Posted Alhamisi,Juni20 2013 saa 22:11 PM
Kwa ufupi
Tanzania ambayo kwa muda mrefu imejinadi kuwa ni
kisiwa cha amani, utulivu na mshikamano, inapitia katika kipindi kigumu
mno pengine kuliko kingine chochote katika historia yake tangu ipate
uhuru mwaka 1961.
Ni katika kipindi hiki cha mpito ambacho nchi yetu
imeshuhudia kuzuka kwa matukio mengi yakiwamo yale yanayoashiria
uvunjifu wa amani, vurugu za hapa na pale na harakati nyingine nyingi
zilizojitokeza katika maeneo mbalimbali.
Tumeshuhudia kwa mfano, matukio ya Mtwara ambayo
yamesababisha uharibifu mkubwa kwa mali na maisha ya watu na hivi sasa
Arusha ambako milipuko ya bomu imetumiwa kusababisha umwagikaji wa damu
ya watu wasio na hatia.
Machafuko kama hayo pia yamewahi kutokea mkoani
Iringa zaidi ya mara moja na pia katika Mkoa wa Morogoro na kote huko
damu ilimwagika. Wakati hayo yakitokea, kumezuka mtindo wa kurushiana
makombora ya lawama kunakofanywa na wanasiasa au viongozi wetu wakiwamo
wa chama tawala, CCM kwa upande mmoja na wale upinzani hasa Chadema, kwa
upande mwingine.
Wote wameshambuliana na kutuhumiana kuhusu vyanzo
au sababu za matukio hayo ambayo yamezidi kujitokeza na kuchafua sifa ya
taifa hili.
Maneno mengi yamesemwa kuhusu matukio hayo, kiasi
kwamba kupitia safu hii tumejitahidi kuweka wazi msimamo wetu kwamba
hatuiungi mkono mizozo na migogoro ambayo inazidi kujitokeza.
Tunasema nchi yetu inahitaji utulivu, umakini, busara katika kutatua mizozo na migogoro ambayo imejitokeza.
Hata leo bado tunashauri kuwa kamwe hakutakuwa na
mshindi wa moja kwa moja katika mizozo hii inayoendelea nchini mwetu na
kuhusisha wanasiasa, viongozi, wanaharakati au hata wananchi.
Tunaamini, kauli hizi ambazo zimekuwa zikitolewa
na viongozi wa ngazi mbalimbali za kisiasa hazina tija. Tujielekeze
kwenye utatuzi wa mizozo au migogoro ambayo inaota mizizi na siyo
kuikuza. Ni vyema viongozi wetu wote, wale walioko madarakani au wa
vyama vya siasa wawe makini kwa kauli na ndimi zao zinazoweza
kuisambaratisha nchi.
Tunasema kauli zinazochochea vyombo kama polisi
kujichukulia sheria mkononi kwa kisingizio cha kutuliza ghasia, kuleta
amani kwa vyovyote vile hazikubaliki, hata kama zimetolewa na kiongozi
mkubwa au mwenye ushawishi kiasi gani.
Viongozi wa vyama vya siasa na Serikali, watumie
nafasi zao kuwaeleza wananchi na wanachama wao kuheshimu sheria na
kuzitii bila shurti, kama kaulimbiu ya Jeshi la Polisi inavyosema.
Kwa upande mwingine, vyombo vya dola ikiwamo
polisi navyo viongozwe na misingi ya sheria, taratibu au kanuni za
kuanzishwa kwao, siku zote vitimize wajibu wao kwa umma tena kwa
uadilifu usiotiliwa shaka. Siku zote vijiepushe kuwa chanzo au sababu za
kuendelea kwa vurugu hizi ambazo zinajitokeza katika maeneo mbalimbali
ya nchi yetu.
Tunavishauri vyombo hivi vikumbuke jambo hili kila mara
vinapotimiza wajibu wao, vijiepushe na kutumiwa na watu, vikundi vya
watu, wanasiasa au viongozi hata kama ni wale walioko madarakani kwa
maslahi yao wenyewe. Tunasema kwamba moto hauwezi kuzimwa kwa kumwagiwa
mafuta bali, kwa maji au vifaa rasmi vya kazi hiyo.
Hivyo, tunasema viongozi wetu wajitambue, wachunge ndimi, kauli zao ambazo nyingine zinaweza kuwasha moto badala ya kuuzima.