Friday, 27 September 2013

Abdul Haji:Mkenya aliyekuwa tayari kuuawa

Abdul Haji akimwokoa mtoto asiuawe na magaidi. Picha ya maktaba 
Na  Fredy Azzah, Mwananchi

Posted  Ijumaa,Septemba27  2013  saa 12:46 PM
Kwa ufupi
  • Kikundi hicho hupata faida kubwa kutokana na biashara ya jino la tembo, kwani wao hununua jino moja kwa Dola 100 kutoka kwa majangili.
  • Fedha wanazopata hununulia silaha zozote watakazo, kuwalipa vizuri wanamgambo wao na kuwawezesha kuwalipa washirika wao fedha zitakazowafanya waishi maisha ya kifahari watakavyo.

Wakati vyombo vya usalama vya Kenya vikitangaza kulidhibiti jengo lote la Westgate lililovamiwa na magaidi wanaodaiwa kuwa wa kundi la Al-Shabaab, baadhi ya watu waliojitoa muhanga na kufanikiwa kuokoa maisha ya wengine, wanaendelea kuibuka.
Hivi karibuni gazeti hili lilichapisha habari juu ya askari wa Kikosi Maalumu cha Anga (SAS) cha Uingereza, aliyeweza kuokoa zaidi ya watu 100 ndani ya jengo hilo.
Hivi karibu, baadhi ya vyombo vya habari vya Kenya vimemnukuu pia  Abdul Haji (38) ambaye ni raia wa kawaida aliyeweza kufika ndani ya jingo hilo na kuokoa watu waliokuwa wametekwa na wanamgambo hao wanaodaiwa kuwa wa Al Shabaab.
Gazeti la Daily Nation, limemnukuu kijana huyo akisema alipata ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (SMS) kutoka kwa kaka yake ukisomeka kuwa “Nimekwamba Westgate, nadhani kuna magaidi wamevamia hapa, niombee”.
Kijana huyo ambaye asili yake ni Msomali, alisema alipata sana hofu kutokana na ujumbe huo wa kaka yake kwani ilikuwa ni wiki mbili tu tangu televisheni moja ya nchi hiyo kumtaja kaka yake huyo kama mmoja wa watu anaowasaidia magaidi hao wa Al Shabaab.
Kijana huyo ambaye ni mtoto wa Seneta, Yusuf Haji alisema hali hiyo ilimpa wasiwasi zaidi kwani tayari walishaanza kupata vitisho kutoka kwa baadhi ya watu wakiamini kuwa kweli familia yake wanawasaidia Al Shabaab.
Anasema baada ya ujumbe huo alikimbia mara moja na kwenda katika jengo hilo la Westgate, na muda mfupi tu tangu magaidi hao kuingia ndani ya jengo hilo na kuanza kuwafetulia watu risasi alikuwa ameshawasili eneo hilo.
Haji ambaye ni mfanyabishara na baba wa watoto wane wa kike, alisema aliamini kuwa magaidi hao walikuja kumfuata kaka yake na baadaye familia nzima hivyo aliamua kujitoa muhanga ili kumuokoa kaka yake na familia yake yote.
Mtoto huyo ambaye baba yake ni Seneta wa Garissa na aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ulinzi wan chi hiyo, alisema aliingia kwenye jengo hilo akiwa na bastola ambayo anaimiliki kwa kufuata sheria zote za Kenya.
Anasema kuwa, alipofika ndani ya jengo hilo aliona watu wengi wakiwa wameuwawa wakiwa wamelala chini na wengine wakiwa bado wapo hai huku milio ya risasi ikiendelea kulia kila kona.
Aliungana na watu wengine kama 10 waliokuwa ndani ya jengo hilo ambao pia walikuwa na silaha ili waone namna  ya kusaidia baadhi ya watu.
 “Nimewahi kuona miili ya watu waliokufa lakini sijawahi kuiona mingi kama ile ikiwamo ya watoto na kinamama wasiojiweza,” anasema Haji


Anasema katika ghorofa ya juu ambapo watu walikuwa wamehudhuria shindano la watoto kupika, sakafu, mafuta ya kupikia na vyakula vilivyokuwa  eneo hilo vilikuwa vimefunikwa na damu.
Anasema saa moja tangu magaidi hao wavamie jengo hilo, huku kikosi cha kupambana na ugaidi kikiwa hakijafika eneo hilo, kijana huyo na baadhi ya askari polisi waliokuwa wamefanikiwa kuingia kwenye jengo hilo waliweza kuokoa baadhi ya watu.
Inaelezwa kuwa, kaka yake ambaye jina lake halikutajwa, alikuwa amejificha kwenye choo kilichopo ghorofa ya kwanza ya jengo hilo.
Anasema kuwa, waliweza kuokoa watu wengi waliokuwa wamejificha kwenye maduka yaliyokuwa kwenye jengo hilo pamoja na watumishi wa benki ya  Barclays, ambao pamoja na wateja wao walikuwa wamejifungia ndani ya ofisi za benki hiyo zilizo ndani ya jengo hilo.
Baada ya kuokoa watu wengi kwenye ngorofa za juu, alirudi ile ya chini na kugundua kuwa kaka yake ameshasaidiwa pia kutoka nje ya jengo hilo.
“Nimekasirika kwa kitendo ambacho hawa watu wamefanya na kusingizia kuwa wametekeleza hilo kwa jina la Uislam,” anasema.
“Mimi ni Mkenya mwenye asili ya Kisomali na pia ni Muislamu, Uislamu hauubiri vurugu, wanafanya kinyume na mafundisho ya Kiislamu,” anaongeza.
“Sijisikii kama shujaa hata kidogo, yule mtoto wa kike aliyeonekana kwenye picha akinikimbilia ni shujaa, sidhani kama nilikuwa na ushujaa kama ule nilivyokuwa na umri kama wake,” anasema.
Katika hatua nyingine, baadhi ya mashirika ya kimataifa yamesema kuwa, uhalifu huo uliosababisha vifo vya zaidi ya watu 60 Kenya, umefadhiliwa na fedha zitokanazo na mauzo ya meno ya ndovu na pembe za faru.
Taarifa hizo zinasema kuwa, magaidi hao wanategemea fedha hizo kwa ajili ya kununua silaha na kufadhili uhalifu kama uliofanyika kwenye jengo la Westgate.
Kituo cha Uchunguzi wa Mambo ya Mazingira cha Afrika Kusini, kinasema kuwa asilimia 40 ya fedha zote zinazotumiwa na kundi hilo zinatokana na mapato hayo.
Mtu mmoja alinukuliwa akisema kuwa, “Shabaab wamekuwa wakijishughulisha na kununua na kuuza pembe na meno hayo ili kupata fedha za kufanikisha shughuli zake” .

Takwimu zaidi zinaonyesha kuwa, kundi hilo kwa mwaka 2011 lilipata dola za Marekani 200,000 mpaka 600,000 kwa mwezi kutokana na biashara hiyo.
Kwa takwimu za mwaka 2012, kilo moja ya meno ya tembo ilikuwa inauzwa kwa dola 1800 za Marekani.
Taarifa hizo zilifafanua kuwa kwa kawaida tembo mkubwa jino lake moja huwa kati ya kilo 50 mpaka 70.
Zinaeleza kuwa, kikundi hicho hupata faida kubwa kutokana na biashara hiyo kwani wao hununua jino moja kwa dola 100 kutoka kwa majangili.
Kutokana na hali hiyo, taarifa hizo zinasema kuwa kikundi hicho hupata fedha nyingi za kununua silaha zozote watakazo, kuwalipa vizuri wanamgambo wao na kuwawezesha kuwalipa washirika wao fedha zitakazowafanya waishi maisha ya kifahari watakavyo.
Mapema mwaka huu, Kenya ilisema imeanza uchunguzi juu ya kikundi hicho kujishughulisha na ujangili wa tembo na faru nchini humo.
Ingawa Serikali haijaweza kutoa matokeo ya uchunguzi huo kama ni kweli kiundi hicho kinahusika au kinahusika kwa kiwango gani, tafiti za mashirika mengine zinathibitisha kuwa Al Shabaab wanawatesa Wakenya kwa kutumia rasilimali zilizoko Kenya.
Baadhi ya wananchi wanaomba Serikali kuchukua hatua kali za kupambana na ujangili kama mojawapo ya njia za kupambana na matukio ya kigaidi nchini humo.
Vitendo vya kigaidi kwa kiasi kikubwa sio tu kwamba vinawafanya wananchi kuishi wakiwa na hofu, pia vinachangia kurudisha nyuma maendeleo kwa wawekezaji kuogopa kuwekeza katika taifa lisilo na amani.
Aidha ni jambo linaloweza kusababisha wawekezaji kupungua, hivyo wananchi wengi wameshauri kuimarika kwa ulinzi ikiwemo kupambana na njia mbalimbali ambazo Al Shabaab wanafanya kuingiza kipato.

SOURCE: MWANANCHI