Kwa ufupi
Hatua hiyo imechukuliwa na uongozi wa JNIA baada ya kuagizwa na Dk Harrison Mwakyembe kuwafukuza kazi.
Dar es Salaam. Mkurugenzi wa
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA), Moses Malaki,
amesema watuhumiwa wa njama za kupitisha kilo 150 za dawa za kulevya
aina ya Crystal Methamphetamine, watasimamishwa kazi wakati wowote
kuanzia leo kabla ya kupewa nafasi ya kujitetea kwenye tume itakayoundwa
kuwachunguza.
Hatua hiyo inatokana na agizo la Waziri wa
Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, kutaka wote waliohusika na njama hizo
kuchukuliwa hatua za kisheria.
Malaki ambaye awali alionyesha kushangazwa na
kiasi kikubwa cha dawa hizo kupita, alisema utaratibu unakamilika wa
kuundwa tume na kuwasimamisha kazi wahusika.
“Baada ya tume kukamilika na kupewa hadidu rejea,
tutawaita mmoja mmoja kwenye kujieleza, hapo tutajua kama wahusika
watakuwa na hatia au la,” alisema.
Alisema baada ya kumaliza kazi, tume itatoa maelekezo kwa Serikali kinachotakiwa kufanyika.
Katika hatua nyingine, jalada la mtuhumiwa wa
dawa za kulevya aliyekamatwa JNIA Alhamisi iliyopita, akiwa na kete 84
na misokoto 34 ya bangi linapelekwa kwa Mwanasheria wa Serikali leo.
Kamanda wa Polisi Vikosi cha Viwanja vya Ndege
nchini, Deusdedit Kato, alisema jana kuwa wameshakamilisha upelelezi na
kwamba, wanasubiri maelekezo kutoka kwa Mwanasheria Mkuu.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa JNIA mwishoni mwa wiki
iliyopita, akiwa katika harakati za kusafirisha dawa hizo kwenda nchini
Italia kupitia Zurich, Uswisi.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, kumekuja ikiwa ni
siku moja baada ya Dk Mwakyembe kufanya ziara ya kushtukiza JNIA kukagua
utendaji.
source: Mwananchi
source: Mwananchi