Wiki iliyopita Jaji Kiongozi, Fakihi Jundu, ametoa taarifa ndefu kwa vyombo vya habari akilishambulia Gazeti la JAMHURI. Mashambulizi ya Jaji Kiongozi yalijielekeza katika msingi kwamba JAMHURI imekuwa ikifuatilia kazi za Mahakama, tena si kwa uzuri bali kwa kutafuta mabaya yanayofanywa ndani ya Idara hiyo.
Kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, katika mkutano huo, Jaji Kiongozi Jundu alifikia hatua akasema: “Tumechoka na habari zao [JAMHURI].” Hakufafanua alimaanisha nini kwa kauli hii ya “TUMECHOKA” au iwapo sasa ametangaza rasmi vita kati ya Mahakama na JAMHURI.
Kilichomsukuma
Jaji Jundu kutoa kauli hiyo na taarifa ndefu yenye kurasa 15, ni habari
tuliyoichapisha toleo Na 98 la Agosti 27- Septemba 2, 2013. Habari hii
ilikuwa na kichwa cha habari kisemacho “Majaji wanaolinda wauza ‘unga’
wabainika.” Tumeichapisha taarifa yote ya Jaji Jundu katika toleo la
leo, na kurudia habari aliyoilalamikia neno kwa neno ili msomaji aweze
kupima mwenyewe.
Kati
ya kesi zilizolalamikiwa ni kesi Na 47 ya mwaka 2011 ambapo mshitakiwa
William Chonde na wenzake watatu walipewa dhamana baada ya kukutwa na
kilo 179 za dawa za kulevya aina ya heroin. Dhamana hii ilitolewa na
Jaji Upendo Msuya kwa kutumia Kifungu cha 148 (5) cha Sheria ya Mwenendo
wa Mashitaka (CPA) na Kifungu cha 27 (1) (b) cha Sheria Na 9 ya Kuzuia
Dawa za Kulevya ya mwaka 1995.
Vifungu
hivi vinamtaka mtu aliyetuhumiwa kukutwa na dawa za kulevya, tuhuma
hizo ziambatanishwe na hati ya kiapo kutoka kwa Kamishna wa Tume ya Dawa
za Kulevya ikithibitisha thamani ya dawa hizo na ikiwa thamani ni zaidi
ya Sh milioni 10, ndipo dhamana ifungwe.
Hata hivyo, sehemu ya (a) inaorodhesha aina ya dawa ambazo akikutwa nazo mtu, basi dhamana inafungwa moja kwa moja. Heroin
imo. Kwa mantiki hiyo, kuna uchochoro katika sheria husika. Ni kutokana
na mtanziko huu, Jaji Kipenka Mussa aliamua kupingana na Jaji Msuya kwa
maneno ya wazi, ambapo hata Jaji Jundu amesema Oktoba hii Mahakama ya
Rufaa itatolea uamuzi ni hukumu ipi itaendelea kusimama (precedence) kati ya ile ya Jaji Msuya na Jaji Mussa.
Wakati
Jaji Msuya akitoa hukumu ya aina hiyo na kuwapa dhamana watuhumiwa
waliokuwa na dawa zenye thamani zaidi ya Sh bilioni tano, Jaji mwenzake
Mussa alipingana wazi na Jaji Msuya katika kesi dhidi ya Ramadhani
Athumani Mohamed, Ally Mohamed Abdallah, Issa Abdallahman Soud na Rashid
Mohamed Flashman, iliyotolewa Septemba 9, 2011.
Watuhumiwa hawa ambao wako rumande hadi sasa kwa amri ya Jaji Mussa, walikutwa na kilo tatu za cocaine
zenye thamani ya Sh milioni 202,500,000. Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga
ilikuwa imewapatia dhamana kwa kutumia kigezo cha hukumu iliyotolewa na
Jaji Msuya awali kwa mazingira yale yale kuwa washitakiwa
walipofikishwa mahakamani, dawa walizokamatwa nazo hazikuwa na hati ya
kuthibitisha thamani ya dawa hizo kutoka kwa Kamishna wa Tume ya Dawa za
Kulevya nchini. Zipo hukumu nyingine kama mbili zinazogongana ikiwamo
ya Jaji Kaduli na Jaji Fauz.
Akitoa
hukumu yake mjini Tanga, Jaji Mussa alisema kwa masikitiko analazimika
kupingana na hukumu ya Jaji mwenzake Msuya, ambayo ilitafsiri sheria
bila kuangalia nia ya wabunge wakati wanatunga sheria hiyo. Alisema pia
kwa mazingira ya watuhumiwa kutakiwa kufikishwa mahakamani ndani ya saa
24, na ukubwa wa Tanzania kusema kuwa ndani ya muda huo Kamishna awe
ametoa hati ya thamani ya dawa za kulevya nchi nzima ni kujidanganya.
Jaji
Mussa alisema nia ya msingi ilikuwa ni kutoa adhabu kali itakayozuia
watu kufanya biashara ya dawa za kulevya zenye madhara makubwa kwa Taifa
na kizazi chote kwa ujumla, hivyo akafunga dhamana ya watuhumiwa na
kuagiza sheria hiyo irekebishwe kufuta kifungu cha kutaka hati ya
thamani kutolewa, kwani kinasaidia wahalifu kuendelea kufanya biashara
hii.
Sitazungumzia
madai ya majaji vihiyo, ambayo Jaji Jundu kwenye taarifa yake kwa
vyombo vya habari aliigusia, lakini nimkumbushe tu kuwa kati ya majaji
hao, alikuwamo aliyekuwa hana shahada ya sheria kama lilivyo hitaji la
msingi kwa mtu kuteuliwa kuwa Jaji, na wakati tunaiandika habari hiyo
Jaji husika alikuwa anasoma sheria katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Kama Jaji Jundu anabisha hili, anyooshe kidole juu.
Sitanii,
niseme mapema tu kuwa kati ya aliyosema Jaji Jundu upo ukweli
usiopingika, lakini nimepata shaka na kulazimika kuandika makala haya,
baada ya kuona hatari ya kauli ya Jaji huyu kutaka kutumia umbumbumbu wa
Watanzania katika sekta ya sheria kuua uhuru wa kutoa mawazo.
Nakubaliana
na Jaji Jundu kuwa Ibara ya 107A, ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania (1977) inaweka mikononi mwa Mahakama kazi ya kutafsiri sheria.
Nasema ni kweli kabisa. Hata hivyo, nimkumbushe kuwa Mahakama haitafsiri
sheria kwa busara bali kwa kutumia misingi, kanuni na sheria za nchi
zinazotoa mwongozo wa kufanya tafsiri husika.
Ni
katika hatua hii, nalazimika kutumia Ibara ya 18 ya Katiba inayompatia
mwananchi uhuru wa kutoa mawazo yake katika jambo lolote bila kujali
mipaka ya nchi. Kwamba mazingira anayotaka kujenga Jaji Jundu ni kwamba
Mahakama ikosee, ipatie; wananchi hawana haki ya kujadili au kutolea
maoni uamuzi au mwenendo wa kesi zilizoamriwa na Mahakama. Nasema
hapana. Katiba inaruhusu hili.
Anajaribu
kujenga hoja kuwa vyombo vya habari havipaswi kujadili kesi zilizoko
mahakamani. Nasema hapa Jaji ameteleza. Nizungumze hili kwanza kabla ya
kurejea kwenye tafsiri ya sheria. Vyombo vya habari visichoruhusiwa
kufanya ni kutolea kauli zenye kuhukumu mtu au taasisi iliyopo
mahakamani sawa na mfano alioutoa Dk. Masumbuko Lamwai.
Hata
hivyo, vyombo vya habari havizuiliwi kueleza historia ya mtuhumiwa.
Kwamba kama mtu aliwahi kuiba mara nne na kufungwa jela mara tatu,
mwandishi anaisaidia Mahakama kwa kuikumbusha kuwa mtuhumiwa aliyepo
mbele yake ni mzoefu katika kutenda makosa, ingawa havipaswi kumhukumu
kuhusiana na kosa la wakati huo. Katika hili rejea kesi ya mwanariadha
Oscar Pistorius wa Afrika Kusini, anayekabiliwa na kesi ya kuua mpenzi
wake!
Hicho kinachoitwa kudharau Mahakama au kuingilia mwenendo wa kesi (subjudice)
hakitokei kwa kuwaeleza watu kilichotokea katika Mahakama ya wazi.
Kwamba Jaji Msuya ametoa dhamana na Jaji Mussa amekataa kutoa dhamana
kwenye Mahakama ya wazi kuliripoti si kuingilia mwenendo wa kesi.
Kwa
kutumia Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
wananchi wakipokwa uhuru wa kujadili, kutolea maoni au kupinga uamuzi
uliotolewa na Mahakama, Bunge au Serikali, basi tutairejesha nchi hii
katika enzi za UKOLONI, ambapo tutakuwa na watawala au watendaji
miungu-watu wanaojua kuwa wanaweza kufanya lolote wasihojiwe wala
wasiguswe.
Sitanii, majaji au mahakimu si binadamu maalum (super human beings)
katika jamii tuishiyo. Kama ni shule za sheria, tunaingia darasa moja,
ila mbele ya safari tunagawanyika, hawa wanakuwa mawakili, hawa
mahakimu, waendesha mashitaka na hatimaye majaji na wengine wanaendelea
kufanya kazi nyingine. Kwa hiyo, sheria inayotumika mahakamani Jaji
Jundu anapaswa kufahamu kuwa wapo wengine wasiokuwa mahakimu au majaji
wenye kuifahamu sawia na wao (majaji) wenye madaraka haya ya kidola.
Ni kwa mantiki hiyo, Gazeti JAMHURI
limepinga uamuzi wa Jaji Msuya kutoa dhamana kwa Chonde. Kama
nilivyosema hapo awali, zipo njia tatu za kisheria za kutafsiri sheria.
Jaji anaruhusiwa kutafsiri sheria kwa kufuata maana inayooneshwa na
maneno yaliyoandikwa katika sheria (literal rule)
kama njia ya kwanza. Akiona utata, anaruhusiwa kuipitia kwa kina sheria
husika kuangalia maana iliyojificha (golden rule), na ikiwa hili
limeshindikana anapaswa kuangalia watunga sheria (Bunge) walimaanisha
nini katika kutunga sheria hii (mischief rule).
Inawezekana
mimi na Jaji Jundu, huyu mzee wangu ninayemheshimu sana tumetofautiana
kiwango cha uelewa, na huu ndiyo ukweli wenyewe kwamba yeye ni Jaji na
mimi ni Mwandishi wa Habari, kwamba busara ya kawaida tu inatutaka
tujiulize kwa nini Jaji Mussa aliwanyima dhamana watu wenye kilo tatu za
cocaine, lakini Jaji Msuya akawapa dhamana watu wenye kilo 179 za heroin. Wawili kati ya waliopewa dhamana ambao ni Wapakistani wamekwishaikimbia nchi.
Hapa
sina mamlaka ya kuielekeza Mahakama, kwani mikono yangu imefungwa -
siruhusiwi kufanya hilo, ila najaribu kuwaza kwa sauti tu, kuwa hapa
Jaji Jundu kweli anaona Gazeti JAMHURI limeikosea adabu Mahakama kwa kueleza ukweli huu uliotolewa kwenye Mahakama za wazi?
Sitanii, jingine ni hili analosema Gazeti JAMHURI
halikuwapa fursa Mahakama kuhojiwa juu ya hukumu hizi. Nadhani hapa
Jaji Jundu amesahau tu, na naomba nimkumbushe kiungwana kuwa hukumu
ikishatolewa inakuwa nyaraka iliyo wazi kuonwa na jamii (public document).
Huwezi kusema Waziri atoe hotuba yake bungeni, au Rais atoe hotuba
kupitia vyombo vya habari, kisha umtafute kumhoji juu ya hotuba hiyo.
Tunachofanya katika tasnia ya habari ni kuchambua nyaraka hizo, iwapo
zimetimiza kigezo cha kisheria na matarajio ya jamii au la. Kimsingi
katika hili, ameteleza tu, hakukuwapo sababu ya kuwaona.
Naamini
Jaji Jundu anafuatilia yaliyotokea kwenye Mahakama ya Kenya. Kati ya
majaji 18 wa Rufani, walipofanyiwa usaili kati yao ni majaji watatu tu
waliopita bila mawaa. Majaji ni sehemu ya jamii tuishimo. Sisi
tunapomulika utendaji wake, si kwamba tuna lengo la kuwaaibisha au
kushusha heshima ya Mahakama, bali tunawajenga zaidi na zaidi kuepusha
wasifanye makosa kama hayo siku za usoni.
Sitanii,
nikiri wazi kwamba Mahakama na hasa Mahakama Kuu wananchi wengi tuna
imani kuwa ndicho chombo pekee kinachotoa haki bila kujali mwelekeo wa
kisiasa. Ndiyo maana tumeshuhudia mara kadhaa wapinzani wakishinda kesi
dhidi ya chama tawala na kinyume chake. Siamini kama siasa zipo kwenye
chombo hiki, hiki ni chombo safi ambacho tukiona kinanyemelewa na mzimu
wa kupotoka inatupasa kununua sabuni tukakisafisha haraka mno kabla
hakijapata doa.
Nihitimishe
makala haya kwa kusema Mahakama isituchoke. Namshukuru Jaji Jundu kwa
kufungua milango, lakini waifungue kweli. Amuulize Afisa Mtendaji Mkuu
Hussein Katanga nilipouliza suala hili alinijibu nini. Narudia, JAMHURI
tunapoimulika Mahakama tunaijenga, hatuibomoi. Nimefurahi kusikia kuwa
Oktoba hii, sheria hizi mbili CPA na Na 9 ya Dawa za Kulevya (1995)
zitapitiwa na kutoa msimano wa hukumu ipi ibaki kuwa halali.
Asante Jaji Jundu. Mungu ibariki Tanzania. Kwa pamoja tutaijenga nchi yetu.
SOURCE: JAMUHRI MEDIA
|