Singo Kigaila.
Huku kukiwa na madai kuwa Chadema
inahusika na matukio ya kula njama za utekaji na kuteka, kupiga na kuua
watu, chama hicho kimekuja juu na kukanusha madai hayo.
Pamoja na kukanusha, kimemwomba Rais Jakaya Kikwete aunde tume huru ya kimahakama kuchunguza matukio yaliyotokea ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote watakaobainika kuhusika.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni wa chama hicho, Singo Kigaila, alisema walishamwomba Rais aunde Tume lakini akadai ombi hilo halijatekelezwa hadi sasa.
Mkurugenzi wa Usalama wa Chama hicho, Wilfred Lwakatare anashitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam kwa madai ya kula njama za kumdhuru Mhariri Mtendaji wa Mwananchi, Dennis Msacky.
Kigaila alisema kuna wanachama wa vyama vingine vya siasa wamekuwa wakipita katika kampeni ya uchaguzi zinazoendelea Nachingwea, Lindi wakikituhumu chama hicho kuhusika na mauaji.
Alitaja baadhi ya matukio hayo, kuwa ni pamoja na kuuawa kwa Yohana Mpinga kwenye vurugu za Ndago, Singida; kumwagiwa tindikali kwa kijana Musa wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo Igunga, Tabora na kuuawa kwa Mwandishi wa Habari wa Channel Ten, Daud Mwangosi.
Pia matukio ya kutekwa na kupigwa kwa Mwenyekiti wa Jumuia ya Madaktari, Steven Ulimboka na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda.
Kigaila alisema upo ushahidi wa kuwapo ushirika wa baadhi ya watumishi wa vyombo vya Dola waliopewa mafunzo ya kuua na kutumia silaha, tindikali, kutesa, kuteka, kuumiza na hata namna ya kutumia sindano kuua kwa sumu.
Alidai kuwa mara kadhaa wamekuwa wakitoa ushahidi wa silaha zinazomilikiwa na CCM, ambazo zimepelekwa katika kambi za Ulemo, Singida; Nzega na Uyui baada ya kuingizwa nchini bila kibali.
"Tunamtaka Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama atwambie ni nani alitoa ruhusa kwa CCM kuwa na kikundi cha kijeshi na kumiliki silaha ambazo zimekuwa zikitumiwa na vijana wake kudhuru watu," alihoji.
Kigaila alitoa madai hayo, huku uchunguzi uliofanywa na kamati iliyoundwa na TEF na Baraza la Habari Tanzania (MCT), ukionesha kuwa baadhi ya waliohojiwa walidai kuwa Chadema imepewa mafunzo maalumu kutoka nje ya jinsi ya kutesa watu na hata kuwaua na kusingizia vyombo vya Dola kuwa vinahusika.
Walisema hilo linafanywa makusudi ili kuonesha kuwa Serikali imeshindwa kulinda watu wake na hivyo wananchi waichukie na kuiondoa madarakani.