Kwa ufupi
Pamoja kuwa nje ya ulingo wa siasa,
ameendelea kuwa kiongozi anayeheshimika na mchango wake wa mawazo
umekuwa ukithaminiwa duniani kote.“Usinipigie simu, nitakupigia.” Hayo ni maneno aliyosema Rais wa
zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela alipotangaza kustaafu maisha ya
siasa na kuhudumia jamii.
Mandela alisema kuwa hataki kupigiwa simu ya
kualikwa sehemu yoyote isipokuwa, ikiwa anahitaji kuwapo atapiga simu
kuomba ashirikishwe.
Tangu wakati huo ameonekana hadharani mara chache.
Mwaka 2010, ofisi yake ilitoa picha ikimwonyesha kiongozi huyo akiwa na
viongozi wa vyama vya soka vya Marekani na Afrika Kusini.
Pamoja kuwa nje ya ulingo wa siasa, ameendelea
kuwa kiongozi anayeheshimika na mchango wake wa mawazo umekuwa
ukithaminiwa duniani kote.
Kwa miaka miwili sasa hali yake kiafya
imetetereka. Mwanzoni mwa mwaka 2011, alilazwa katika hospitali moja
huko Johannesburg kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.
Mzee Mandela amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya
uambukizi katika mapafu. Inaelezwa kuwa alipofungwa katika gereza la
Robben miaka ya 1980, aliwahi kuugua ugonjwa wa TB.
Hata hivyo mwanzoni mwa mwaka jana, alipatiwa
matibabu mengine kwa madai kuwa alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya
tumbo. Katika miezi ya karibuni maambukizi katika mapafu ndiyo yamekuwa
yakimsumbua.
Mandela alizaliwa Julai 18, 1918 na kupewa jina la
Rolihlahla Dalibhunga huku akipewa jina la ukoo Madiba. Jina la Nelson
alipewa na mwalimu wake.
Baba yake, Henry Mandela aliyekuwa kiongozi wa Kabila la Thembu, alifariki wakati Madiba akiwa na umri wa miaka minane.
Mwaka 1941, akiwa na umri wa miaka 23, Madiba
alikimbilia Johannesburg, baada ya kutakiwa amuoe binti aliyechaguliwa
na wazee kijijini kwake.
Miaka miwili baadaye alijiunga na Chuo cha
Witswaterand University kusomea sheria, huko alikuwana na watu
mbalimbali ambao walimfungua macho na hapo ndipo mwamko wake kisiasa
ulianza.
Mwaka huohuo alijiunga na Chama cha African
National Congress (ANC), baadaye alishirikia kuanzisha tawi la vijana la
chama hicho, ‘ANC Youth League’.
Alifunga ndoa na mke wake wa kwanza, Evelyn Mase, mwaka 1944 na
walifanikiwa kupata watoto wanne. Ndoa yake na mwanamke huyo ilidumu kwa
miaka 14 na waliachana mwaka 1958.
Mzee Mandela alipata leseni ya kuwa Mwanasheria
mwaka 1952. Akishirikiana na rafiki yake Oliver Tambo walifungua ofisi
inayoshughulikia masuala ya kisheria katika Jiji la Johannesburg.
Akiwa na rafiki yake huyo, walipambana kuondoa
utawala wa kibaguzi nchini Afrika Kusini kwa miaka mingi. Mwaka 1959
yeye na washirika wake walishtakiwa kwa makosa ya uhaini. Hata hivyo,
kesi yao ilifutwa baada ya miaka minne.
Mandela alipohukumiwa kifungo cha maisha katika
kipindi cha miezi 18 ya mwanzo, mama yake mzazi na mtoto wake walifariki
dunia. Hata hivyo hakuruhusiwa kushiriki mazishi hayo.
Maisha ya Mandela
Nelson Mandela ni mmoja wa viongozi wanaoheshimika zaidi duniani kutokana na juhudi zake za kupigania usawa na demokrasia.
Alifungwa kwa miaka 27, aliachiwa huru mwaka 1990
na kuwa Rais wa Kwanza mweusi wa Afrika Kusini. Miaka minne baadaye
aliachia wadhifa huo. Alishinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka 1993.
Watu waliomfahamu Mandela kwa miaka mingi wanasema
kuwa ni mtu anayeipenda familia yake kuliko kitu kingine, hata wakati
alipostaafu alisema anataka muda uliobaki autumie akiwa na familia yake.
Akiwa na umri wa miaka 80 alifunga ndoa na Graca
Machel akisema kuwa anataka kuiunganisha familia yake baada ya kuachana
na mkewe wa pili, Winnie Mandela.
Na Julieth Kulangwa kwa msaada wa Mashirika ya Habari