Na Mwandishi wetu, Mwananchi
Posted Jumapili,Oktoba13 2013 saa 11:13 AM
Posted Jumapili,Oktoba13 2013 saa 11:13 AM
Kwa ufupi
“Afrika ina viongozi wengi wazuri, lakini pia
tusifiche ukweli kwamba tunao viongozi wa ovyo, ambao wanadhani ni (semi
gods) nusu miungu. Wangependa kila kitu kiwe chao tu.
Addis Ababa. Muungano wa Afrika (AU) umeitaka
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kusitisha kesi dhidi ya wakuu wa
nchi walioko madarakani kwa sasa hadi watakapomaliza vipindi vya uongozi
wao.
Viongozi walioko madarakani kwa sasa ambao
wanakabiliwa na kesi kwenye mahakama hiyo ni Rais Uhuru Kenyatta wa
Kenya na makamu wake, William Ruto wanaotuhumiwa kwa makosa ya
uchochezi, mauaji na uhalifu dhidi ya ubinadamu baada ya uchaguzi mkuu
wa mwaka 2007.
Mwingine ni Rais wa Sudan, Omar al-Bashir ambaye
mahakama hiyo imetoa hati ya kukamatwa kwake akihusishwa na matumizi
mabaya ya madaraka kwa kuamrisha mauaji ya watu kwenye eneo la Darfur
nchini kwake.
Msimamo huo umefikiwa baada ya kikao cha wakuu wa
nchi mjini Addis Ababa jana, kilichozima shinikizo la kutaka nchi
wanachama wa umoja huo zilizo wanachama wa mkataba wa Roma ulioianzisha
mahakama ya ICC mwaka 2002 zijitoe.
Msimamo huo uliosababisha kuitishwa kwa kikao
maalumu cha dharura cha AU ilichofanyika juzi na jana ulipingwa vikali
na viongozi mbalimbali duniani, akiwemo Jaji Mtanzania aliyeapishwa wiki
hii kuwa Jaji wa ICC, Jaji Stephen Bwana ambaye alisema ICC ni wembe
kwa viongozi wanaojifanya miungu watu.
“Afrika ina viongozi wengi wazuri, lakini pia
tusifiche ukweli kwamba tunao viongozi wa ovyo, ambao wanadhani ni (semi
gods) nusu miungu. Wangependa kila kitu kiwe chao tu. Sasa tukisema
kwamba nchi zote za Afrika zijiondoe ICC, tunataka kusema kwamba
hatufanyi makosa.”
Jaji Bwana ambaye aliapishwa rasmi wiki hii kuwa
Jaji wa ICC nchini Cambodia aliongeza kwamba, viongozi hao ‘miungu watu’
wamezifanya taasisi za utoaji haki kwenye nchi zao kuwa dhaifu na
kwamba kwa hali hiyo hawawezi kushtakiwa katika mahakama za nchi zao kwa
makosa wanayoyafanya.
Viongozi wengine maarufu duniani waliopinga hatua
hiyo ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (AU) Kofi Annan ambaye
alisema Afrika itaingia kwenye ‘dimbwi la aibu’ na Askofu Desmond Tutu
wa Afrika Kusini ambaye alisema viongozi wanaotaka nchi zao zijitoe
wanataka kujihalalishia “uuaji uliotukuka”.
Akizungumzia uamuzi wa mkutano huo wa wakuu wan
chi jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Tedros Adhanom Ghebreyesus
alisema uamuzi uliofikiwa ni wa kuitaka mahakama hiyo kutowakamata na
kuwashtaki viongozi walipo madarakani.
Alisema wakuu wa AU wamekubaliana kuiandikia ICC
na kuitaka kusitisha kesi dhidi ya Rais Kenyatta, makamu wake William
Ruto na hati ya kukamatwa kwa Rais Bashir kwa sasa.
Tedros ambaye ndiye mwenyekiti wa Baraza Kuu la AU
kwa sasa, alisema ICC imeonesha wazi kwamba imejigeuza kuwa chombo cha
kisiasa kinacholenga kuiyumbisha Afrika na Waafrika, suala ambalo
haliwezi kukubalika. Alisema kutokana na hali hiyo, ICC imeshindwa
kutilia maanani maombi ya awali ya AU, hivyo suala hilo kwa sasa
litapelekwa kwenye hatua nyingine.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI