Kwa ufupi
“Namkumbuka aliyenipiga risasi alikuwa
amevaa sare za polisi,” alisema Adam mwanafunzi katika Shule ya Msingi
Levolosi huku akitokwa machozi.
Arusha/Dodoma. Wakati watu waliofariki kwenye tukio la kurushwa
bomu katika mkutano wa Chadema ikifikia watatu baada ya jana kufariki
kwa mtoto Amir Ally (7), mtoto mwingine wa miaka kumi na moja
aliyejeruhiwa, amedai kwamba alipigwa risasi na polisi kwenye tukio
hilo.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe naye ametoa
tamko kuwa chama chake kina ushahidi wa kutosha wa watu waliohusika na
tukio la kurushwa bomu katika mkutano wa kampeni wa chama hicho.
Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Arusha Medical
Lutheran Center (ALMC), Dk Paul Kisanga alisema jana kuwa, Amir
alifariki jana asubuhi baada ya kupata majeraha makubwa kichwani
yaliyodhuru ubongo wake.
Dk Kisanga alisema huyo ni mmoja wa watoto watano,
waliojeruhiwa wakati wakitoka madrasa huko Kaloleni, jirani na Uwanja
wa Soweto kulipokuwa na mkutano na alifariki jana asubuhi hospitalini
hapo.
Alisema watoto wengine wawili ambao ni ndugu;
Fatuma na Sharifa Jumanne wamepelekwa Nairobi kwa matibabu zaidi baada
ya miili yao kukutwa na vyuma. Dk Kisanga aliwataja watoto wengine
waliojeruhiwa kuwa ni Fahad Jamal (7) ambaye yupo ICU akisubiri timu ya
madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na hali
yake kutoruhusu kusafirishwa. Pia yupo Abubakar Adam (11) ambaye
amejeruhiwa mguuni na amelazwa katika Hospitali ya Mkoa, Mount Meru.
Mtoto aeleza kupigwa risasi
Adam alisema jana kuwa alipigwa risasi na mtu
aliyekuwa amevalia sare za polisi, wakati akitoka madrasa akiwa na ndugu
yake, Fahdi katika eneo la Soweto.
Alisema akiwa njiani, aliona watu wakimkimbiza mtu na ghafla alishangaa kupigwa risasi na kuanguka chini.
“Namkumbuka aliyenipiga risasi alikuwa amevaa sare
za polisi,” alisema Adam mwanafunzi katika Shule ya Msingi Levolosi
huku akitokwa machozi.
Muuguzi wa zamu, katika katika wodi ya watoto
katika Hospitali ya Mount Meru, Asha Semdeli alisema jana kuwa mtoto
huyo ana vyuma viwili katika mguu wake.
“Tunasubiri afanyiwe upasuaji kwani tayari mashine
ya X-ray inaonyesha vyuma kuwepo katika mguu wa Adam siwezi kusema ni
risasi au la,” alisema Semdeli.
Polisi wazungumzia risasi
Mkuu wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Polisi,
Kamishna Isaya Mngulu alisema hakuwa na taarifa za watu kufa na
kujeruhiwa na polisi kwa risasi. Hata hivyo, alikiri kuwa wameokota
maganda ya risasi, ambayo wanafanyia uchunguzi.
“Ni kweli tulikuta maganda ya risasi kwenye tukio
lakini ni vigumu kusema kama polisi ndio walipiga bunduki. Nadhani ni
mapema mno kwani bado tuko kwenye uchunguzi,” alisema Mngulu, ambaye
yumo katika timu iliyoteuliwa na Mkuu wa Polisi (IGP), Said Mwema
kuchunguza tukio hilo.
Lakini, Kamanda wa Polisi wa Arusha, Liberatus
Sabas alisema hana taarifa ya watu kupigwa risasi... “Mimi sijui lolote
kuhusu watu kupigwa risasi. Naomba usiniulize mambo ya ajabu ajabu,”
alijibu kwa ukali na kukata simu alipoulizwa juu madai hayo ya polisi
kutumia risasi za moto.
Majeruhi mwingine
Majeruhi mwingine, Abdallah Hilali (39),
aliyelazwa katika Hospitali ya Arusha Lutheran Center, amedai kuwa
majeraha aliyopata miguuni yametokana na kupigwa risasi na polisi na
kudondokewa na vipande vya bomu.
Alisema alikuwa nyuma ya jukwaa kuu akimsikiliza
Mbowe na alipomaliza kuhutubia alishuka jukwaani kukusanya sadaka, ndipo
alipoona mfuko wa mweusi mdogo wa plastiki ukipeperuka juu.
“Nilidhani ni upepo unapeperusha kitu, lakini
ghafla nilisikia kishindo na nikamsikia mama mmoja akipiga kelele kuwa
aliyerusha mfuko anakimbia, nilipogeuka nikajikuta nipo chini,” alisema
Hilali.
Alisema alipokuwa anaangalia aliona kijana mmoja
amekaribia kumfikia aliyerusha bomu lakini ghafla akapigwa risasi na
kuanguka chini na aliyekuwa anafuatia kwa nyuma naye akapigwa risasi
akaona anaruka na kudondoka chini huku damu zikivuja.
“Lakini mwisho wa yote kijana aliyerusha hilo fuko
aliingia kwenye gari na kuondoka kwa kasi. Mimi nilikuwa chini,”
alisema Hilal mbele ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu, alipotembelea majeruhi hospitalini hapo.
Jana, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda walitembelea majeruhi waliolazwa katika
hospitali mbalimbali za Arusha.
Mbowe tunawajua watuhumiwa
Mbowe amedai kuwa wamewagundua watu waliohusika na urushaji wa
mabomu katika Viwanja vya Soweto Juni 15, mwaka huu na kusababisha vifo
vya watu watatu na majeruhi zaidi ya 60.
Akizungumza jana baada ya kutembelea majeruhi
katika Hospitali ya Seliani, Mbowe alisema Chadema tayari imewajua
wahusika wakuu wa mabomu hayo kwa ushahidi wa picha. Alidai kuwa ni
askari mmoja wa Kikosi cha Polisi wa Kuzuia Fujo (FFU).
Alidai kuwa ushahidi huo unaonyesha kuwa wakati
askari huyo akirusha bomu, alikuwa na kofia inayofanana na ile
inayotumiwa na Polisi na mara baada ya kurusha bomu na risasi za
mfululizo alikimbilia kwenye gari aina ya Land Cruiser na kusindikizwa
na Polisi.
“Duniani hakuna siri yoyote ile. Tumeshafanikiwa
kugundua chanzo kikubwa na ushahidi unaonyesha wahusika ni polisi.
Ushahidi huu tutauweka hadharani na kila mwanadamu aweze kujionea kwa
kuwa waliokufa hawana hatia yoyote na sisi tumechoka kila siku kuonewa
na Polisi,” alisema.
Aidha, Mbowe amepinga kauli ya Spika wa Bunge,
Anne Makinda na ile ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge,
Uratibu na Sera), William Lukuvi kuwa Arusha inaharibiwa na wanasiasa
pamoja na asasi binafsi.
Nape aituhumu Chadema
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
amekituhumu Chadema kuwa ndicho kilichofanya mpango wa kulipua bomu
lililosababisha vifo vya watu watatu jijini Arusha baada ya kubaini kuwa
kitashindwa katika uchaguzi wa udiwani katika kata nne.
Amedai kuwa mpango huo ulipangwa na Chadema baada
ya wananchi wa Arusha kuapa kutokichagua tena kutokana na kuchoshwa na
kauli za viongozi wake zinazochochea maandamano na vurugu, jijini humo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dodoma jana,
Nape alisema Chadema kinatakiwa kuacha kutafuta umaarufu kwa mtindo wa
kumwaga damu za Watanzania na kwamba juhudi hizo zinatakiwa kulaaniwa
vikali.
Alipoulizwa sababu za kukitaja Chadema kuwa
kinahusika moja kwa moja licha ya kuwa uchunguzi wa awali uliofanywa na
Jeshi la Polisi umeonyesha kuwa mazingira ya tukio hilo yanafanana na
lile la kanisani alisema, “Tunasema hivyo kutokana na kauli zilizokuwa
zikitolewa na viongozi wa Chadema kabla ya tukio na walipanga ndani ya
chama chao ili uchaguzi usifanyike.”
Mamia wakusanyika Soweto
Mamia ya wananchi jana walikusanyika katika Viwanja vya Soweto ulikotokea mlipuko huo, kwa ajili ya kuomboleza
Mazishi ya waathirika wa tukio hilo yanatarajiwa
kufanyika mara baada ya uchunguzi wa madaktari kukamilika na miili
itaagwa katika eneo hilo kabla ya kusafirishwa katika maeneo yao ya
asili. Mwili wa Judith Moshi utasafirishwa kwenda Kilimanjaro, Ramadhan
Juma (Tabora) na wa Amir utapelekwa Lushoto.
Mlipuko huo ulitokea juzi wakati Chadema,
kilipokuwa kikihitimisha kampeni zake za udiwani na kusababisha
kuahirishwa kwa uchaguzi katika kata za Themi, Kaloleni, Elerai na
Kimandolu hadi Juni 30.
Marekani yalaani
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso
Lenhardt ameshutumu vikali mlipuko wa bomu kwenye mkutano huo wa kampeni
wa Chadema Arusha ambao ulisababisha vifo vya watu watatu na wengine
zaidi ya 60 kujeruhiwa.
Balozi Lenhardt ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizofiwa na kutoa pole kwa wale walioumia.
“Tunaomba vyombo vya dola kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kushtakiwa,” alieleza Balozi huyo katika taarifa yake.
chanzo: Mwananchi
chanzo: Mwananchi