*Watumia madini kutapeli Wazungu hadi bilioni 160/-, watamba
*Mwanza, Dar, DRC, Zambia, Papa Msofe, Aurora waongoza ‘jeshi’
*BoT, NBC, Exim Bank, Polisi, Mahakama, Uhamiaji nao watumika.
Baada
ya sifa ya Tanzania kuingia doa kutokana na watu wengi maarufu
kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, uchunguzi wa JAMHURI
umebaini kuwa matajiri wengi nchini wanatuhumiwa kufanya utapeli wa
kutupwa kwa Wazungu kupitia ahadi hewa za kuwauzia madini.
Taarifa nyeti zilizonaswa na Jamhuri,
zinaonyesha uchunguzi wa kina uliofanywa na Serikali umebaini uwepo wa
wafanyabiashara wenye leseni halali za udalali wa madini, lakini
biashara wanayofanya ni kuwatapeli Wazungu, kisha wanatembeza rushwa kwa
baadhi ya polisi na mahakamani kukatisha tamaa Wazungu waliotapeliwa.
“Ndugu
zangu nawambia watu hawa hawana woga kabisa. Majina haya unayoyaona
wizara imefikia uamuzi wa kuyapeleka kwa Mheshimiwa Rais [Jakaya]
Kikwete, pengine aingilie kati na kuzilazimisha mahakama na hawa polisi
kuhakikisha wahusika wanakamatwa… jina la Tanzania linanuka nje ya nchi
kwa sababu ya watu hawa,” kilisema chanzo chetu.
Baada ya kupata orodha ya majina haya, JAMHURI
kwa nyakati tofauti iliwasiliana na matajiri wanaoutumiwa mmoja baada
ya mwingine kwa kutumia barua pepe na simu zao za mkononi, na mchezo
ukawa ule ule jinsi wanavyowatapeli Wazungu.
Hawa
wana utajiri mkubwa ajabu. Wanaingia kwenye mtandao na kuwadanganya
Wazungu kuwa wana madini hadi kilo 600, wanawatumia vivuli vya leseni
zao halali walizozipata kutoka Wizara ya Nishati na Madini, kisha
Wazungu wanaamini kuwa ni biashara halali, na wanapotuma fedha tu
zinaondolewa kwenye akaunti mara moja.
Mtandao
huu ni mpana kwani unahusisha baadhi ya watumishi wa benki za hapa
Tanzania na nje ya Nchi ikiwamo Marekani na Australia, ambako mabilioni
ya fedha yanaingizwa kwenye akaunti kwa njia ya utapeli na kuondolewa
haraka. Wahusika wanamiliki magari ya kifahari na wanajenga maghorofa.
Maeneo
yaliyokithiri katika utapeli wa madini ni Dar es Salaam, Arusha na
Mwanza. Waraka ulioonwa na Jamhuri unaokwenda kwa Rais unaonyesha kuwa
vitendo vinavyoendelea sasa hivi vya utapeli katika biashara ya madini
nchi vinavyochafua sifa ya Tanzania na kuikosesha serikali mapato
yanayotokana na biashara ya madini.
“Kutokana
na tabia hiyo isiyofaa nchi inapoteza imani ya kibiashara kutoka kwa
wafanyabisahara wa nje na hata wa ndani kwa sababu ya watu wasio
waaminifu. Matukio ya utapeli katika biashara ya madini kwa namna moja
ama nyingine yanaathiri pia wafanyabisahara waaminifu na wachimbaji wa
madini,” inasema sehemu ya waraka huo.
Baadhi ya matukio ya utapeli
Oktoba
15, 2009, Japheti Kija Mnada anatuhumiwa kumtapeli Khalil Ibrahim
mwenyeji wa Dubai U.A.E madini aina ya dhahabu yenye uzito wa kilo 10
yalikuwa na thamani ya Sh 300,000,000 katika utapaeli uliotokea Mkoa wa
Mwanza.
Aprili
13, 2011 Aloyce Chacha Keng’anya anatuhumiwa kumtapeli raia wa Korea
Kusini, Kim Sun Tae madini kilo 2 yenye thamani ya dola 4,400 za
Marekani katika tukio lilitokea Mtaa wa Uhuru Mwanza.
Juni
20, 2011 Japheti Kija Mmanda anatuhumiwa kumtapeli Gordon Fraizer
madini kilo 120.572 yenye thamani ya dola 4,301,600.32 za Marekani
(karibu Sh bilioni 7). Fedha hizi ziliingizwa na Fraizer katika Benki ya
Exim Mwanza na mhusika akazitoa ndani ya muda mfupi. Mzungu alikaa hapa
nchini akizungushwa polisi na matapeli hadi akaishiwa fedha na kurejea
kwao Uingereza.
Kampuni
ya Royal Security Group (T) LTD Dar es Salaam inatuhumiwa kumtapeli
raia wa Uingereza Jonathan Andrew Golightly madini kilo 5 za dhahabu
zenye thamani ya pauni 78,000 (karibu Sh milioni 200) na kilo 100 za
madini ambayo JAMHURI haikufanikiwa kufahamu
mara moja ni yapi yenye thamani ya Sh 158,496,000 utapeli huu ulifanyika
kupitia Benki ya NBC Mtaa wa Samora, Dar es Salaam Februari 2, mwaka
2010.
Aprili
18, 2012 katika eneo lisilofahamika Dar es Salaam Mkurugenzi wa Kampuni
ya Trans Trading and Shipping LTD, Said Rashid Ntimizi anatuhumiwa
kumtapeli, Mzungu Dk. David Oyengo madini kilo 10 yenye thamani ya dola
250,000 za Marekani karibu Sh milioni 440.
Novemba
11, 2011 katika tukio lililotokea Jijini Dar es Salaam , Richard Kaseya
anatuhumiwa kumtapeli Raia wa Australia, Collin Ostron kilo 100 za
madini yenye thamani ya dola 1,450,000 za Marekani (karibu Sh bilioni
2.4) ambapo alilipwa dola 195,000 kama malipo ya awali.
Kuthibitisha
mtandao huu wa kuibia Wazungu ulivyo mpana, Oktoba 26, 2010 Benki Kuu
ya Tanzania (BoT) Dar es Salaam ilitumika kupitisha mabilioni ya
Frederick James Chacha anayotuhumiwa kuitapeli Kampuni ya Eminent
Capital ya Uingereza kuwa ana kilo 100 za madini. Kupitia akauni
aliyoifungua Benki Kuu Chacha aliingiziwa kiasi cha dola 857,000 (karibu
Sh bilioni 1.4) kwenye akaunti yake.
Mwaka
2010 Jijini Dar es Salaam Freerick James Chacha anatuhumiwa kuiitapeli
Kampuni ya Eminent Capital ya Uingereza kilo 72 za madini yenye thamani
ya Dola 2,033,130.
Mwaka
2010 Jijini Dar es Salaam Freerick James Chacha anatuhumiwa kuitapeli
tena Kampuni ya Eminent Capital ya Uingereza kilo 100 za madini yenye
thamani ya dola 4,062,500 (karibu Sh bilioni 6.4) na mwaka 2008 alipata
kuitapeli kampuni hiyo hiyo dola 2,033,13 (karibu Sh bilioni 3.2) karibu
sh akiwambia kuwa ana madini ya dhahabu wastani wa kilo 72, kisha
akabadili jina la kampuni.
Mwaka
2010 kupitia Benki ya Exim Bank Mwanza mteja aliyejitambulisha kama
SADC aliitapeli Kampuni ya Gold and Gemstone Traders ya Mwanza wastani
wa dola 390,000 (karibu Sh milioni 600) zikiwa sehemu ya mzigo mkubwa wa
madini kilo 500 aliyowaahidi kuwapatia yenye thamani Dola 13,000,000
(Sh bilioni 164.8). Alipopata malipo ya awali akatimka.
Majina ya matajiri wanaotuhumiwa kutapeli Wazungu
Yafuatayo
ni majina ya matajiri wanaotuhumiwa kuwa vinara au kuongoza magenge ya
kutapeli Wazungu hapa nchini. Wengine ni raia wa kigeni wanaoishi hapa
nchini bila vibali na wengine wana vibali au kampuni halali lakini
wanafanya biashara haramu.
Watuhumiwa
matajiri hao ni mchanganyiko wa raia wa Congo na Watanzania, ambao
baadhi yao JAMHJURI imeamua kuweka hadi namba zao gazetini. Hawa ni Jean
Claude Mundeke Kambamba, Ruphin Kazadi Elumba, Jean Claude Kanza
Dyansangu na Abubakar Awaz anayemiliki kampuni ya Trans Trading and
Shipping LTD ya S. L. P. 16178 Dar es Salaam Tel 255653111555 Email
rashidsaid@yahoo.comph . Katika kampuni hiyo wamo pia Rashid Said
Ntimizi na Joseph Ntabazi.
Wengine
ni Rodgers David Mawelle, Tambwe Moses Chunda mwenye hati ya kusafiria
Na AB 083159, Raia wa Zambia Musonda Chisimba, Mtanzania Kalibi Luis
Brown mwenye hati ya kusafiria Na AB 297257, Kashinde Lutshakula Jean
Claude mwenye hati ya kusafiria Na OB120538, John Chizsumo raia wa
Kenya, Zenga Bongeili Andy na Mandege Kibwana Amran Said mwenye hati Na
AB 049031.
Wamo
pia Yaofanga Isa Yauli (RDC) mwenye hati Na OB 23190997, Mulumba
Baptista Fernando (RDC), Ally Aurora wa S.L.P 8450 Aurora Security Co
LTD Plot No 192 Undali Street Upanga na pia anatumia anwani nyingine ya
S.L.P 2365 Dar Salaam simu 255 22 2124439 na Fax 255- 22-2124437. Hapa
yupo pia Abdulkarim Omari Sadik-Uorora anatumia namba hiyo hiyo. Hawa
kina Aurora kuna mmoja amefariki hivi karibuni.
Papa
Msofe, ambaye ni mkazi wa Mikocheni Dar es Salaam naye yumo kwenye
kundi hili. Wengine ni Naftari M Njoree a.k.a Mmasai, ambaye ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya The Arcade yenye makao yake Plot 72
Block A Old Bagamoyo Road S. L. P 80026 Dar es Salaam Tel 255 2774924
Fax 255-22-2774925 Cell 255 719750888 au 255 754 282624 na Email:
info@kiutuadiventures.com, Web kiutuadventures.com.
Orodha
ya matajiri hawa ni ndefu. Wamo David Kazibwe anayetumia simu Na
255-765444888 wa kampuni ya Royal Security Group LTD inayotumia pia Fax
Na 255-222124437, Ally Selemani Hamis 0716 999987 na Johnson a.k.a
Custom official 0713 466622 wote wa kampuni hiyo. Wengine ni Japhet Kija
Mnanda mwenye utambulisho wa DL 19113/2009 wa Mwanza na Aloyce Chacha
Kengenya anayeishi mtaa wa Uhuru Mwanza.
Taarifa
za uhakika zinasema matajiri hawa watakamatwa wakati wowote kuanzia
sasa, baada ya kuwa taarifa zao zimefikishwa Ikulu na Rais Jakaya
Kikwete akasema: “Sina urafiki na mtenda maovu. Kama hawa mmejiridhisha
kuwa wanatapeli watu, wakamateni tu.
“Yeyote
atakayewakwamisha nileteeni taarifa kuwa fulani ndiye kikwazo katika
kuwakamata ili mimi nipambane na huyo asiyeitakia mema nchi yetu.
Haiwezekani, nchi yetu ikageuzwa taifa la matapeli,” mtoa habari wetu
alisema akimkariri Rais Kikwete kuchukuzwa na utapeli huu mara tu
alipopata taarifa hizi hivi karibuni. Kampuni hizo zimesajiliwa kihalali
lakini zinajihusisha na utapeli wa madini
Biashara ya madini inavyofanyika
Biashara
udanganyifu wa madini hufanyika kwa wahusika kuanza kutangaza biashara
yao kupitia mtandao wa internet na kupitia kwa watu ambao wanafahamiana
nao wasiojua tabia zao kwa kufahamisha wateja kuwa wao au kampuni yao
wanajihusisha na biashara ya madini ya vito dhahabu cooper au madini
mengine kwa njia hiyo pia hushawishi wateja kuwa wauzia madini hayo kwa
bei nafuu ukilinganisha na bei ya soko.
Matapeli
hao pia wanazo nyaraka halali kutoka wizara husika na pia wanakuwa na
nyaraka za kughushi wateja wanapopatikana na huonyeshwa nyaraka halali
na madini halisi yanayojulikana kwa lugha ya kitapeli kama RUNGU. Mara
nyingi wakati wa kufanya biashara matapeli hao huja na askari kutoka
Jeshi la Polisi au Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa
nia ya kuwaaminisha kuwa wanafanya biashara halali.
Wakati
mwingine askari wanakuwa si askari halisi katika mazingira hayo
humshawishi mteja kutoa gharama za wali kwa ajili ya uhakiki wa madini,
mrabaha wa Serikali na gharama nyinginezo. Kinyume na matarajio ya
ateja, wanapomaliza kufanya malipo bila kujua hupewa hati feki za malipo
zilizogushiwa zikiashiria kuwa zinatoka serikalini.
Nyaraka
hizo huwa na mihuri na sahihi zinazofanana na nyaraka halali za
serikali kumjenga mteja imani na kumfanya atoe malipo kupita benki kumbe
ni kaunti za matapeli. Hadi sasa benki zilizothibitika kutumika kwa
mchezo huu ni Exim Bank (T) Ltd, FBME Bank, NBC Bank, BoT na baadhi ya
Benki za Marekani.
Nyaraka
wanazotumia kudanganya wateja ni kibali cha kuuza madini nje ya nchi,
gharama ya kubadili umiliki wa dhahabu kutoka jina moja kwenda jingine,
na wanakwenda mbali zaidi wanaanzisha vibali vipya vinavyoonyesha kuna
udhibiti katika ngazi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuya ya
Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kuwa jumuiya hizi
zinatoa vibali vinavyopaswa kulipiwa.
Baada
ya mteja kulipa gharama hizo matapeli hayo humtaka mteja kulipa malipo
yaliyosalia, kabla biashara haijakamilika ili mteja akabidhiwe madini
yake. Malipo akiishafanyika, matapeli hayo huwasiliana na matapeli
wenzao ambao wanakwenda katika eneo la tukio na kujifanya ni askari
polisi kisha huakamata matapeli hao na wanunuzi kwa maelezo kuwa
wamekutwa na kitu chochote haramu kwa mfano noti bandia, dawa za kulevya
au bangi.
Ikiwa
mteja ni raia wa kigeni matapeli hao huwasiliana na baadhi ya maafisa
wa polisi ambao wanashirikiana nao kumtapeli mteja na kumwangaisha
kujikwamua na kesi bandia badala ya kujishughulisha na biashara ya
madini.
Ikiwa
mteja ni raia wa kigeni matapeli hao huwasiliana na baadhi ya maafisa
uhamiaji ambao wanashirikiana nao pia katika utapeli na kumurudisha
mgeni huyo nchini kwake kwa kisingizio kuwa amehuska na biashara haramu.
Wakati
mwingine mteja anaweza kutapeliwa na matapeli na kumtoroka bila ya
kukamatwa na polisi, mteja anaripoti utapeli huo polisi huwasaka
matapeli na wakiwakamata inadaiwa kuwa matapeli hutoa rushwa kwa polisi
na maaafisa wa Ofisi ya Mkurugenzi Mashtaka ya Jinai (DPP) hivyo jalada
la kesi hiyo hupelekwa mahakamani na ushahidi dhaifu ambao hautakuwa na
ushahidi wa kuwatia hatiani matapeli hao ili haki itendeke.
Kuna
nyakati kesi hizo huwaingiza mahakimu kwenye mtandao ambao huzipangia
tarehe za mbali na hivyo mteja huishiwa na fedha za kuishi hapa nchini
na visa yake na kulazimika kuondoka kurejea kwao kuepuka kukumbwa na
kosa za kuishi nchini bila visa halali au kuishiwa fedha akauza hadi
nguo.
Serikali ilichoshauriwa
Baada
ya Wizara ya Nishati na Madini kuchunguza ikajiridhisha na uwapo wa
matapeli hawa na kutengeneza majalada yenye hadi namba za simu za
mawasiliano, barua pepe wanazotumia kutapeli na kila aina ya ushahidi,
wameamua kupendekeza kwa Rais aruhusu Idara ya Madini ishirikiane na
TMAA kuhakiki leseni zote za biashara ya madini nchini ili kubaini
leseni ambazo zinatumika kuendesha utapeli na zifutwe nchi nzima .
Mambo
mengine ambayo wanapendekeza ni kuongeza udhibiti wa vibali vya kuuza
madini nje ya nchi na baada ya madini kusafirishwa vibali vilivyotolewa
kurejeshwa wizarani badala ya wafanyabiashara kukaa navyo wakaendelea
kuvitumia kuvusha madini kinyemela.
“Wizara
inatakiwa kuunda kikosi kazi cha kushughulikia na kupambana na vitendo
vya utapeli na biashara haramu ya madini nchini. Inapendekezwa kuwa
kikosi kazi hicho kiundwe na maaafisa sita ambao ni maafisa wa ngazi ya
juu kutoka Jeshi la Polisi (2), Idara ya Madini (2), Mamlaka ya Mapato
(TRA - 1) na TMAA (1). Wizara iliwahi kuunda kikosi kazi kama hicho
kipindi cha nyuma ila kikafa kifo cha asili,” inasema sehemu ya waraka
ambao JAMHURI imeuona.
Wanapendekeza
pia kuimarisha uwazi katika biashara ya madini kwa wizara kutoa taarifa
za majina na anwani za wafanyabiashara halali wa madini nchini kwenye
tovuti ya wizara na ile ya TMAA. Taarifa hiyo ifafanue kwa kina
utaratibu utakaotumika kufutwa kwa leseni za watu wanaogeuka kuwa
matapeli na taratibu za wanunuzi wa madini nchini kununua na kusafirisha
nje ya nchi.
Hatua
hiyo itasaidia kupunguza utapeli na udanganyifu katika biashara ya
madini nchini. Wanapendekeza kuwa taarifa hiyo inaweza kusambazwa kwenye
vituo vya biashara vilivyoko nje ya nchi.
Hatua
nyingine ni serikali kupitia Idara ya Forodha , Jeshi la Polisi Idara
ya Madini na TMAA kuimarisha usimamizi na ukaguzi wa madini katika
viwanja vikubwa vya ndege nchini vya Kilimanjaro na Julius Nyerere
International Airport, bila kusahau njia kuu za mipaka ya nchi ili
kudhibiti vitendo vya utapeli na biashara haramu ya madini.
Kubwa
zaidi wizara imependekeza kuanzisha mfumo wa kutoa motisha mahsusi kwa
raia wema watakatoa taarifa sahihi kwa biashara haramu ya madini kwa
kuwalipa asilimia 40 ya thamani ya madini yatakayokamatwa.
Mtoa habari wa JAMHURI
amesema ikiwa mapendekezo hayo na mengine yatapita, heshima ya Tanzania
itarejea enzi za Mwalimu Nyerere ambapo hakuna Mtanzania aliyethubutu
kufanya utapeli wa aina hiyo kwani alijua fika kuwa mkono wa dola
ungeweza kumnasa muda wowote na mahala popote.
SOURCE: JAMUHURIMEDIA.CO.TZ
|
TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO