Sunday, 15 September 2013

IRENE DAVID: Binti aliyejiajiri kuuza matunda Dar


Imeandikwa na Christopher Gamaina, Dar es Salaam   
Ijumaa, Septemba 13, 2013 07:34
IRENE DAVID:
. Alikataa kutoa rushwa ya ngono aajiriwe
. Awaasa mabinti, wanawake wanaojiuza


Ni binti mrefu wa wastani, mwenye rangi ya maji ya kunde na umri wa miaka 23. Ni mhitimu wa kidato cha nne na fani ya kompyuta ngazi ya cheti, aliyejiajiri kuuza matunda. Binti huyu si mwingine yeyote bali ni Irene David, mkazi wa Mbagala, jijini Dar es Salaam. Ana kawaida ya kutabasamu anapozungumza na mtu.
Katika hali ya kawaida, hasa kwa mazingira ya hapa nchini si rahisi kuona binti mwenye umri mdogo kama huyu na mwenye wazazi amejiajiri na kujigharamia mahitaji muhimu ya chakula, mavazi na malazi. Kwa Irene hilo limewezekana.

Wakati baadhi ya mabinti na wanawake wamechagua maisha ya kujidhalilisha kwa kujiingiza katika biashara haramu ya kujiuza, Irene ameapa kulinda maadili na kutokwepa jukumu la kutumia njia halali kujitafutia riziki ya kujikimu maishani.

Ameanza na ujasiriamali wa kuuza matunda yaliyofungashwa kwenye sahani za plastiki, lakini ana ndoto ya kumiliki duka kubwa la bidhaa za urembo, achilia mbali kujiendeleza kielimu.

Kilichomsukuma kuuza matunda.
Katika mahojiano maalum na JAMHURI Dar es Salaam wiki iliyopita, Irene hakuficha kilichomsukuma kuanza biashara hiyo. Ni tukio ambalo hatalisahau maishani.

Anasema mwanzoni hakuwa na wazo la kujianzishia biashara yoyote bali alitamani kuajiriwa kufanya kazi yoyote iliyo halali. Lakini dhamira hiyo hatimaye ilimfikisha katika mazingira yaliyomkatisha tamaa, baada ya mwajiri katika kampuni fulani kumwomba rushwa ya ngono ili amwajiri.

Kwamba mwajiri huyo mwenye asili ya India (jina tunalihifadhi) alimpigia Irene simu kumtaka wakutane siku iliyofuata katika jengo fulani lililopo Mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam, lakini alipokwenda alishuhudia tukio analosema hatalisahau maishani.

“Nilikuwa nimeshapeleka ofisini kwake barua ya kuomba kazi yoyote kwenye kampuni yake. Basi nilipofika katika jengo alilonielekeza nilimkuta akanikaribisha kwenye chumba ambacho nilikiona kama siyo ofisi maana hakikuwa na kiti.

“Alifunga mlango kisha akaanza kunihoji huku tukiwa tumesimama. Aliniuliza kiasi cha fedha ninachotaka kulipwa baada ya kuwa ameniajiri kwenye kampuni yake (jina tunalo) nikamweleza. “Pale ndani kulikuwa na laptop [kompyuta mpakato], mara akatoa simu yake mfukoni akafungua picha za X [ngono] akaniambia niangalie akimaanisha tufanye mambo hayo, mimi nikamwambia sipendi mambo hayo. Naye akaniambia 'basi siwezi kukulazimisha'. Nikamwambia nataka kuondoka akasema 'sawa', nikaondoka,” anasema Irene.

Anasema hakuona sababu ya kukubali kudhalilishwa kijinsia na utu wake kiasi hicho wakati ana akili timamu na uwezo wa kufanya kazi halali za kujipatia fedha za kujigharamia mahitaji yake. Binti huyu anasema kutoka hapo alianza kufikiria jinsi ya kujiajiri katika biashara yoyote ndogo. “Kwa kuwa nilikuwa na shilingi elfu hamsini niliyokuwa nimelipwa baada ya kufanya usafi katika ofisi moja kwa siku kadhaa, nikaamua kuanza biashara hii ya kuuza matunda,” anasema.

Anavyoendesha biashara
Irene anasema ameanza biashara hiyo Agosti, mwaka huu na kwamba huamka saa 10:00 alfajiri na kutumia usafiri wa daladala kutoka Mbagala kwenda kununua matunda sokoni Buguruni, jijini Dar es Salaam.

Ananunua na kuuza matunda ya aina mbalimbali yakiwamo maembe, mapapai, machungwa, maparachichi, matango, ndizi, matikiti maji na karoti. “Nikishanunua matunda kule Buguruni huwa ninatumia pia usafiri wa daladala kwenda eneo la Posta na ninakaa sehemu tulivu kwa ajili ya kuyamenya, kuyakatakata na kuyafungasha tayari kwa kuyauza,” anaeleza. Kwa kawaida Irene hutembeza biashara hiyo katika ofisi mbalimbali eneo la Posta kati ya saa 2:00 asubuhi na saa 10:00 jioni. Anauza sahani moja yenye matunda mchanganyiko kwa bei ya Sh 1,500.

Anaeleza kuridhishwa na biashara yake hiyo akibainisha kuwa inamwingizia faida ya wastani wa Sh 15,000 kwa siku, na kwamba idadi ya wateja wake inaongezeka siku hadi siku kutokana na kauli yake nzuri, uaminifu na uzingatiaji usafi.

Anaongeza kuwa mbali ya kumudu kujilipia kodi ya chumba, kipato kinachotokana na biashara hiyo kimemwezesha kununua samani na vyombo muhimu vya ndani na kulipia huduma za umeme na maji. Anataja kero pekee anayokutana nayo wakati wa kutembeza matunda kuwa ni baadhi ya watu wanaomwomba namba yake ya simu ya kiganjani. “Unakuta watu wengine shida yao ni kuniomba namba ya simu badala ya kununua matunda. Lakini huwa nakataa kuwapa maana nilishaogopa kutokana na kile kitendo alichonifanyia yule Mhindi,” anasema.

Alivyofika Dar es Salaam
Binti huyu alihamia jijini Dar es Salaam kujitafutia maisha akitokea jijini Mwanza, baada ya kupata baraka za wazazi wake. Alipofika jijini Dar es Salaam Irene alipokewa na dada yake (hakumtaja) anayeishi eneo la Mbezi, ambako alipata hifadhi kwa miezi kadhaa kabla ya kuamua kupanga chumba eneo la Mbagala baada ya kupata uwezo wa kujitegemea.

“Niliwaomba wazazi wangu ruhusa wakakubali nikawaaga, nikaondoka Mwanza kuja Dar es Salaam. Ingawa kwa sasa baba anataka nirudi nyumbani, lakini ninataka kujitegemea maana hana uwezo wa kunisomesha,” anasema Irene.

Ndoto zake
“Siwezi kubeza biashara hii ya kuuza matunda, lakini nina mpango wa kufanya biashara nyingine kama kuwa na duka kubwa la urembo,” anasema Irene na kuongeza: “Pia nikipata mdhamini wa kunigharamia masomo, nitasoma. Ninapenda kujiendeleza kielimu, ninatamani kusomea ualimu ili nifundishe hata shule za English medium.
“Lakini hata nikiolewa sitaki kuwa mama wa nyumbani. Mara nyingi nakutana na vijana wanaosema wanataka kunioa, lakini mimi ninawaambia sasa hivi kuna matapeli wengi, anayetaka kunioa apeleke posa kwa wazazi wangu, siyo kuoana barabarani.”

Awaasa mabinti, wanawake
Huku akizungumza kwa makini zaidi, Irene ametoa wito kwa mabinti na wanawake kujihadhari na vitendo vya kujiuza, kwani vinahatarisha afya na maisha. Badala yake wajenge dhana ya kujishughulisha na biashara halali katika jamii.

“Mabinti na wanawake wasione aibu kujishughulisha na biashara halali, hata kama ni kuuza karanga ilimradi maisha yanakwenda. Ukijiuza unahatarisha na kufupisha maisha yako,” anasisitiza. Kwa upande mwingine, anawashauri mabinti na wanawake kupenda kazi za kujiajiri kuliko za kuajiriwa, ambazo wakati mwingine zinazungukwa na mazingira ya unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia unaofanywa na waajiri walioporomoka kimaadili.

Lakini pia binti huyu anatoa wito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusimamia ipasavyo sheria zinazokataza unyanyasaji wanawake kijinsia, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinadhalilisha utu na kudhoofisha maendeleo ya wanawake nchini. “Sheria ichukue mkondo wake dhidi ya waajiri wanaoendekeza uovu wa kuwanyanyasa watoto wa kike, mabinti na wanawake kijinsia,” anasema Irene na kuongeza:

“Hili tatizo la wanawake kunyimwa ajira kwa sababu tu wamekataa kutoa rushwa ya ngono kwa waajiri likomeshwe, vinginevyo Tanzania bila ukimwi haitawezekana.”

Alisoma wapi?
Irene anasema alipata elimu ya msingi katika Shule ya Mbugani jijini Mwanza kati ya mwaka 2000 na 2006. Alijiunga katika Shule ya Sekondari ya Mbugani mwaka 2007 na kuhitimu kidato cha nne mwaka 2010.

“Mwaka 2011 niliunga na chuo cha mafunzo ya kompyuta wilayani Sengerema kinachojulikana kwa jina la Sengerema Tele Centre, nikahitimu mafunzo hayo ngazi ya cheti mwaka 2012,” anaongeza. Irene.

SOURCE: JAMUHURI MEDIA