Kwa ufupi
Hakimu huyo pia aliwataka washtakiwa
kusalimisha hati zao za kusafiria mahakamani na kutokutoka nje ya Dar es
Salaam bila ya kuwa na kibali cha Mahakama.Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare (mbele) akisindikizwa na wafuasi wa chama hicho kutoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana baada ya kuachiwa kwa dhamana. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam. Baada ya kusota rumande kwa takriban miezi mitatu, hatimaye Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare ameachiwa kwa dhamana.
Hata hivyo, mwenzake Joseph Ludovick ambaye
wanashtakiwa pamoja, alikwama kupata dhamana baada ya wadhamini wake
kushindwa kuwa na vielelezo vyenye vigezo kulingana na masharti ya
dhamana
hivyo alirejeshwa rumande.
Baada ya Lwakatare kuachiwa, alipokewa kwa shangwe
na wafuasi wa Chadema waliokuwa na mabango yenye maandishi mbalimbali
ya kuelezea furaha yao na mengine yakikiponda chama tawala CCM, huku
wakimshangilia kwa kuimba: “peoples’ power... peoples’ power!” wakiwa na
maana ya nguvu ya umma.
Akitoa uamuzi kuhusu dhamana hiyo, Hakimu Mkazi wa
Mahakama ya Kisutu, Aloyce Katemana alisema imetolewa baada ya
kuzingatia kigezo cha washtakiwa kufutiwa mashtaka ya ugaidi ambayo
yalikuwa yanaangukia kwenye sheria inayozuia dhamana.
Aliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika na wanaotoka katika taasisi zinazotambulika kisheria.
Sharti lingine ni kila mdhamini kutia saini hati ya udhamini ya Sh10 milioni pamoja na washtakiwa wenyewe.
Hakimu huyo pia aliwataka washtakiwa kusalimisha
hati zao za kusafiria mahakamani na kutokutoka nje ya Dar es Salaam bila
ya kuwa na kibali cha Mahakama.
Hakimu Katemana aliiahirisha kesi hiyo hadi Juni
24, mwaka huu itakapotajwa tena kwa lengo la kujua iwapo upelelezi
umekamilika ili ipangiwe tarehe ya kuanza kusikilizwa.
Awali, uamuzi huo wa dhamana ulipangwa kutolewa
Mei 13, mwaka huu lakini ulikwama baada ya Katemana kuripotiwa kuwa
likizo na badala yake, Hakimu Mkazi Sundi Fimbo aliitaja tu kesi hiyo na
kuiahirisha.
Mei 27, mwaka huu ilitajwa tena hata hivyo uamuzi wa dhamana haukutolewa.
Awali, Lwakatare kupitia kwa mmoja wa mawakili
wanaomtetea, Peter Kibatala aliwasilisha maombi ya dhamana mahakamani
hapo Mei 13, mwaka huu wiki moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam kumfutia mashtaka matatu ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili.
Pamoja na dhamana hiyo, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) tayari
ameandaa maombi ya marejeo katika Mahakama ya Rufaa akipinga uamuzi wa
Mahakama Kuu wa Mei 7, mwaka huu kuwafutia mashtaka ya ugaidi washtakiwa
hao.
Katika maombi hayo, DPP anaiomba mahakama hiyo
iitishe majalada ya kesi hiyo na kuchunguza uhalali wa uamuzi huo wa
Mahakama Kuu, uliotolewa na Jaji Lawrence Kaduri.
Anadai kuwa katika hati ya maombi ya washtakiwa
hao waliyowasilisha Mahakama Kuu, hapakuwepo na maombi ya kufuta
mashtaka na kwamba hapakuwa na taarifa zilizowasilishwa dhidi ya
washtakiwa ambazo Mahakama Kuu ingezizingatia katika kufikia uamuzi.
Hata hivyo, jopo la mawakili wa Lwakatare nalo
liliwasilisha pingamizi la awali dhidi ya maombi hayo ya DPP,
likiainisha hoja mbili ambazo mawakili wake watazitoa wakati wa
usikilizwaji wa maombi hayo.
Lwakatare anadai kuwa maombi hayo ya marejeo yana
dosari ambazo haziwezi kurekebishwa kutokana na kushindwa kuambatanisha
nakala ya mwenendo wa uamuzi unaolalamikiwa ambao ndipo maombi hayo
yalipojengwa na kwamba kiapo kinachounga mkono maombi hayo kimehusisha
mambo mengine yasiyohusika.
Chanzo : Mwananchi.co.tz
Chanzo : Mwananchi.co.tz