>>Gazeti hili sasa limeamua kuwataja kwa majina >>Mahakimu nao wanawaachia mapapa kienyeji >>Kigogo ofisi ya DPP, Mahakama Temeke, Kinondoni ni balaa
Mahakama
kupitia baadhi ya majaji na mahakimu wasio waadilifu imebainika kuwa
kikwazo kikubwa katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini, uchunguzi
wa JAMHURI umebaini.Pamoja na Mahakama, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa
Serikali (DPP), nayo imelaumiwa kwa kufuta kesi katika mazingira ambayo
hata mtu ambaye hakusoma sheria, anaweza kuyatilia shaka.
Wakati
vyombo hivi vikikwamisha vita hii, lawama zimekuwa zikielekezwa kwa
polisi na vyombo vingine vya usalama, ambavyo watendaji kazi wake
wanafanya kazi usiku na mchana.
Juhudi zote zinazofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama zinagonga mwamba mahakamani kwa msaada wa ofisi hiyo ya DPP.
Wakati
kesi nyingine zikifutwa, nyingine hazisikilizwi, kiasi cha kusababisha
zirundikane mahakamani tangu mwaka 2005. Kesi chache zinazohusu
watuhumiwa wakubwa wa kuuza ‘unga’ zinamalizwa haraka kwa utaratibu wa
ofisi ya DPP kuwasilisha nia ya kutoendelea na mashtaka mahakamani
(nolle prosequi) au wasimamizi hao wa utoaji haki kutoa hukumu
zinazoacha wengi vinywa wazi na kuwakatisha tamaa polisi.
Katika
hali ya kushangaza, majaji na mahakimu wamekuwa wakikiuka wazi Sheria ya
Kuzuia Dawa za Kulevya Na, 9 ya Mwaka 1995 inayozuia mtu yeyote
aliyekamatwa na dawa zenye thamani kuanzia Sh milioni 10 asipewe
dhamana, lakini hilo halizingatiwi. JAMHURI haikubahatika kufahamu
bayana nini kinawapofusha majaji na mahakimu wakati ‘mapapa’
wanapofikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuuza unga, lakini ni wazi kuwa
kuna mtandao mkubwa wa kulindwa kwa watuhumiwa hao wenye ukwasi mkubwa.
Wakati
polisi wanafanya kazi ya hatari usiku muda wote, wakipambana na wauaji,
wahongaji na watu wanaouza dawa za kulevya, kesi za mapapa zinamalizwa
kienyeji mahakamani.
Moja ya kesi inayotia shaka ni Na. 47 ya
Mwaka 2011. Kesi hii ilifunguliwa dhidi ya watuhumiwa Fredy William
Chonde, Kambi Zuberi Seif; ambao ni Watanzania na Abdulghan Peer Bux na
Shaaban Malik ambao ni raia wa Pakistani.
Hawa walikamatwa eneo
la Mbezi Beach, Dar es Salaam wakiwa na kilo 175 za heroin, ambako kesi
dhidi yao ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini
humo. Wakati kesi inaendelea Kisutu, mawakili wa vigogo hawa walikwenda
Mahakama Kuu wakafungua shauri la kuomba wapewe dhamana chini ya Jaji
Pendo Msuya, wakitambua kuwa sheria inazuia.
Bila kuchukua jalada
wala kuwasiliana na Mahakama ya Kisutu, huku Jaji Msuya akijua fika
kuwa kilo 175 ambazo thamani yake ni zaidi ya Sh bilioni tano, na
watuhumiwa hawapaswi kupewa dhamana; yeye kwa mamlaka aliyonayo kama
Jaji aliamua kuwapa dhamana watuhumiwa hawa. Baada ya kupata dhamana,
Wapakistani walirejeshewa pasipoti zao na wakakimbia nchi. Hawajakamatwa
hadi leo.
“Cha kusikitisha kesi iliendelea bila kujua kuwa
watuhumiwa wamekwishapewa dhamana na hadi Aprili 8, mwaka huu 2013 kesi
hiyo ilitajwa… baadaye Mahakama ikapewa taarifa kuwa watuhumiwa
walishapewa dhamana na Mahakama Kuu ndiyo maana hawaonekani mahakamani.
Tulishangaa sana,” kilisema chanzo chetu kutoka Mahakama ya Kisutu.
Kesi
nyingine iliyomalizwa kienyeji ni ya Mwinyi Rashid Mkoko. Vyanzo vya
JAMHURI vinaonesha kuwa huyu na familia karibu yote wanatuhumiwa kufanya
biashara ya dawa za kulevya. Ndugu zake waliokamatwa kwa nyakati
tofauti na baba yao, ambako mmoja alidhulumiana, na ‘mzigo’ na wauza
unga, hali iliyofanya wamuue kwa kumpiga risasi.
Katika familia
hii, Rashid Ismail Mkoko ndiye aliyeuawa na wauza unga wenzake eneo la
Ilala, Dar es Salaam. Huyu alipata kukamatwa kuhusiana na dawa za
kulevya, ila pia kwa kosa la mauaji. Shuhuda wa tukio la Rashid Ismail
Mkoko anasimulia kama ifuatavyo:
“Huyu ndiye wa kesi ile ambayo
kijana aliyemtuma mzigo Pakistan pipi zilipasukia tumboni akafia gesti
kule Tabata, Dar es Salaam. Mmoja wa ndugu wa kijana huyu aliyefariki,
alimpigia simu akamwambia ‘si unajua alikuwa na mzigo wako ndiyo
umemuua? Sasa mbona umetususa? Hata maji ya kunywa hutupatii msibani?’
“Mkoko
akamwambia nitakuja jioni. Na kweli jioni iliyofuata akampigia simu
kuwa anakwenda hapo nyumbani msibani. Alipofika akampigia simu,
akamwambia njoo tuonane. Huyu ndugu wa kijana aliyefariki akatoka nje,
akaenda kwenye gari kuonana na Mkoko.
“Alipofika Mkoko akamuuliza
ndiye wewe uliyenipigia simu jana, yule ndugu wa marehemu akajibu
‘ndiyo’, basi Mkoko alichofanya akatoa bastola akampiga risasi ya usoni
yule kijana…akafariki papo hapo, Mkoko akaondoka.
“Polisi
walimkamata wakamfikisha mahakamani. Mahakama ikamwachia kwa mizengwe.
Ila Mungu si Athumani, ikatokea naye akadhulumu wauza unga wenzake huko
Ilala, nao wakamuwinda wakampiga risasi akafa mwaka juzi.
“Huyu
alikuwa muuza dawa za kulevya mkubwa. Mdogo wake Mwinyi Rashid Mkoko,
naye anauza dawa. Tulimkamata na heroin gramu 250 zenye thamani ya Sh
milioni 11, ikafunguliwa kesi Temeke Na. PI 26 chini ya Hakimu Mkwawa,
lakini ajabu wakati kesi inaendelea kutajwa Temeke hadi leo, huyu Mwinyi
Mahakama Kuu imekwishamwachia huru bila vielelezo vyovyote,” kilisema
chanzo chetu kutoka mahakamani.
Uchunguzi wa JAMHURI umeonesha
kuwa awali mawakili wa Mwinyi waliwasilisha ombi la dhamana kwa Jaji
Munisi, ambaye aliwaelekeza mawakili wa Serikali kuwa badala ya
kumshtaki Mwinyi kwa kukutwa na dawa za kulevya, waiondoe kesi
mahakamani na kuifungua upya kama kesi ya kusafirisha dawa za kulevya.
Kwa kawaida tuhuma za aina hiyo huwa hazina dhamana.
Mawakili
walivyopata mwanya huo, wanajua jinsi walivyozungumza na wanasheria wa
Serikali. Kesi hiyo badala ya kuiondoa kama alivyoelekeza Jaji Munisi
wakaihamishia kwa Jaji Dk. Fauz Twalib, ambaye katika hukumu yake ya
Julai 30, 2012 alikiri kuwa mbele yake halikufikishwa jalada la kesi
hiyo na wala hakuwa na mamlaka ya kuisikiliza kwani yeye si hakimu, ila
akasema kwa kuwa Mahakama ya Temeke haina mamlaka ya kusikiliza kezi za
dawa za kulevya kama cocaine, basi akatoa fursa ya kumsikiliza
mtuhumiwa.
“Kwa kasi ya aina yake, siku hiyo hiyo ya Julai 30,
2012 baada ya Jaji Dk. Fauz kutoa hukumu hiyo ya ajabu, mawakili wa
Serikali ambao ni upande wa mashitaka wakawasilisha nolle chini ya
Section 91 ya CPA (Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka), hivyo Mwanasheria
wa Serikali Mpembo kwa niaba ya DPP akawasilisha hati hiyo, na Jaji Fauz
akaifuta kesi dhidi ya Mwinyi.
“Kisichoeleweka na kufahamika ni
nini kilitokea na nini kiliendelea siku hiyo hiyo kutoa hukumu, na siku
hiyo hiyo Mpembo akawasilisha nolle na kesi ikafutwa siku hiyo hiyo.
Hapa kuna maswali mengi. Mwinyi amekimbilia Zanzibar. Yupo anaponda
raha, kesi bado ipo Temeke na hakuna kinachoendelea,” kimesema chanzo
chetu.
Baba yao Mwinyi na Rashid, naye kwa nyakati tofauti
anadaiwa kukamatwa na polisi akituhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa
za kulevya. Mtoto wake mwingine, Abubakar Mkoko, yeye alitolewa dawa za
kulevya tumboni, lakini Mahakama ikampiga faini ya Sh milioni 1 na
kumwachia huru.
Kesi nyingine inayowakosesha usingizi polisi ni
ile ya Dhoulkefly Awadh Abdallah Na. 238 ya Mwaka 2010. Kesi hii
ilimhusisha Abdallah na mkewe Asha Seif Kiluvya. Asha ndiye aliyekamatwa
na dawa za kulevya. Hata hivyo, katika mazingira ya kutatanisha, ofisi
ya DPP ilipeleka nolle prosequi mahakamani Asha akaachiwa huru, na sasa
anashitakiwa Abdallah ambaye hakukutwa na kitu chochote.
Kioja
kinginge kilifanywa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kinondoni anayetajwa
kwa jina la Msongo. Kesi hii ilianza mwaka 2005 na kumalizika mwaka
2008. Mshitakiwa alikuwa Yusufu Hassan Yossye, mkazi wa Kinondoni A,
Mtaa wa Togo, aliyekutwa na gramu 1,244 za heroin ambazo alikamatwa nazo
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Aliwekwa chini ya ulinzi kwa lengo la kumfanya atoe ‘pipi’ kwa njia ya
haja kubwa. Katika hukumu ambayo inatia shaka Hakimu Msongo aliandika
hivi:
“Katika ushahidi wote uliotolewa, hakuna ubishi kuwa ni
kweli amekutwa na dawa za kulevya. Pia ushahidi unaonesha kuwa
mshitakiwa alitoa madawa hayo kwa njia ya haja kubwa. Hata hivyo, upande
wa mashitaka umeshindwa kueleza ni dalili zipi zilipelekea
(zilisababisha) kushukiwa kuwa mshitakiwa ana madawa ya kulevya. Na pia
hawakushirikishwa watu au wataalamu wa afya ya binadamu.
“Upande
wa mashitaka katika ushahidi wao umeonesha walipishana kutoa idadi [ya
pipi alizotoa kwa haja kubwa]. Kutokana na hilo, ushahidi hautoshelezi
na mshitakiwa namwachia chini ya Kifungu cha 235 cha CPA (Kanuni ya
Mwenendo wa Mashitaka) katika mashitaka yote mawili.” Hukumu hii
ilitolewa na Hakimu Msongo Mei 2, 2008. Yossye alikuwa akishitakiwa kwa
kukutwa na dawa; na pia kwa kuwaambia polisi uongo kuwa hakuwa na dawa,
lakini baadaye akazitoa kwa njia ya haja kubwa.
Katika Mahakama
ya Kisutu, mwanamke mwingine aliyetambuliwa kwa jina la Pilly,
alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa na
zawadi ya kinyago ambacho ndani yake kilikutwa na dawa za kulevya,
lakini Mahakama ya Kisutu wakati inatoa taarifa ilimwachia huru Pilly
kwa maelezo kuwa wakati polisi wanamkamata, hakuwapo mwanamke, hivyo ni
kosa mhalifu mwanamke kukamatwa na polisi mwanaume. Akaachiwa huru!
Kesi
nyingine ni ya Kwaku Sarfo, raia wa Ghana, alikamatwa Uwanja wa Ndege
wa Julius Nyerere mnamo Novemba 14, 2010. Thamani ya dawa ilikuwa Sh
milioni 390. Kesi ilipelekwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Samora kwa Hakimu
Mkazi Luago.
“Tulishangaa, kwamba kwanza Mahakama hii haina
mamlaka ya kusikiliza kesi hii, lakini pia baada ya kupita siku 60; bila
mamlaka kisheria, Hakimu Luago akaifuta. Hakimu huyu ni kero.
Amehamishiwa Lindi akagoma kwenda. Hatujui anapewa jeuri na nani.
Tungeomba Rais Kikwete na mhimili wa Mahakama waingilie kati suala hili
vinginevyo nchi inateketea,” kimesema chanzo chetu.
Uchunguzi
umebaini kuwa kati ya kesi 423 zilizofikishwa Mahakama Kuu kati ya mwaka
2005 na 2013 hadi leo kesi iliyokwisha ni moja tu ya Shaaban Mintanga,
ambayo nayo imeisha kutokana na mashahidi muhimu kufariki dunia kabla
kesi haijasikilizwa. Kati ya mashahidi waliofariki dunia ni Mkemia Mkuu,
Dk. Ernest Mashimba, aliyefariki Septemba 2010.
Kamanda wa
Kikosi Maalumu cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, alikiri
matukio hayo kuwapo na akasema: “Mimi mamlaka yangu ni kukamata, na
kuwafikisha mahakamani. Sasa huko kama mmekuta hali iko hivyo, ambayo ni
kweli kimsingi inasikitisha na kukatisha tamaa, inabidi muwaulize huko
mahakamani au kwa DPP wao ndiyo waeleze nini kinatokea.”
JAMHURI
haikufanikiwa kuzungumza na Msajili wa Mahakama Kuu kwani mara zote kila
mwandishi wetu alipofika aliambiwa yuko kwenye vikao kwa wiki nzima, na
hata alipoacha ujumbe wa maandishi haukujibiwa.
Baada ya juhudi
za kumpata Msajili wa Mahakama Kuu kugonga mwamba, JAMHURI iliwasiliana
na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge),
William Lukuvi, ambaye Kamisheni ya Dawa za Kulevya iko chini yake. Yeye
alisema ni kweli tatizo hilo lipo, na kwamba kuna mengi zaidi ya hayo.
“Mimi
nasema sheria zinapaswa kubadilishwa, na Serikali tayari imeanza
mchakato. Mtu akipatikana na pipi za dawa za kulevya zikatolewa tumboni
mwake, nataka sheria irahisishwe na kuwezesha ashitakiwe na kufungwa
maisha ndani ya siku saba.
“Hali ilivyo sasa ambapo unapaswa
kuhifadhi ushahidi kwa miaka hadi 10 ukiendesha kesi moja, ushahidi
unapoteza ubora. Wakati mwingine mtuhumiwa anashindwa kesi anatozwa
faini ya Sh 500,000. Hatuwezi kupambana na dawa za kulevya tukashinda
vita hii kwa utaratibu huo.
“Sasa Serikali imejipanga, ipo kwenye
mchakato wa kuanzisha mahakama maalum ya kudhibiti dawa za kulevya na
kwa kweli katika hili tunataka mchakato uwe mfupi kadiri inavyowezekana.
Ndani ya muda mfupi kadiri inavyowezekana tupitishe sheria hii ili
sheria iwe kali itoe adhabu itakayowazuia wengine kufanya biashara hii,”
alisema Lukuvi.
Hivi karibuni, Tanzania imeanza kuzungukwa na
sura ya kuwa Taifa la wauza dawa za kulevya baada ya Watanzania wengi
kukamatwa ndani na nje ya nchi wakiwa na dawa hizo. Taarifa za uhakika
zilizoifikia JAMHURI zinasema Rais Jakaya Kikwete ametoa maelekezo ya
dhati kuhakikisha linafanyika jambo kubwa litakalowezesha kukamata
mtandao wa wauza dawa za kulevya na kumaliza tatizo hili nchini.
Kwa
mwezi mmoja sasa, JAMHURI imekuwa ikichapisha orodha ya wauza unga
‘dagaa’ na ‘mapapa’ hapa nchini, ambako hadi sasa gazeti hili
limekwishatangaza hadharani majina ya wauza unga 504 katika matoleo
manne yaliyotangulia.
SOURCE: JAMUHURI MEDIA |