Kwa ufupi
Dodoma/Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
ameagiza vyombo vya dola kuwashughulikia kwa kuwapiga wale watakaokataa
kutii amri wakati wakifanya vitendo vya uvunjifu wa amani.
Akizungumza katika Kipindi cha Maswali ya Papo kwa
Hapo kwa Waziri Mkuu, bungeni Dodoma jana, Pinda alisema watu
wanapokaidi wanajitakia matatizo na vyombo vya dola.
Alisema hayo alipokuwa akijibu swali la nyongeza
la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu aliyeuliza:
“Serikali ipo tayari kiasi gani kubainisha na kuchukua hatua stahiki,
badala ya kusakama makundi fulani, tujue chanzo halisi cha vurugu hizi
na matatizo haya na jinsi gani vyombo vya dola vinavyoshughulikia kwa
sababu yapo malalamiko katika baadhi ya maeneo kama Mtwara kwamba
wananchi wanapigwa na vyombo vya dola?”
Waziri Mkuu alijibu: “Ni lilelile nililosema...
mwishowe unaona anasema vyombo vya dola vinapiga watu. Ukifanya fujo,
umeambiwa usifanye hiki, ukaamua kukaidi, utapigwa tu... hamna namna
nyingine, maana wote tukubaliane kwamba nchi hii tunaiendesha kwa
misingi ya kisheria.
“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni
imara zaidi... wewe ndiyo jeuri zaidi watakupiga tu.... Mimi nasema
muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine... maana tumechoka.”
Pinda alisema Serikali imedhamiria kurejesha amani
nchini ikiwamo mkoani Mtwara na kuwataka Watanzania waiache Serikali
ifanye kazi hiyo. Alisema Serikali ina orodha ya watu wanaosemekana kuwa
ni vyanzo vya vurugu na matatizo yaliyotokea Mtwara na kushangaa wale
wanaopinga kukamatwa kwao.
“Lazima tuwakamate na kama katika kuwakamata
watafanya jeuri, jeuri, watapigwa tu kabla ya kupelekwa tunapotakiwa
kuwapeleka, kwa sababu hatuwezi kuendelea na hali hii, mkadhani kwamba
tutafika tunapokwenda. Nami nasema vyombo vya dola vijipange imara
vihakikishe vinadhibiti hali hii,” alisema.
Hata hivyo, jibu hilo lilipata upinzani wakati
Mbunge wa Konde (CUF), Khatibu Said Haji alipomwuliza Waziri Mkuu: “Hapo
awali umetoa kauli nzito ya kuliambia taifa hili kwamba wale raia wote,
ambao watakaokuwa wakaidi wapigwe tu na watapigwa tu; naomba ninukuu
Katika Ibara ya 13 na Kifungu cha 6B cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
“Ni marufuku kwa mtu yeyote aliyeshtakiwa kwa kosa
la jinai kuteswa kama mtu mwenye kosa, mpaka itakapothibitika anayo
hatia kwa kutenda kosa hilo.
“Pia ibara hiyohiyo Kifungu cha 6 E; kinasema ni
marufuku kwa mtu yoyote, kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu
zinazoweza kumdhalilisha. Kwa kauli yako uliyoitoa huoni kwamba umevunja
Katiba?” Akijibu swali hilo, Pinda alisema ni lazima kutofautisha kati
ya mtu aliyekwishakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria...
“Mimi ninayemzungumza hapa ni mtu yule ambaye ameamua kufanya vitendo
hajakamatwa na ndiyo maana nilikwambia usiandamane... hapa mahali
hutakiwi kwenda wewe ukaamua kutumia mabavu kwa sababu mko wengi, ndiyo
maana nikasema, hawa watu tutashughulika nao hivyohivyo.”
Mbunge huyo hakuridhishwa na majibu hayo na kumtaka Waziri Mkuu kuyafuta.
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda
aliingilia katika na kumweleza mbunge huyo kuwa kila mtu alikuwa
amemwelewa Waziri Mkuu na hakukuwa na haja ya kuendelea na hoja hiyo.
Kabla ya swali lake la nyongeza, Mangungu aliuliza: “Ukisikiliza
nyimbo nyingi za taifa katika Afrika zinasema hekima, umoja na amani
ndiyo ngao zetu. Je, hali ambayo imejitokeza katika nchi yetu na
matatizo yaliyojitokeza Arusha na maeneo mengine kama Mtwara. Nini tamko
la Serikali?
Waziri Mkuu alijibu: “Swali lililoulizwa na
Mheshimiwa Mangungu ni jambo linalotugusa sisi wote. Suala la amani,
ulinzi, utulivu ndiyo hasa tunu ya kila nchi ingependa kuwa nayo. Ni
kweli hivi karibuni kumejitokeza vurugu za hapa na pale kwa hiyo
angependa tuwaeleze Watanzania kama Serikali tunafikiria tufanye nini.
Alisema ipo haja ya jukumu hilo kuachwa kwa
viongozi wa kisiasa bila ya kujali itikadi zao... “Yako mambo ambayo
lazima tukubali kwamba ni jukumu letu sisi wote na kila mmoja lazima
azungumze lugha moja.
Ninyi wote ni mashahidi. Chadema waliposhinda
hapa, wao walikuja waziwazi, wakasema tutahakikisha nchi hii
haitawaliki. Sasa, inawezekana pengine ndiyo mwendelezo wa utekelezaji
wa kauli hizo.
“La pili ni upande wa Serikali, lazima tuhakikishe
kwamba wale wote ambao kwa kweli wanajaribu kuvunja amani kwa namna
yoyote ile, kazi kubwa tuliyonayo ni kubanana, kupambana kwelikweli kwa
njia zozote zile zinazoonekana zinastahili.
“Sasa mimi ninaomba sana Watanzania, maana kila
juhudi zinapoonekana zinaelekea huko, unapata watu wengine wanajitokeza,
unajua...unajua. Acheni Serikali itimize wajibu wake kwa sababu jambo
hili ni la msingi, lazima tulilinde kwa nguvu zetu zote.
“Rai yangu kwa Watanzania kila mmoja ajue kwamba
siku tukiingia katika vurugu, hakuna mshindi. Wote tutaumia, sasa wote
tuhakikishe hili jambo tunalisimamia vizuri.”
Chadema waja juu
Akizungumzia kauli hiyo, Mkurugenzi Habari na
Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema: “Kauli ya Pinda inakiuka Katiba
ya nchi na imethibitisha kwamba matumizi mabaya ya vyombo vya dola na
kusababisha mauaji ya raia yana baraka za Serikali.”
Alisema kauli ya Pinda kama ilivyokuwa ya Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi
zinatoa mwelekeo kwamba mauaji ya Arusha yana baraka za Serikali.
Wanasheria wakerwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema Waziri Mkuu hakustahili
kutoa kauli kama hiyo.
Alisema Pinda hapaswi kuwa na jazba, bali anatakiwa kuwa na
busara na kuzungumza kwa kuzingatia sheria za nchi badala ya kutoa
matamshi ambayo siyo mwafaka kwa nchi inayoongozwa kwa kufuata sheria na
taratibu.
Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS),
Francis Stola alisema kauli hiyo ya Waziri Mkuu, mbali ya kwenda kinyume
cha Katiba na sheria ya nchi, inaweza kuhatarisha amani.
Stola alisema matumizi ya nguvu kupita kiasi kudhibiti hali yoyote korofi hayaruhusiwi.