Kinana amfungulia mashtaka Mch. Msigwa.
KATIBU Mkuu wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdul-rahman Kinana amemfungulia kesi Mbunge
wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), kutokana na kumtuhumu
anajihusisha na ujangili na biashara haramu ya pembe za ndovu.
Kinana amefungua kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam
kutokana na kitendo cha Mbunge huyo kutoa tuhuma hizo dhidi yake kwa
nyakati tofauti nje na ndani ya Bunge, pia alikataa kuzikanusha na
kumuomba radhi.
Inadaiwa kuwa Aprili 21 mwaka huu Msigwa ambaye ni Waziri Kivuli wa
Maliasili na Utalii alitoa tuhuma hizo kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika katika Shule ya Msingi Mbuguni wilayani Nyamagana mkoani
Mwanza.
Aidha alizitoa bungeni wakati akiwasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani
katika Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka
2013/2014. Katika hati ya madai, Kinana anadai kuwa kutokana na tuhuma
hizo ameharibiwa tabia yake, uaminifu, hadhi yake kitaaluma na weledi na
kumfanya achukiwe na kudharauliwa katika jamii.
Anadai jina lake na heshima ambayo ameijenga kwa muda mrefu,
vimeharibiwa na Msigwa kwa nia mbaya, pia kwa tuhuma hizo anazosisitiza
kuwa ni za uwongo, licha ya kumsababishia maumivu ya kisaikolojia, pia
zimemsababishia hasara ya fedha.
Anadai kuwa kabla ya tuhuma hizo alikuwa katika hatua za mwisho za
mchakato wa mazungumzo ya mradi wa ubia wa kilimo cha mboga na mwekezaji
kutoka kampuni ya nje, lakini tuhuma hizo zimesababisha kampuni hiyo
kuvunja majadiliano hayo.
Kinana anadai kuwa sababu iliyotolewa na kampuni hiyo kuvunja mazungumzo
hayo ni kutajwa kwake na mbunge huyo kuwa ni jangili anayejishughulisha
na biashara hiyo.
Kwa mujibu wa hati ya madai, Mradi huo ulikuwa na thamani ya Dola za
Marekani milioni nne, Hisa za ushiriki wa Kinana zilikuwa ni asilimia 25
katika kipindi cha miaka mitano hivyo anatathmini kuwa amepata hasara
ya Sh milioni 350.
Kinana anaiomba Mahakama hiyo imwamuru Msigwa amlipe fidia ya Sh milioni
350 kama hasara rasmi, pamoja na fidia ya maudhi na fidia ya hasara
ikiwemo gharama za kesi.
Aidha anaiomba Mahakama imwamuru amlipe riba kwa kiwango kitakachopangwa
na Mahakama, tangu tarehe ya hukumu hadi malipo ya mwisho, imwamuru
kufuta tuhuma dhidi yake na kumuomba radhi kwa kuchapisha katika
magazeti mawili ya Kingereza na mawili ya Kiswahili yanayosambazwa
nchini.
Pia Mahakama itoe zuio la kudumu kumzuia Msigwa, au wakala wake kutoa au
kuchapisha taarifa zozote za kashfa dhidi yake. Katika hati ya madai
amenukuu baadhi ya kauli za Msigwa, ikiwemo "Kinana (naomba waandishi wa
habari mnisikie na nyie Usalama wa Taifa mkapeleke habari) hana sifa za
kupita barabarani na kuwaambia Watanzania waiamini CCM. Kinana mikono
yake si misafi."
"Hata kwenye Nassaco, Shirika la Meli Tanzania kuna harufu ya ufisadi
ndani yake; ajibu hoja...Kinana meli zake ndizo zinazohusika kubeba
pembe za ndovu nchini. hajajibu hoja hizo! Kwa siku nchi hii
tembo 67 wanauawa. Hao ndio wanaokifadhili Chama Cha Mapinduzi, halafu
wanakuja eti kuwashawishi Watanzania muwasikilize na kwamba Chama Cha
Mapinduzi eti ni kizuri."
".Haya mambo ninayoongea ni hatari kwa sababu haya yote ni majangili ni
organized Crime. Ni mtandao wa Kimafia, uko duniani kote, unaweza
ukatuua lakini wabunge tumesimama tunawatetea..."
chanzo : Jamii forum.