'Kutegemea kubaya kupita kote ni kutegemea mtu mwingine kwa mawazo
Katika
sehemu iliyopita, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alisema hata angekuwa
anafuata sera za kibepari, angejenga viwanda. Anasema mabepari ndiyo
walioanza kujenga viwanda, na viwanda vyenyewe havikuwa na sera.
Ifuatayo ni sehemu ya hotuba ya Mwalimu aliyoitoa katika kilele cha
Sherehe za Mei Mosi, mwaka 1995 mkoani Mbeya.Juzi
juzi, wakati nipo pale Dodoma , vijana walinikumbusha. Mwalimu,
ulipotoka, uliacha viwanda vya nguo vya umma kumi na viwili. Kati ya
viwanda hivyo kumi na viwili, kumi vimefungwa na viwili vilivyobaki
kimoja hatujui hata kama kitapata pamba. Tusipoangalia, vyote viwili
vilivyobaki vitafungwa.
Juu ya Mashirika ya Umma
Nataka
kusema kidogo juu ya hiki kitu kinachoitwa mashirika ya umma. Sijui
yananuka? Hata hivyo, hata kama yananuka, nataka kujua kwa nini
yananuka. Lazima tujiulize kwa nini yananuka. Sababu ya kusema hivi ni
kwamba mimi nilikuwa sijui, lakini vijana walinikumbusha wakaniambia
“Mwalimu, ulipondoka, uliacha kumi na mbili”, Mimi kitu kimoja
nilichokuwa nakifikiria ni kwamba sasa viwanda vyetu vya nguo vilikuwa
vinafikia shabaha ile tuliyokuwa tunataka ya kuweza kutumia asilimia
themanini na tano (85%) ya pamba hapa nyumbani.
Nilipowauliza
vijana kwa nini viwanda kumi vimefungwa na viwili vilivyobaki vipo
katika hatari ya kufungwa, nilielezwa kwamba kuna sera inayoitwa sera ya
ubinafsishaji. CCM wasiogope sana , na ninyi mniwie radhi kwa kusema
CCM, maana ndiyo yenye serikali inayotawala.
Sasa
mimi nifanyeje? Wala CCM wasije wakaninung’unikia, maana ndicho chama
kinachotawala, na wale wa vyama vingine wasije wakasema “mbona Mwalimu
umesema kama unaipendelea CCM? Aka! Kama wanataka niwabomoe, naweza
kuwabomoä, lakini sitaki.
Mimi
nataka kueleza hali yetu ilivyo hivi sasa na nataka kusema; mosi,
tunatoka wapi, tuko wapi na tunataka kwenda wapi. Pili, kama tunataka
kwenda huko, tufanye nini tusije tukashitukia tunapelekwa mahala ambako
siko tunakokusudia kwenda. Na hiyo ndiyo shabaha yangu.
CCM imebadili sera ya Azimio la Arusha
CCM
imebadili sera ya Azimio la Arusha. Mimi sina ugomvi hata kidogo.
Naweza kusema nina ugomvi wa kiitikadi, ingawa sijasema “mbona mnaacha
sera yetu ina ubaya gani?” Aidha, sina ugomvi wa msingi wa kitaifa kwa
sababu mnaweza mkaacha Azimio la Arusha na baadaye mkajenga uchumi imara
tu kwa manufaa ya wananchi. Ziko namna nyingi za kufanya hivyo na si
lazima kufuata Azimio la Arusha.
Sera za CCM
Sasa
CCM wanazo sera ambazo zimefafanuliwa katika kakitabu haka kanakoitwa
Mwelekeo wa Sera za CCM katika Miaka ya Tisini. Hii imetengenezwa na
ndiyo marekebisho ya Azimio la Arusha. Ndiyo sera yao mpya baada ya
kusahihisha Azimio la Arusha. Kuna sehema ninayotaka kuitumia kueleza
hayo ninayotaka kuyaeleza ambayo inahusu mashirika ya umma.
Sera ya ubinafsishaji wa mashirika ya Umma
Kuhusu mashirika ya umma, sera yake inasema. “Mashirika
ambayo ni ya msingi na nyeti kwa maendeleo ya taifa kama bandari, reli,
posta ma simu, nishati na mabenki ya umma yaliyopo, yaendelee
kumilikiwa na dola. Hata hivyo, wananchi wataweza kuuziwa sehemu ya hisa
katika mashirika hayo yote na mashirika haya yanaweza kuingia ubia na
makampuni binafsi, mradi tu kwa uwiano unaolifanya shirika kuendelea
kuwa la dola”. Mimi nilipokuwa nasoma jana nikaafiki na kukubali.
Sina ugomvi na hilo na sina ugomvi kabisa kwani ndivyo tulivyosema
katika Azimio la Arusha. Lakini mambo haya lazima yabadilike. Sasa sina
ugomvi na hili.
Pili: “Mashirika
ya umma ambayo yanaendelea kwa ufanisi lazima yaendelee kuwa ya dola
kwa lengo la kuendelea kuwashirikisha wananchi katika umilikaji. Mipango
itaandaliwa ya kuwawezesha wananchi kununua hisa katika mashirika hayo.
Pia mashirika ambayo yanahitaji mtaji au kupenyeza sayansi na
teknolojia ya kisasa yataweza kuingia katika ubia ili kutimiza azma
hiyo. Aidha, kwa mashirika ambayo serikali italazimika kumiliki,
mashirika haya itabidi yaendeshwe kibiashara”. Mimi nakubali mia kwa mia, sina maneno na wala sioni tatizo na hilo .
Tatu: “Kwa
upande wa mashirika ambayo yanaweza kufanya shughuli zake kwa faida
lakini yana matatizo mbalimbali kama ya ukosefu wa mtaji, madeni makubwa
katika mabenki, menejimenti mbovu na kadhatika, dola itachukua hatua ya
kulazimika kuondoa menejimenti mbovu, kuimarisha mtaji kwa kuwauzia
wananchi hisa na kuingia ubia na vyombo vingine vya kiuchumi au
kuyakodisha kwa mteja mwenye uwezo wa kuyaendesha kwa faida”. Mimi hiyo bado naikubali na sina matatizo.
Nne: “Mashirika
yaliyo sugu [“mashirika yaliyo sugu” tena Kiswahili kizuri sana ] kwa
kufanya shughuli kwa hasara yatakodishwa, ama kuuzwa au kufungwa kwa
kutilia maanani zaidi jawabu ambalo ni la maslahi zaidi kwa taifa”.
Sasa mimi nasema hilo bado nalikubali kwani shughuli hii imekuwa
inaendelea. Nimesikia kwamba shirika, halikuwa ni shirika la umma,
lilikuwa ni Benki ya Ushirika na Maendeleo Vijijini (CRDB), peke yake
ndicho chombo cha namna hiyo ambacho kimepitapita kuuza hisa. Mengine
sijayasikia, yanaweza kuwa yapo.
Uuzaji wa mashirika ya umma
Uuzaji
wa mengine, ambayo sivyo sera inavyosema [sera haisemi mashirika
yanayoendeshwa kwa faida yauzwe hata kidogo], sijui yanavyouzwa. CRDB
wamepita kwangu pale wameniomba ninunue hisa. Nitapata wapi mimi? Hata
hivyo, wamepitapita wanaomba watu wanunue hisa; wanakwenda kwenye vyama
vya ushirika na wanawaomba watu binafsi. Angalau, hicho ni kitendo cha
kushirikisha watu ambacho wamekifanya na watu wametumia fursa hiyo kama
sera inavyosema.
Mengine
tunasikia yanakwenda tu. Eti sasa ni kwamba, kwa mfano, kile Kiwanda
cha Sigara, ni cha umma ni chetu wote pamoja. Najua wewe huna hisa, mimi
sina hisa na wala hakuna mtu mwenye hisa. Lakini ni cha umma na
kinafanya shughuli zake kwa faida.
Tofauti kati va shirika ya umma na shirika/kampuni binafsi
Nimechukua
mfano wa kiwanda ambacho kinafanya shughuli zake kwa faida. Kama
kinafanya shughuli zake kwa faida, wote tunapata faida. Chukua mfano wa
viwanda viwili vinavyoendeshwa vizuri na vinapata faida. Kimoja kama
kile cha sigara na cha pili ni cha watu binafsi. Sasa tofauti yake ni
nini? Hiki cha watu binafsi kinalipa kodi ya serikali na hiki cha umma
kinalipa kodi ile ile na kwa mujibu wa sheria ile ile. Kwa hiyo, hivyo
vyote vinalipa kodi ile ile juu ya faida kwa asilimia ya faida zao kwa
mujibu wa sheria. Baada ya kodi, pato lililobaki linagawanywa kwenye
hisa. Kile cha umma pato lake linakwenda kwa serikali: kwa umma. Hiki
kingine, faida yake inakwenda kwa watu binafsi wachache.
Ndiyo
maana, mpaka leo, mimi napendelea hiki cha umma zaidi kuliko kile cha
watu binafsi. Vyote vinafanya biashara nzuri tu na vinalipa kodi ya
serikali kama kawaida na vinawapa faida iliyobaki wenye kiwanda. Hata
hivyo, hicho cha kwanza, cha umma kinawapa faida iliyobaki wenye kiwanda
hicho ambao ni umma, na msimamizi wake ni serikali. Kwa hiyo, serikali
ndiyo inayochukua mapato yake kwa niaba ya wananchi wake. Mimi mpaka
leo, hata ninyi mngesemaje, bado nakipenda hiki cha umma.
Tukitaka kuongeza viwanda vya watu binafsi, tuongeze tu!
Kama
tunasema sasa hivi tunataka kuongeza vile viwanda vya watu binafsi,
tuongeze tu! Nani atatuzuia? Ongezeni vile vya watu binafsi. Viongezwe
kwa wingi kabisa! Hata hivyo, mnapochukua hiki cha umma, kwa maana
niliyoieleza, mkasema eti mnataka sasa kiwe cha wananchi moja kwa moja
ili na mimi Nyerere niseme “sasa nina hisa pale”, mimi siafiki. Watu
wangapi mtakuwa na hisa? Hebu niambieni, wangapi?
Mnachukua
mali yetu wote kabisa, kiwanda cha sigara kile kina mali , kinapata
faida na serikali inaitumia kuongezea fedha za kodi na tunaifanyia kazi
ya umma. Mnavyosema leo ni kwamba mmegundua njia moja nzuri zaidi ya
kushirikisha wananchi katika uchumi. Mimi nawambineni: ongezeni viwanda.
Muwashawishi
wananchi wa Tanzania waongeze viwanda. Wasaidieni kuongeza viwanda.
Lakini, hiki cha wote, mnataka kuwapa watu wachache, halafu mnasema
ndiyo ushirikishaji? Mimi sielewi maana yake. Hii ni mali yetu wote
pamoja: ni mfuko wa pamoja tunachota inatusaidia katika elimu, afya na
mahitaji mengine.
Sasa
hivi tunayo matatizo ya ukusanyaji kodi. Kiwanda hiki hakina matatizo
hata kidogo. Kinaendeshwa vizuri kwa faida. Kwa hiyo, tunacho chombo
ambacho kinatoa faida. Kinatusaidia. Leo shule na hospitali zina
matatizo kwa sababu kodi mbalimbali hazikusanywi. Lakini kiwanda hiki
kinalipa kodi yake kama kawaida. Miongoni mwa wale wanaokwepa kulipa
kodi, si mmoja wao. Viwanda vya umma si mmoja wapo hata kidogo. Vinalipa
kodi zake kama kawaida, havikwepi kulipa hata senti moja. Halafu,
kinapopata faida, tunabaki nayo na tunafanya shughuli za wananchi. Hiki
mnasema leo tukigawanye tuwashirikishe wananchi kwa kukimiliki moja kwa
moja. Wangapi mtamiliki: ninyi wangapi? Itakuwa ni kuchukua fulani na
fulani tu! Kiwanda ambacho ni chetu wote kabisa na faida itakapobaki,
badala ya kwenda Hazina, iende kwa wewe na mimi!
Ndiyo
tumekibinafsisha na hii ndiyo sera mpya ya kuleta manufaa Tanzania !
Hii ndiyo mbinu mpya imegunduliwa? Ujamaa mpya huo! Huo ni unyang’anyi
tu wa mali yetu wote.
Kutegemea mtu mwingine kwa mawazo ni kubaya kupita yote kabisa
Hili
ni jambo la upumbavu. Katika masuala ya uchumi wa nchi, lazima tufanye
tofauti baina ya kujitajirisha wachache na kuleta manufaa ya watu wengi.
Sasa, sera hii itazaa mamilionea sasa hivi na sio baadaye, lakini
watakuwa mamilionea watano. Hata hivyo, wakati huo huo, pia itazaa
masikini na Tanzania itakuwa na masikini wengi sana .
Sasa
nataka niseme kuwa nimetumia Kiwanda cha Sigara kama mfano tu kuonyesha
kwamba nchi haiwezi kuendelea hata kidogo kwa kupuuza viwanda. Sasa
tunafunga viwanda. Sijui hiyo inaitwa sera ya kuondoa ama kuzuia
viwanda, lakini haya ni matatizo ambayo tunayo na usifikiri ni Tanzania
peke yake. Nilikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kusini. Nimepita pita Afrika,
Asia na Amerika ya Kusini. Nimeshuhudia mawazo na mipango ya aina hiyo
kuwa ndiyo inayoongoza na kutawala. Hilo ndilo nililowambia hivi punde
kwamba, wakati Waingereza wanatawala India , waliwaambia Wahindi. “Hapana kutengeneza nguo.”
Hali
hiyo inaendelea na wala haijabadilika mpaka leo kwani bado duniani
tunaona nchi zenye viwanda huvibana vi-nchi vidogo viache mambo ya
viwanda. Sasa taabu yetu, wala si Tanzania peke yake kuna vi-nchi vingi,
ni kwamba viongozi wetu hawakatai. Wanakubali tu. Lakini sisi ni
madodoki? Dodoki ulitumbukize katika maji, hata yenye takataka, linazoa
tu!
Kusema
kweli, duniani watu wanafikiri kwamba labda sisi ni masikini. Lakini
umasikini mbaya kulio wote ni umasikini wa mawazo. Ni mbaya sana .
Duniani kuna kujitegemea na kutegemea. Unaweza kutegemea, lakini
kutegemea kokote ni kubaya sana . Kwa hali yo yote ile, kutegemea kubaya
kupita kote kabisa ni kutegemea mtu mwingine kwa mawazo. Ni kwa ovyo
sana kunakunyima utu wako.
Watu
tunaafikiana na wazo. Lakini mawazo ambayo wazi wazi ni ya kijinga
lazima tuyakatae. Kwa sababu mtu mwenye akili akikupa mawazo ya
kipumbavu, usipoyakataa, atakudharau. Narudia, mtu yeyote mwenye akili
akikupa mawazo ya kipumbavu na wewe una akili na unajua ni ya kipumbavu
na ukayakubali, atakudharau. Sasa hatuwezi tukakubali mambo ya kipumbavu
Tanzania .
Itaendelea
SOURCE: JAMUHURI MEDIA |