Habari hii imeishapita, ila ni kujikumbusha jinsi hawa M23 walivyo funga virago
Sasa
ni wazi kwamba waasi wa kundi la March 23 (M23), wamelewa kiasi cha
kuomba mapambano yasimamishwe ili mazungumzo ya kuleta amani yaweze
kutekelezwa. M23
wamelazimika kurudi nyuma baada ya kupigwa na Majeshi ya Umoja wa
Mataifa (FIB) yanayoongozwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ). Kuna taarifa kuwa kwenye mapambano hayo, FIB waliwanasa waasi
zaidi ya 1,000 na kuwanyang’anya silaha mbalimbali.
Habari kutoka kwenye uwanja wa mapambano zinasema M23 wamepoteza
mwelekeo na kukimbia kutoka kwenye ngome zao ambazo wamezishikilia kwa
muda mrefu. “Hivi
sasa tuko katika kambi yao na tunawashikilia waasi zaidi ya 1,000
wengine wamekimbia, wametawanyika wengine wako msituni hawajui nini cha
kufanya,” kimesema chanzo chetu kutoka Goma.
Mapigano
makali yalitokea Agosti 21 hadi Agosti 24 katika vijiji vya Mutaho na
Kibati umbali wa kilometa zaidi ya 20 kutoka Goma. Mapigano hayo makali
yaliibuka baada ya kuuawa kwa Meja Khatibu Shaaban Mshindo wa JWTZ na
kujeruhiwa kwa wanajeshi wengine wengine.
Ofisa
huyo amesema kwamba tukio hilo liliwakasirisha mno wanajeshi wa
JWTZ. “Kuuawa kwa Meja Mshindo kulifanya kila askari wa Tanzania na
wenzetu kutoka nchi mbalimbali zinazoshiriki katika Majeshi ya MUNUSCO
wawe na hasira,” amesema.
“Kifo
cha Meja Mshindo kilitupa hasira na nguvu za ajabu, hawana hamu tena,
nahisi huko waliko wanajuta. Hapa Goma pia katika ngome yao kuu mambo ni
kimya kabisa, hakuna kelele za bunduki wala nini, wananchi wanafurahi,”
amesema.
Meja
Mshindo aliyefariki dunia Agosti 28, mwaka huu, baada ya kujeruhiwa kwa
bomu, alizikwa kwa heshima zote nyumbani kwao katika Kijiji cha
Mangapwani, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa Kaskazini Unguja. Alizaliwa
Septemba 29, 1972 na kujiunga na JWTZ Machi 1995 na kutunukiwa heshima
ya kamisheni Mei 17, 1997.
Kinachoendelea Goma
Habari
kutoka Goma zinasema majeshi ya FIB kwa sasa yanasubiri hatima ya
mazungumzo yaliyotarajiwa kuanza mjini Kampala, jana. “Kwa hali ilivyo
sijui kama watafikia makubaliano, waasi wana msimamo wao, na Serikali ya
DRC ina msimamo wake, sijui kama wataafikiana. “Mama Mary Robinson
(Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa), ametangaza msimamo
mkali. Kasema hata kama kutafikiwa makubaliano ya kumaliza mapigano,
wahusika wa M23 na vikundi vingine waliofanya maovu ni lazima wafikishwe
kwenye vyombo vya kisheria vya kimataifa. Kasema wazi hakuna
kusameheana. Baada ya makubaliano wahusika watakamatwa.
“Msimamo
huo umewafanya wengi waone kuwa suala la kufikia makubaliano ya
kumaliza mapigano litakuwa gumu, lakini ukweli ndiyo huo,” kimesema
chanzo chetu kutoka Goma.
Chanzo hicho kimethibitisha kuwa M23 kwa sasa wamekimbia. Anasema walikabiliwa na wakati mgumu baada ya kumuua Meja Mshindo.
“Tuliingizwa
kwa nguvu na M23 wenyewe, sisi hapa hatupo kivita, tupo kuwanyang’anya
silaha, lakini inapotokea tumeshambuliwa ni lazima tujihami,” amesema na
kuongeza:
“Baada
ya jamaa kuona hali imekuwa mbaya (kipigo kimewalemea) wakaamua
ku-withdraw (kurudi nyuma), walishtuka kuwa wakifanya masihara
tutawamaliza. Tulifika mahali tukasema enough is enough (imetosha),”
amesema.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge
Hadi
tunakwenda mitamboni, kamati mbili za kudumu za Bunge za Ulinzi na
Usalama, na Mambo ya Nje zilikuwa zimetakiwa zikutane jijini Dar es
Salaam jana. Kamati hizo zilitakiwa zikutane Jumatatu saa 3 asubuhi
katika Ofisi Ndogo za Bunge jijini humo. Mkutano huo ulitarajiwa kuwa wa
siku tatu. Haikuwekwa wazi dondoo za mkutano huo, lakini wafuatiliaji
wa masuala ya kisiasa wamedokeza kuwa huenda suala la majeshi ya
Tanzania nchini DRC na kulegalega kwa utangamano miongoni mwa nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni mambo yaliyopewa
kipaumbele.
“Wajumbe
wote wa kamati hizi mbili tumetakiwa tuwe Dar es Salaam kuanzia
Jumatatu bila kukosa. Tumesisitiziwa sana, inaelekea kuna mambo mazito,”
amesema mmoja wa wajumbe wa kamati hizo.
Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama inaongozwa na Mbunge wa Viti
Maalumu, Anna Abdallah; ilhali ile ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa inaongozwa na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.
Source: Jamuhurimedia.co.tz
|