Na Florence Majani, Mwananchi
Posted Ijumaa,Septemba27 2013 saa 14:37 PM
Posted Ijumaa,Septemba27 2013 saa 14:37 PM
Kwa ufupi
- Wanawake wenye kiwango kikubwa cha vichocheo (homoni) aina ya oestradiol, wana mwamko mkubwa wa kushiriki tendo la ndoa kuliko wanawake wenzao wenye kiwango kidogo cha vichocheo hivyo.
Ni ajabu, wala si jambo la kawaida kwa wanawake
walio wengi kujikuta katika matamanio, kiasi cha kujikuta wakilazimika
kushiriki tendo la ndoa.
Hata hivyo, homoni kadhaa zilizoko katika miili ya wengine zinawachochea kujitumbukiza kwenye tendo hilo.
Utafiti wa baadhi ya wanasayansi umeonyesha kuwa
baadhi yao wana kiwango kikubwa cha vichocheo mwili kinachoweza
kushawishika kuwa na mpenzi wa nje au kumchoka haraka mwenza wake baada
ya kuishi naye kwa kipindi fulani.
Wanasayansi hao wamefanya uchunguzi na kugundua
kuwa, wanawake wenye kiwango kikubwa cha vichocheo (homoni) aina ya
oestradiol, wana mwamko mkubwa wa kushiriki tendo la ndoa kuliko
wanawake wenzao wenye kiwango kidogo cha vichocheo hivyo.
Vichocheo hivi aina ya oestradiol (oestrogen) ni
vile vinavyotumika katika kuzalisha mayai ya uzazi wa mwanamke. Pia,
vichocheo hivyo ni vile ambavyo humpa mwanamke mwamko wa tendo la ndoa.
Wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Saikolojia nchini
Uingereza walifanya utafiti kuhusu uhusiano uliopo kati ya vichocheo na
tabia za watu na kubaini kuwa kiwango cha vichocheo huweza kuelezea
tabia ya mwanamke ikiwamo kumsababisha kuwa na tamaa za mwili zaidi
tofauti na wanawake wengine.
Wanasayansi hao, Dk Kristina Durante na Norm Li
walitoa ushahidi wa utafiti wao kuwa mfumo wa kisaikolojia unachangia
kwa kiasi kikubwa katika mwamko wa tendo la ndoa na tabia kwa wanawake.
Wanawake 52 wenye umri wa kati ya miaka 17 na 30,
wote wanafunzi wa vyuo vikuu walishiriki katika utafiti huo na
kuambiwa wasitumie njia yeyote ya uzazi wa mpango kwa sababu njia hizo
huongeza vichocheo mwilini.
Kwa upande wao, watafiti walipima kiwango cha
homoni hizo kwa wanawake wote na walipewa maswali ya kujibu yaliyohusu
mienendo yao ya kimapenzi, kutosheka na wenzao pamoja na uwezo wa
kuvumilia kutofanya tendo la ndoa kwa kipindi fulani.
Pia, washiriki hao walitakiwa kujibu maswali maalumu ambayo yanapima uwezekano wa washiriki hao kuwasaliti wenzao wao.
Mwishowe, watafiti hao walibaini kuwa, wanawake
wenye kiwango kikubwa cha vichocheo vya oestradiol wanapenda utani,
wanapenda kupigana busu na ni rahisi kupata mwenza mpya wa kudumu wakati
wowote.
“Matokeo yetu yalibaini kuwa, wanawake wenye
kiwango kikubwa cha rutuba za uzazi hawatosheki na mwenza mmoja hasa
waliyeishi naye kwa muda mrefu. Wana uwezo wa kutafuta mwenza mwingine
anayewatosheleza,” alieleza Dk Durante.
Hata hivyo, daktari huyo alisema kuwa, wanawake wa aina hiyo
hawapendi kushiriki tendo la ndoa ovyo au kuwa na wapenzi wa muda mfupi,
bali wanaweza kuwa na wenza wawili wa kudumu ili mradi wamtosheleze.
Almasi Nyangasa, Daktari Bingwa wa magonjwa na
upasuaji wa moyo anasema, vichocheo vya mwanamke vinabadilika kulingana
na mzunguko wake wa mwezi.
“Wanawake wana vichocheo vya aina nyingi. Viwango vya vichocheo hivyo hubadilika kulingana na mzunguko wake” anasema
Anaizungumzia homoni ya oestradiol na kusema kuwa
homoni hiyo inatakiwa kuwa katika kiwango cha kawaida, ikizidi au
ikipungua basi mwanamke anaweza kuwa na tabia zisizo za kawaida.
Kwa mfano, mwanamke anaweza kuwa na mwamko wa
kufanya mapenzi au asiwe nao kabisa. Pia, baadhi wanapata mabadiliko ya
miili yao kama chunusi au kuwa na hasira.
“ Hata hivyo, si lazima mwanamke mwenye kiwango
kikubwa cha homoni hii akawa na uwezo mkubwa wa kushika mimba. Wingi wa
homoni hizo zinaweza kumfanya mimba ziharibike au asishike kabisa”
anasema
Dk Nyangasa anasema tabia za mwanamke
hubadilika pindi homoni zake zinapopita katika mzunguko ambao
husababisha yai kupevushwa na ama ashike mimba au apate hedhi.
“Inawezekana mwanamke akawa siyo wa kawaida,
hivyo akawa na homoni hii kwa kiasi kikubwa hivyo akawa na mwamko mkubwa
wa tendo la ndoa” anasema
Anaongeza kuwa wingi au uchache wa homoni huweza
kuharibu mzunguko wa hedhi kwa mwanamke ambapo anaweza kupata hedhi siku
nyingi zaidi au siku chache.
Naye Dk Meshack Shimwela, Bingwa wa Magonjwa ya Ndani ya Mwili, anasema homoni humbadilisha mwanamke kwa hali ya ajabu.
Anatoa mfano kuwa wako wanawake wenye vinyweleo
vingi mikononi na miguuni, wenye sauti za kiume na wenye miili imara
mithili wa wanaume.
Kuhusu mwamko mkubwa wa kujamiiana, Dk Shimwela
anasema wingi wa homoni ukizidi unaweza kumfanya mwanamke akawa na
mwamko mkubwa lakini wapo ambao si wa kawaida.
“Kuna watu ambao si wa kawaida, lakini hili linahusiana na saikolojia ya mtu pamoja na tabia yake,.” Anasema.
Hata hivyo anasema, mwamko wa kujamiiana humkuta
kila mwanamke kadri homoni zake zinavyobadilika lakini baadhi yao
homoni zao zinakuwa nyingi na wanapata mwamko ambao si wa kawaida.
Dk Antoinnete Molekhele wa Kitengo cha Afya ya
Uzazi, Hospitali ya Rosebank, Afrika Kusini anachambua namna vichocheo
vinavyofanya kazi na kusema kuwa, mayai ndiyo yanayozalisha homoni.
“Mayai yetu yanatengeneza homoni za oestrogen na
progesterone kwa kiasi kikubwa na kiasi kidogo cha homoni za kiume aina
ya testosterone na andorstenedione,” anasema
Pia, anasema wanawake na wanaume wana homoni mbili za muhimu ambazo zinatengenezwa na tezi ya ‘pituitary’ ambazo ni FSH na LH.
Anasema kichochezi cha FSH (Follicle Stimulating
Hormones) kinadhibiti utengenezwaji wa mayai na kichochezi cha LH (au
luteinizing horomone) inasimamia utengenezwa wa vichocheo vya mwamko wa
kujamiiana.
“Kichochezi cha LH, ndicho kinachosimamia kwa
kiasi kikubwa mwamko wa kujamiiana na inapozidi kiwango chake cha
kawaida basi inaweza kumuathiri mwanamke,” anasema Dk Molekhele
Kwa wanawake, kiwango cha homoni za oestrogen
(oestradiol) hupanda taratibu katikati ya mwezi, kisha huanza kushuka
kwa kasi wakati yai linachavushwa na siku ya 14 hushuka kabisa na
mwanamke huanza kupata hedhi.
“Wanawake hutofautiana viwango vya homoni hii na kuwafanya kuwa tofauti linapokuja suala la mwamko.” Anasema
Anaongeza kuwa, homoni humuathiri zaidi mwanamke
ambaye anaanza kufikia kikomo cha hedhi, kwani wakati mwingine huweza
kupata dalili za ujauzito wakati hana au kupata hasira na kukosa
kujiamini.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI