Dar na Dodoma: Serikali jana ilitangaza Bajeti
yake kuu kwa mwaka wa fedha 2013/14 ambayo inaashiria machungu kutokana
na ongezeko la kodi na ushuru katika baadhi ya bidhaa, zikiwamo mafuta,
soda, vinywaji vikali pamoja na leseni za magari.
Akisoma bajeti hiyo bungeni jana, Waziri wa Fedha,
Dk William Mgimwa pia alitangaza kuanzisha kodi na ushuru katika huduma
mbalimbali zinazotolewa kupitia simu za mkononi, ikiwamo kodi ya zuio
ya asilimia 10 ya kamisheni (commission) ya usafirishaji wa fedha.
“Serikali itaanza kutoza ushuru wa bidhaa wa
asilimia 14.5 kwenye huduma zote (all mobile phone services) za simu za
kiganjani/mkononi badala ya muda wa maongezi tu (airtime alone),”
alisema Dk Mgimwa na kuongeza: “Katika ushuru huu, asilimia 2.5
zitatumika kugharimia elimu nchini.”
Kutokana na hali hiyo, Mtafiti kutoka Taasisi ya
Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF), Dk Oswald Mashindano amelaumu kile
alichokiita kuwa ukubwa wa kodi hasa kwa wasio na kipato kikubwa ili
kufidia uendeshaji wa Serikali.
“Kama kawaida kutakuwa na ongezeko la mapato ya
Serikali kutoka katika vyanzo vyake hasa ukusanyaji wa kodi. Inamaanisha
kuwa kutakuwa na mzigo mkubwa kwa walipakodi hasa kundi la wenye kipato
kidogo.
“Tofauti na nchi zilizoendelea ambazo wenye mitaji
mikubwa ndiyo wanaobanwa kulipa kodi zaidi, nchi zinazoendelea,
Tanzania ikiwamo, kuna udhaifu mkubwa wa kukusanya kodi,” alisema Dk
Mashindano.
Mafuta na magari
Waziri Mgimwa alisema katika mwaka ujao wa fedha,
Serikali itapandisha ushuru wa mafuta ya dizeli kutoka Sh215 kwa lita
hadi Sh217 kwa lita, likiwa ni ongezeko la shilingi 2.
“Tumeongeza Sh2 tu kwa kuwa tunatambua tukiongeza
ushuru mkubwa kwa magari makubwa ambayo yanatoa huduma kwa jamii,
tutawaumiza wananchi,” alisema Dk Mgimwa.
Kadhalika, ushuru wa mafuta ya petroli umeongezwa
kwa Sh61, kutoka Sh339 kwa lita hadi Sh400. Hata hivyo, imeongeza
kiwango cha ushuru wa mafuta (fuel levy) kutoka shilingi 200 kwa lita
hadi shilingi 263 kwa lita, sawa na ongezeko la shilingi 63 kwa lita na
wakati huohuo mafuta hayo yakiongezewa Sh50 kwa kila lita, fedha
zitakazotumika kuchangia mfuko wa kusambaza umeme vijijini.
Wakala wa Umeme Vijijini (Rea), umeongezewa kiasi
cha Sh186.9 bilioni ambazo awali, hazikuwa zimetengwa baada ya Serikali
kukubaliana na mapendekezo ya Bunge kupitia Kamati yake ya Bajeti,
inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
Serikali pia imepandisha viwango vya ada ya mwaka
ya leseni za magari. Magari yenye ujazo wa injini yenye ukubwa wa kati
ya cc 501 na 1500 yatatozwa Sh150,000 kutoka Sh100,000 za sasa.
hadi Sh200,000 wakati magari yenye ujazo wa injini zaidi ya cc 2501 yatatozwa Sh250,000 kutoka kiwango cha sasa ambacho ni Sh200,000.
hadi Sh200,000 wakati magari yenye ujazo wa injini zaidi ya cc 2501 yatatozwa Sh250,000 kutoka kiwango cha sasa ambacho ni Sh200,000.
Hata hivyo, uamuzi huo hautazigusa bajaji na
pikipiki (maarufu kama bodaboda) kwani Dk Mgimwa alisema vyombo ambavyo
injini zake zina ujazo chini ya cc 501, ambavyo havitatozwa ada ya
leseni. Ushuru pia umeongezwa kwenye magari yasiyokuwa ya uzalishaji na
yenye umri wa miaka 10 kutoka asilimia 20 mpaka hadi asilimia 25. Dk
Mgimwa alisema hatua hiyo imelenga kupunguza uagizaji wa magari
chakavu ili kulinda mazingira na kupunguza ajali za mara kwa mara.
Pombe na Sigara
Bidhaa zisizokuwa za mafuta ambazo zimefanyiwa
marekebisho na kuongezwa kodi ni mvinyo, pombe, vinywaji vikali na
sigara. Vimeongezwa kodi kwa asilimia 10.
Ongezeko la kodi kwa kipimo cha lita moja ni kwa
vinywaji vikali ambayo imepanda kutoka Sh2,392 hadi Sh2,631, sawa na
ongezeko la Sh239, bia inayotengenezwa kwa nafaka za nchini ambayo
haijaoteshwa, imepanda kutoka Sh310 hadi Sh341, sawa na ongezeko la Sh31
kwa lita wakati bia nyingine zote zimepanda kutoka Sh525 hadi Sh578
sawa na ongezeko la Sh51.
Vinywaji baridi vimepanda kutoka Sh83 kwa lita hadi Sh91 sawa na ongezeko la Sh8 kwa lita.
Sigara zenye kichungi na zinazozalishwa nchini
zimepanda kwa asilimia 75, kutoka Sh19,410 hadi Sh21, 351 kwa sigara
1,000 sawa na ongezeko la Sh1.94 na senti 94 kwa sigara moja.
Mabadiliko ya Sheria
Ili kutekeleza uamuzi wa kuongeza ushuru na kodi,
Dk Mgimwa amependekeza kufanya maboresho ya sheria mbalimbali za kodi
ambazo ni za; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Kodi ya Mapato, Ushuru
wa Bidhaa, Ushuru wa Mafuta, Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Sheria
ya Usalama Barabarani. Nyingine ni Sheria za; Petroli (Petroleum Act),
Uwekezaji Tanzania, Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na
marekebisho mengine madogomadogo katika baadhi ya sheria za kodi.
Dk Mgimwa alisema mabadiliko ya Sheria ya
Uwekezaji yanalenga kutoza asilimia 25 ya ushuru wa forodha unaopaswa
kutozwa kwenye bidhaa zinazotambulika kama “Deemed Capital Goods” (yaani
kutoa msamaha wa kodi wa asilimia 75 kwenye bidhaa hizo badala ya
asilimia 90 za sasa) na kuondoa baadhi ya bidhaa kwenye orodha ya kupata
msamaha.
“Bidhaa hizo ni zile ambazo hazina uasilia wa kuwa
bidhaa za mtaji kama vile vifaa vya ofisi, samani, sukari, vinywaji
(viburudisho), bidhaa za mafuta ya petroli, magari madogo (Non Utility
Motor Vehicles), viyoyozi, majokofu, na vifaa vya kielektroniki,
mashuka, vijiko, vikombe nk,” alisema waziri huyo. Alisema marekebisho
hayo pia yanalenga kupunguza misamaha ya kodi na kubakiza misamaha yenye
tija na yenye kuchochea uwekezaji mkubwa katika sekta za uchumi za
kimkakati, hivyo kuongeza mapato ya Serikali.
Alisema pato la taifa linatarajiwa kukua kutoka
asilimia 7.0 mwaka 2013 hadi asilimia 7.2 mwaka 2014 na wakati huohuo,
bei zikitarajiwa kubaki kwenye viwango vya tarakimu moja na mfumuko wa
bei kushuka hadi asilimia 6.0 Juni 2014.
Kuhusu akiba ya fedha za kigeni, Dk Mgimwa alisema katika mwaka
ujao wa fedha Serikali itajitahidi kuwa na akiba itakayoweza kukidhi
mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi
kisichopungua miezi minne.
Alisema jitihada zitafanywa ili kupunguza tofauti
ya viwango vya riba vya kuweka na kukopa na kuimarisha thamani ya
shilingi na kuwa na kiwango imara cha ubadilishaji wa fedha
kitakachotokana na mwenendo wa soko la fedha.
Mbowe, wabunge
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa
Hai, Freeman Mbowe alisema: “Bajeti ya mwaka huu haina jipya” kwani
Serikali imeendelea kupandisha kodi katika bidhaa zilizozoeleka badala
ya kusimamia kodi kwenye rasilimali za nchi.
“Bajeti hii inaonyesha Serikali ilivyokosa ubunifu
wa vyanzo vya mapato, kila mwaka wanapandisha kodi kwenye bia, sigara,
magari na mafuta,” alisema Mbowe.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi na Mbunge wa Kuteuliwa,
James Mbatia alisema sheria ya ununuzi ikirekebishwa kama alivyoahidi
Waziri Mgimwa itasaidia kupunguza gharama ya bidhaa mbalimbali.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya alisema
kuongezwa kwa fedha za mfuko wa vijana ni ukombozi kwa kuwa miaka mingi
kilio hicho hakikusikika.
“Tunaona sasa Serikali imekuwa sikivu kwa kuwa kwa
muda mrefu tuliomba lakini hatukupewa,” alisema baada ya Serikali
kuongeza Sh3 bilioni kwa ajili ya mfuko.