Sunday, 15 September 2013

KATIBA MPYA ITAKIMUDU KIZAZI CHA ‘FACEBOOK


Imeandikwa na Albert Sanga, Iringa   
Ijumaa, Mei 04, 2012 07:32
“Nasema Katiba ya kweli ya Watanzania inapaswa kuandikwa katika mioyo na utashi wao, na wala si ya kuandikwa kama hii tunayoililia sasa”.

Hayo si maneno yangu ya Manyerere Jackton aliyoyaandika kupitia gazeti hili katika makala yake iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Nitakuwa wa mwisho kuishabikia Katiba mpya’.


Nimeisoma makala ya Manyerere na kuirudia zaidi ya mara nne nikisoma aya kwa aya, mstari kwa mstari. Ningeweza kuielezea kwa upana lakini niseme tu kwa kifupi ‘ilinikuna mno’.

Manyerere ameibua mjadala ambao nina uhakika wengi wamepatwa na upofu kuuona na ni hatari katika ustawi wa nchi hii kwa siku zijazo.

Kuna matumaini ‘mengi hewa’ yaliyojengwa akilini mwa Watanzania wengi, kwa ujio wa katiba mpya. Vijana wengi ambao kwa sasa wamefunga ‘ndoa’ na mitandao ya kijamii kama ‘facebook’, ‘twitter’ na mingine wameaminishwa na wanaendelea kuaminishana kuwa suluhu ya matatizo na changamoto zao binafsi inapatikana katika mambo mawili - katiba mpya na wanasiasa wapya.

Aina ya siasa zinazoendelea sasa Tanzania naweza kuziita kuwa ni ‘momentum politics’. Ni siasa zinazokwenda zikikusanya watu wa upande mmoja kwenda mwingine, kutukanana, kuchafuana na hata kuhujumiana pasipo kujali mwelekeo wa Watanzania wenyewe.

Kadiri siasa hizi zinavyopata ‘spidi’ kubwa ndivyo zinavyozidi kusomba wengi na kadiri wengi wanavyozidi kusombwa ndivyo zinavyozidi kupata ‘momentum’ kubwa. Kwa kuwa ‘momentum politics’ zinatafuta umaarufu utakaohanikiza utwaaji wa madaraka kwa mbinu yoyote, fikra za wananchi na ustawi wao unakosa mwelekeo.

Mchambuzi Manyerere ameendelea kusugua kichwa (na bado hajapata majibu) namna Katiba mpya itakavyowadhibiti wezi, mafisadi, wavivu na wazembe. Hata mimi ninaafiki kuwa nchi hii ina katiba na sheria nzuri sana; tunapoililia katiba mpya nadhani tunakuwa hatujaelewa tatizo letu.

Vile vile mjadala wa katiba mpya tumeshauingizia mdudu kwa kutanguliza maslahi na hisia za vyama vya kisiasa. Watu wanasahau kuwa taifa hili linatakiwa kujengwa kwa misingi halisi itakayodumu; wala si misingi itakayofanikisha chama ama watu fulani kuingia madarakani katika kipindi fulani.

Midomoni na akilini mwa Watanzania wengi kwa sasa kumejaa siasa. Hakuna kinachoonekana zaidi isipokuwa siasa. Maswali mengi yanajibu lile lile moja - siasa! Hebu angalia maswali yafuatayo na majibu yake kwenye mabano. Kitendo cha kuhusisha siasa katika kila kitu ndicho ninachokiita, ‘ku-politicalize’.

Kwa nini wewe kaya yako imekumbwa na njaa wakati una mashamba yanayofaa kilimo cha kumwagilia? (Kwa sababu mawaziri wanaiba fedha serikalini). Kwa nini wewe umeshindwa kudumisha upendo katika ndoa yako? (Kwa sababu ya mfumko wa bei).

Wewe kiongozi wa dini unayefundisha neno la Mungu, kwa nini sasa unaiba wake za waumini wako? (Polisi nchi hii wanakula sana rushwa na wameshindwa kazi, kwa sababu mimi nilipokamatwa ugoni niliwapigia waje kuniokoa lakini wakachelewa hadi nimeaibika).

Inakuwaje watu wawe wanashinda wakilalamika na wakati huo huo wakiwa wavivu wa kutekeleza wajibu wao? (Tumewaambia mawaziri wajiuzulu lakini hawataki, kweli wanatukatisha tamaa, hapa tupo kijiweni tunajadili hilo!).

Kwa nini wengine wanaendelea kutajirika na wengine wanazidi kuwa masikini (kwa sababu ya wawekezaji). Inakuwaje mwanafunzi aliyepewa fedha na serikali ama mzazi lakini badala ya kusoma anaendekeza starehe na ulevi na baadaye kufeli? (Baraza la Mitihani ni waonevu sana, yule katibu inabidi ajiuzulu haraka).

Orodha ya maswali inaendelea na ni ndefu mno, lakini linatolewa jibu moja jepesi (Serikali iliyopo madarakani imeshindwa).

Suala la maisha na siasa ni kama lile fumbo la yai na kuku. Kipi kinaanza kati ya siasa na maisha. Ni siasa ndiyo inayozaa maisha ama ni maisha ndiyo yanayozaa siasa? Kipi ni mzazi wa kingine?

Katika maswali kadhaa hapo juu nimetoa swali kuhusu mtu kushindwa kudumisha upendo katika ndoa yake. Ukiamua ‘ku-lipoliticalize’ suala hilo utasema uchumi mbaya na ugumu wa maisha unaleta kutoelewana ndani ya ndoa.

Lakini inakuwaje kwa wale walio na maisha mazuri na bado ndoa zinawasumbua? Je, nao watasema ni kushindwa kwa siasa? Tuache hilo, tumuangalie huyu kiongozi wa dini anayeiba wake za waumini wake. Huyu naye atatuambia ni kutokana na sababu za kisiasa ndiyo maana anafanya hivyo?

Ninachokiona mimi ni kuwa jamii ya Kitanzania imepotoshwa mno na inaendelea kupotoshwa na hili dude liitwalo siasa. Siasa zimechukua nafasi ya uwajibikaji na sasa wengi wanaona ukombozi upo katika siasa.

Unapomuuliza mtu kwa nini anafanya uzembe kazini  halafu anakujibu (kwa sababu ya katiba mbovu), basi bila shaka unatambua moja kwa moja kuwa tupo katika hali mbaya ya kifikra na kimtazamo.

Wanasiasa wametudanyanya na kutupoteza kwa ajili ya maslahi yao na wafuasi wao. Kwa ushirikiano na baadhi ya vyombo ‘uchwara’ vya habari, wanaelekea kushinda makakati wao wa kugeuza akili za Watanzania kuwa za kiutumwa.

Kama alivyoniambia rafiki yangu mmoja, “sasa wanatu-localize bila falsafa na tunaendelea kuamini kuwa ukombozi wetu umo mikononi mwao.” Tunapotea!

Propaganda na blaa blaa zitapita lakini uhalisia utadumu daima. Chama tawala wakati mwingi hakiweki peupe ukweli wote na wakati huo huo vyama vya upinzani vinawaghilibu wananchi. Wakati chama tawala kupitia viongozi wake na watendaji serikalini wanawaambia wananchi kuwa wanafanya kila juhudi kuwaokoa kimaisha, vyama vya upinzani vinahubiri kuwa wokovu unaonenwa na CCM umeshahamia kwao, hivyo wapewe nafasi. Hakuna anayewapa ukweli wananchi kuwa ‘wawajibike!’

Kwa mfano, katika sayansi ya uchumi wa mataifa wapo wadau watatu wanaotajwa kuratibu ukuaji ama udororaji wa uchumi (major economic players). Hawa ni mtu mmoja mmoja (households), biashara, taasisi na kampuni (firms) na mwisho ni serikali (government). Katika mfumo wa kijamaa serikali inakuwa ndiyo mhimili wa uchumi kwa maana kuwa ukuaji na mdororo wa uchumi unaweza kukamilishwa kwa sehemu kubwa na serikali pekee.

Katika mfumo wa kibepari (ambao Tanzania tunaogelea kwa kasi), serikali inabaki kama msimamizi wa sheria zinazotawala mchezo wa uchumi (regulating and monitoring).

Mtu yeyote anayefahamu uchumi vizuri atakubaliana nami kuwa hali mbaya ya uchumi wa Tanzania (chini ya ule wastani ulioletwa na mabadiliko ya kidunia), imechangiwa kwa sehemu kubwa na kushindwa kwa mtu mmoja mmoja. Nashangaa kuwa wanasiasa wanajifanya kuwa hawalioni hili, wanaingiza siasa kwa mambo hata yanayoweza kumalizwa kitaalamu.

Ni kweli kuwa siasa ina nafasi katika kuandaa mazingira ya uchumi wa kitaifa, lakini kukwamuka kiuchumi katika ngazi ya mtu mmoja mmoja kunategemea juhudi za mtu binafsi. Wanasiasa hawataki kuwaeleza ukweli mchungu Watanzania ya kwamba wafanye kazi kwa bidii.

Sijawahi hata siku moja kuwasikia viongozi wa vyama vya upinzani wakisema angalau sentensi ifuatayo; “Watanzania wengi mna maisha magumu lakini sehemu ya ugumu huo wa maisha yenu umetokana na kasumba ya kutofanya kazi kwa bidii”.

Pamoja na kuwa wanasiasa wanafahamu kuwa umasikini wa Watanzania unatokana na uvivu wetu wa kuwajibika na kukosa ubunifu hata kwa rasilimali tulizojaliwa, lakini hawasemi hili.

Wanaona kuwa wakisema hili watu watafumbuka na kubaini kuwa kumbe siasa ni msaidizi tu na si ‘mungu pekee’ wa maendeleo. Huenda ni hofu ya kukosa watu kwenye maandamano ama katika foleni za kuwapigia kura ili wapate ‘kula’ (wao wanajua!)

Kuna mtu anakumbwa na baa la njaa kwa sababu alilima na mvua hazikunyesha, lakini kuna ambaye anakumbwa na baa la njaa kwa sababu hakulima licha ya kuwa na ardhi na mvua za kutosha.

Kuna tatizo la askari wa barabarani kupokea rushwa kwa sababu magari ni mabovu, lakini kuna watu wanaagiza ama kununua magari mabovu bila hofu kwa sababu wamekusudia kuendelea kutoa rushwa.

Ni watu hawa hawa wavivu wa kulima wanataka katiba mpya ili kuwe na neema ya chakula! Ni hawa hawa watoa rushwa wakubwa barabarani ambao nao wamo katika kulilia katiba mpya!

Tumekuwa watu wa ajabu na hatujielewi kuwa tunapotea. Katiba mpya inahitajika sana sana, lakini katiba mpya haitaingia majumbani kuwasaidia watu waivishe vyakula, katiba mpya haitawafulia watu nguo. Katiba mpya haitazuia mtu kuwa na vimada nje ya ndoa.

Nimetoa mifano midogo lakini katika ngazi mbalimbali kuna mambo yanayotokana na watu kutowajibika, halafu lawama zinahamia kwa siasa. Zinyoosheni vidole siasa lakini tusisahau kuhimizama kuwajibika.

Mimi ni mwanamapinduzi halisi na ninatamani kuona taifa hili likipata mabadiliko makubwa ya kisiasa - ikibidi hata kuking’oa chama tawala madarakani. Na tulipofikia ninaona kuwa ni pazuri kwa sababu miaka ya CCM kukaa madarakani inaelekea mwishoni.

Lakini ninawatahadharisha wote wanaojiandaa kuiondoa CCM wawe makini. Mbinu wanazotumia kuandaa fikra za Watanzania ili wawachague (ama wawasaidie kuendesha mapinduzi kwa maandamano) zitakuja kuwagharimu.

Ukweli ni kwamba hakuna serikali yoyote duniani inayomfanyia mwananchi kila kitu, lakini fikra za Watanzania kwa sasa zinaamini kuwa CCM ikiondoka madarakani wanaokuja watawaingiza katika nchi ya ahadi.

Katiba inaweza kubadilika lakini tutafanyaje kuwabadilisha wale waliozoea kushinda vijiweni wakicheza bao na huku wanalalamika kuwa maisha ni magumu?

CCM itaondoka madarakani lakini utamaduni wa watu kukosa maadili tutauondoaje? Kwa vyovyote vile mimi si mwanaharakati wa kisiasa (nina falsafa ya kutoruhusu siasa kuamua hatima ya maisha yangu) lakini ninawashauri wanasiasa na Watanzania wote kuacha kuwa kama makinda ya ndege, kwa hulka ya kupanua midomo na kusubiri siasa iwaletee kila kitu.

Ninaona kiini cha kukwama kwa taifa hili tunakipita pembeni; hili linanipa shaka kuhusu ‘jeuri’ ya Katiba mpya kukimudu kizazi cha ‘Facebook’.

stepwiseexpert@gmail.com  0719 127 901
SOURCE: JAMUHURI MEDIA