwa matibabu.
Waandishi wa habari walishuhudia baadhi ya wanachma wa Chadena pamoja na viongozi wao akiwamo Mbowe wakitoa damu kwa ajili ya majeruhi.
Awali Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe jana alihitimisha kampeni kwa chopa katika Kata ya Makuyuni, wilayani Monduli na kukumbana na mkutano wa kampeni wa CCM uliokuwa ukihutubiwa na Mbunge wa Jimbo hilo, Edward Lowassa.
Viongozi hao, walifanya mikutano katika kata hiyo na kila chama kilitamba kushinda leo na kuwaondoa wananchi na hofu za kutokea vurugu.
Mbowe licha ya kufanya mkutano huo, pia alifanya mikutano katika Kata ya Kaloleni Uwanja wa Soweto mjini Arusha na mamia ya wakazi wa Arusha wa kata zote nne na mkoani Manyara, katika kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani unaofanyika katika kata mbalimbali nchini.
Uchaguzi mdogo wa kata nne za Jiji la Arusha na Kata ya Makuyuni, wilayani Monduli, unatarajiwa kufanyika leo.

Uchaguzi wa Kata ya Makuyuni, unafanyika kuziba nafasi ya Diwani wa CCM, Abdilah Warsama aliyefariki dunia, kata nne za Jiji la Arusha, uchaguzi unafanyika kutokana na waliokuwa madiwani wa Chadema kufukuzwa uanachama kwa tuhuma za kukisaliti chama hicho.
Vyama vilivyosimamisha wanaogombea udiwani ni CCM, Chadema na CUF. Kwa upande wa CCM ni Emanuel Meliali (Kaloleni), Emmannuel Laizer (Elerai), Edna Jonathan Sauli (Kimandolu) na Victor Mkolwe (Themi) .
Chadema wanaogombea ni Melance Kinabo “Kaburu” (Themi), Emmannuel Kessy (Kaloleni), Jeremiah Mpinga (Elerai) na Rayson Ngowi (Kimandolu).
Kwa upande wa CUF waliosimamishwa kugombea ni Abbas Mkindi Darwesh (Kaloleni) John Bayo (Elerai) na Lobora Ndarvoi (Themi).
Kampeni
Kampeni za uchaguzi huo, mdogo, zilikuwa na upinzani mkubwa na kwa Jiji la Arusha, wakati Chadema, ilikuwa ikiongozwa na mbunge wa jimbo hilo, Godbless Lema, CCM iliwatumia vigogo wake wote wa juu wa chama hicho.
Vigogo hao waliokuwa Arusha ni Naibu Katibu Mkuu, Mwigulu Nchemba, Katibu wa Uenezi na Itikadi, Nape Nnauye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Abdalah Bulembo.
Wengine waliokuwa Arusha ni Naibu Waziri wa Tamisemi, Agrey Mwanri, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano), Stephen Wassira na wabunge kadhaa wakiongozwa na mbunge wa Simanjiro, Christopha ole Sendeka.
Kata ya Makuyuni
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole alisema jana kuwa chama hicho, kina uhakika wa ushindi katika Kata ya Makuyuni na kata nne za Arusha.
“Tumefanya kampeni kwa amani na utulivu na nina imani ya ushindi mkubwa hasa hapa Makuyuni,” alisema Nangole.

Mbowe aliwataka wakazi wa kata hiyo, wasiwe na hofu wajitokeze kupiga kura leo. Kwa upande wa Lowassa, ambaye ameweka kambi katika kata hiyo, pia alitoa wito kwa wakazi wa kata hiyo, kujitokeza kwa wingi kupiga kura leo.
Kwa pamoja viongozi hao ambao walipishana muda mfupi, Mbowe akianza kupita na baadaye Lowassa kuhitimisha mkutano, kila mmoja alitamba chama chake kushinda leo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Nape alisema chama hicho kina imani na ushindi leo na alipongeza kampeni kuwa za amani.
“Tuna imani polisi wataimarisha ulinzi leo,” alisema Nape.
Nape jana jioni, alitarajiwa kuhitimisha kampeni mkoani Manyara.
Lema akizungumza katika mikutano jana, alisema wana imani Chadema itaibuka na ushindi katika kata zote.
Mbowe katika kata hiyo, jana alifanya mkutano mfupi baada ya kutua kwa chopa, akitokea mkoani Manyara.