Kwa ufupi
Inawezekana hufurahii umbo ulilozaliwa nalo. Kama ndivyo sasa teknolojia hiyo tayari imeingia nchini.
Miaka ya hivi karibuni, kumeibuka wimbi kubwa la
wanawake kwa wanaume ambao wanafanyia matengenezo maumbile yao ‘Plastic
Surgery’ kama sura, kupunguza vitambi, kuongeza makalio, kuongeza au
kupunguza matiti.
Awali wimbi hili lilibuka zaidi kwenye nchi za
magharibi, lakini kutokana na utandawazi, dunia kuwa kijiji, kwa hivi
sasa watu wengi wamekuwa na mwamko wa kutengeneza shepu katika sehemu
mbalimbali za maumbile yao.
Kwa hapa Tanzania, watu wengi hukimbilia nchini
India kwenda kufanya upasuaji wa aina hii ambao wengi wao wanafanya
aidha kwa kujua au kwa kutokujua madhara yake, lakini lengo kuu ni
kujipendezesha na kuonekana mwenye mvuto machoni mwa watu.
Dk Zaituni Sanya bingwa wa upasuaji Hospitali ya
Taifa Muhimbili alifanya mahojiano maalum na Mwandishi wa habari hizi na
kusema: “Kwa hapa Tanzania upasuaji unaofanyika ni ule wa kurekebisha
sura na ule wa matiti ndiyo sana.”alisema
Akifafanua zaidi alisema: “Kwa upande wa sura
upasuaji tunaofanya ni kwa wale ambao utakuta wameota vinyama au wana
uvimbe uvimbe kwenye sura, ndiyo tunawafanyia na tena upasuaji wake
unatumia nyuzi nyembamba sana maalumu ambazo hazionekani, lakini ule wa
kuchonga sura kama ule uliokuwa ukifanywa na kina Michael Jackson
hatufanyi.
“Upasuaji wa matiti ndiyo tunafanya sana hapa
nchini, mimi binafsi ninafanya na kwa hapa Muhimbili gharama zake ni
zilezile kama za upasuaji mwingine wowote, lakini kwenye hospitali za
binafsi upasuaji huu ni gharama sana.
“Wengi wanaokuja hapa unakuta niwasichana kuanzia
umri wa miaka 20 hadi 35 na hawa wanakuja siyo kwamba wanaumwa la hasha,
wanafanya upasuaji huu kwa ajili ya urembo tu, unakuta matiti yao ni
makubwa hivyo wanakuja kwa lengo la kuyapunguza.
“Matiti makubwa yanasababishwa na chembe chembe
ambazo zinatengeneza mafuta na kuyafanya kuwa makubwa kupita kiasi,
tunapofanya upasuaji tunaondoa mafuta yaliyozidi na kuliweka titi kwenye
umbo zuri ambalo mhusika atataka na kwa saizi ambayo atapendelea, na
pia wakati wa kushona inabidi uangalifu sana ili isisababishe madhara.
Mbali na kupunguza wanaongeza?
“Kwa hapa Tanzania hapana, toka nimeingia kwenye
udaktari wa upasuaji mwaka 2004 sijapata mgonjwa ambaye anahitaji
kuongeza ukubwa wa matiti zaidi ni kuyapunguza, na hii si tu kwa hapa
Muhimbili bali pia kwenye hospitali kubwa zote za watu binafsi hakuna
wagonjwa wa aina hii zaidi ya wale wanaohitaji kupunguza.
Hata hivyo Dk Sanya alisema kuwa hana takwimu
sahihi za idadi ya watu ambao wanaenda kwa ajili ya tatizo hilo zaidi ya
umri ambao wengi wao ni wasichana kati ya miaka 20 hadi 35.
“Upasuaji wa kupunguza matiti hauna madhara yoyote
kwa vile tunapunguza chembe chembe zilizozidi pamoja na mafuta na
hatutumii kemikali zozote. Ila kama upasuaji wake utakosewa basi madhara
ambayo muhusika atapata ni kuwa hatoweza kumnyonyesha mtoto na kama
mnavyojua matiti yakijaa misuli inapanuka na hivyo ni lazima mhusika
atapata maumivu makali ambayo yatatibiwa na dawa za kutuliza maumivu.
“Kansa ni ugonjwa unaotokea tu kutokana na mfumo wa maisha na
vyakula tunavyokula, lakini upasuaji huu wa kupunguza matiti
hausababishi kansa, na maziwa mtoto asiponyonya kwa siku kadhaa
‘automatic’ yatakauka yenyewe ndiyo maana hata mama anayenyonyesha
akiacha kumnyonyesha mtoto kwa wiki moja, mbili maziwa yanakauka.
“Ila kwa wale wanaongeza ukubwa wa matiti kuna
madhara makubwa na si maziwa tu hata wale wanaongeza hipsi na makalio
kwa kuwa ufanyaji wake unatumia kemikali... “Kitu chochote ambacho ni
‘artificial’ kina madhara na madhara makubwa ya kemikali zinazotumika
kuongeza maziwa, hipsi na makalio ni saratani kwa kuwa ngozi ni
‘delicate’.
“Watu wanaofanya upasuaji huu kwa ajili ya urembo
lazima watakuwa wanatumia maisha yao yote (medication) hali hii ni
kujilimbikizia dawa mwilini, mwisho wa siku anajiua mwenyewe kama
ilivyotokea kwa Michael Jackson.
WANAWAKE WANASEMAJE
Rhoda Sanga: Yawe makubwa yenye mvuto siyo pwaaa
kama yanataka kumwagika, ukiwa na makubwa yaliyokaa vizuri unavutia
zaidi ya yule mwenye vinyonyo vidogo.
Aisha Ally: Wengine wanatumia matiti kuvutia
wanaume, wengine wanapenda tu jinsi yanavyowavutia na wengine tunapenda
kumfurahisha mume na kupenda jinsi tu yalivyo, na ukiwa na ulapa lazima
uongeze ‘sponge’ yavimbe.
WANAUME WANASEMAJE?
Henry Masanja: “ Wanawake wamegundua wanaume ndiyo
wanapenda, na ni kweli tunapenda na yanatumika kwa staili nyingi,
maziwa makubwa yana mvuto wa kimahaba na kimuonekano tofauti na mwenye
maziwa madogo.
Allan Masawe: “Napenda makubwa yaliyosimama
yamejaa siyo kandambili (yaliyolala) yanashikika, yanaongeza mvuto
katika masula ya kimapenzi, unaweza maliza haja zako.
Kwa mujibu wa gazeti la The Sun la Uingereza,mama
mmoja mwenye umri wa miaka 46 anakumbuka namna alivyokaribia kupoteza
maisha kutokana na matumizi ya dawa kwa ajili ya kufanyia marekebisho
baadhi ya viungo vyake vya mwili, kwa nia ya kujipendezesha zaidi.
Apryl aliyetumia muda wake mwingi wa ujana kuremba nywele zake akizipaka dawa za aiana mbalimbali sasa anajuta.
Akiwa na kiu ya kurembesha mwili wake na kuwavutia
wale wanaokatiza mbele ya macho yao, Apryl alichukua jukumu la
kuongezwe vikorombwezo kwenye baadhi ya viungo vyake. Sasa akiwa na umri
wa miaka 46, mwanamke huyo anatoa sauti ya masikitiko huku akiwaonya
wengine kutofuata mkondo wa maisha aliyopitia.
Anasema kuwa amelazimika kujitokeza hadharani na kuelezea
historia ya maisha yake, ili iwe funzo wa wengine wenye kiu kama
aliyokuwa nayo awali. Anasema kuwa hakuwa na ufahamu wa kutosha juu ya
kile alichokwenda kukifanya kama kingeweza kuvuruga kabisa amani na
mwonekano wake aliojaaliwa na Mwenyezi Mungu.
Maisha yake kwa sasa ni ya wasiwasi na wakati
mwingine anatakiwa kuwa mwangalifu mkubwa juu ya vyakula anavyokula,
kutokana na kile kinachoelezwa kwamba ni mabadiliko ya kijenetiki
yaliyojitokeza baada ya kutumia dawa ambazo zimefumua mfumo wa mtitiriko
wa tishu za mwili.
“Kwa sasa naishi maisha mabaya… natakiwa kuwa
mwangalifu saana maana nimejikuta nasumbuliwa na aleji ya mara kwa
mara…nah ii ni kutokana na zile sindano nilizochomwa ili kuunda upya
mwili wangu.”
Anasema kuwa anakumbuka kuwa na kiu ya kuwa na
mwonekano kama ule wa mwanamuziki Janet Jackoson ama J-Lo, ambao mara
zote huonekana nadhifu na wanawake wenye kuvutia machoni mwa watu
kutokana na maumbile yao kuwa na mvuto wa ajabu.
Anakumbuka mwaka 2004 ndiyo ulibadilisha historia
ya maisha yake pale alipokutana na dada mmoja, ambaye baada ya
majadiliano ya muda mfupi alichukua uamuzi wa kuchomwa sindano hatimaye
mwili wake upate madiliko makubwa kwa kufanana na wale kinadada
aliowataja.
Apryl ambaye ni mkazi katika jiji la Los Angeles,
Marekani anasema kuwa: “Nilipozungumza na yule dada na namna
alivyonionyesha kuwa ni mtu mwenye kuelewa mambo mengi nilikubali wazo
la kuchomwa sindano ya kubadilisha mwonekano wa mwili wangu.”
“Nilichomwa sindano mara mbili kisha nikatulia….kusema kweli uamuzi ule ulikuwa kama kujitakia kifo.”
Inasemekana kuwa dada aliyemchoma sindano hiyo
alikuwa hana utalamu wowote wa utabibu mbali ya kutaka fedha kwa ajili
ya kuendeshea maisha yake. Inaelezwa kwamba alilipwa kiasi cha pauni za
Uingereza 650.
Madaktari walioendesha uchunguzi waligundua kuwa
dawa iliyotumika kwa dada huyo ilikuwa na madhara makubwa kwa mwili wa
binadamu, kwani ilitengenezwa maalumu kwa ajili ya kutumika katika
viwanda.
Shauku yangu ya kutaka kuwa na mwonekano mpya na
namna nilivyomwamini dada yule nikachukua uamuzi wa mara moja kuruhusu
nichomwe sindano ile. Nilimwamini sana yule dada kwa vile alionekana
kama mweledi na mtaalamu aliyebobea.”
source: Mwananchi news paper
source: Mwananchi news paper