Dar es Salaam/Dodoma: Mapendekezo yaliyotolewa katika Rasimu ya Katiba Mpya na Tume ya Marekebisho ya Katiba yamewavuruga wanasiasa ambao tayari walikuwa wamejipanga kwa ajili ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Mwananchi limebaini.
Tangu juzi Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph
Warioba alipotangaza rasimu hiyo, kumekuwa na wasiwasi mkubwa sasa
kwamba mipango ya urais wa 2015 itavurugika ikiwa mapendekezo hayo
yatapitishwa.
Tishio kubwa katika rasimu hiyo ni pendekezo la
kuwapo kwa Serikali ya tatu hali ambayo inatafsiriwa na baadhi ya
wanasiasa kwamba inaondoa nguvu ya Rais yeyote; awe wa Jamhuri ya
Muungano, Zanzibar au Tanzania Bara.
Habari za kuaminika zilizopatikana kutoka ndani ya
kambi za vyama vya CCM na Chadema zinaeleza kuwa wale waliokuwa
wakifikiria kuwania nafasi hiyo wameingiwa na wasiwasi.
Kadhalika, suala la umri wa kuwania urais kubakia
miaka 40 pia linaonekana kuwagusa waliowahi kutangaza kutaka nafasi hiyo
ya juu ya uongozi wa nchi kabla ya mapendekezo ya tume.
Katika suala la urais, wanasiasa wenye nia hiyo
wanauona uongozi wa Jamhuri ya Muungano kuwa ni kama hauna nguvu tena
kutokana na kushughulikia mambo machache, lakini wakati huohuo wanauona
urais wa Tanzania Bara kwamba hauna mamlaka kamili ya kuwawezesha
watambuliwe nje ya nchi.
Tume ya Marekebisho ya Katiba imependekeza mambo
saba tu yawemo chini ya Serikali ya Muungano kati ya 22 ya sasa.
Yanayopendekezwa ni Ulinzi na Usalama, Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya
Muungano, mambo ya nje, sarafu na Benki Kuu, uraia na uhamiaji, usajili
wa vyama vya siasa, ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo
na Muungano.
Ndani ya CCM
Makundi mbalimbali yanayowania urais ndani ya CCM inaaminika hayajafurahishwa na mapendekezo ya rasimu ya kutaka Serikali tatu.
Kwa maneno mengine, wanaona kama Rais wa Muungano
ameng’olewa baadhi ya meno na masuala mengi yatakuwa yanashughulikiwa na
Serikali ya Tanzania Bara na ile ya Zanzibar.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel
Sitta amesema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeliacha hewani suala la
Tanganyika hasa baada ya kutoa mapendekezo ya Serikali tatu kwenye
Rasimu ya Katiba.
Sitta ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM),
alisema hakuna mantiki ya kuunda Serikali tatu ikiwa Tume haikutoa
mwongozo wa hali itakavyokuwa kwa Tanzania Bara, Serikali ya Muungano na
ile ya Zanzibar.
“Ukiangalia kwa haraka, hivi Serikali ya Tanganyika itakuwaje?
Bunge la Tanganyika litakuwa la namna gani na utaratibu gani utatumika
kupata wabunge?” alisema Sitta kwenye Viwanja vya Bunge, Dodoma jana.
Pia, Sitta aliyewahi kujipambanua kuwa atawania
urais 2015 na hata kutaja kundi la muungano wa marafiki zake, alisema
Tume pia haikuweka wazi utawala utakavyokuwa ndani ya Serikali tatu.
“Hivi viongozi wa Tanzania Bara na Zanzibar na wao
wataitwa marais! Wapi duniani imeshatokea nchi moja ikawa na marais
watatu? Hii haijawahi kutokea, na Tume inatakiwa kuweka sawa katika
uongozi hasa ngazi ya Rais wa kuongoza hapa,” alisema Sitta.
Alipinga mpango uliopendekezwa wa wabunge
kuchaguliwa wawiliwawili akionya kuwa utasababisha matatizo kwa kuwa
Tume haijaweka wazi njia za kuwapata.
MwanaCCM mwingine ambaye ni miongoni mwa watu
wanaotajwatajwa kuwania urais 2015 alikaririwa akisema: “Hivi kweli Mzee
Warioba kweli anataka kututengenezea Mikhail Gorbachev (Rais wa zamani
wa Urusi) hapa Tanzania? Hatutakubali!” Alikuwa akimfananisha Rais
ajaye, ambaye atatokana na rasimu hiyo na Rais wa zamani wa Urusi,
Gorbachev, ambaye mwaka 1991 alipoteza mamlaka yake baada ya kutoa
madaraka ya ndani kwa nchi 14 zilizokuwa zinaundwa Muungano na baadaye
zikajitangazia uhuru jambo ambalo kiongozi huyo alishindwa kulizua.
Pia watu wa karibu na mgombea huyo wanaamini kuwa kukubaliana na pendekezo la Serikali tatu ni sawa na kuvunja Muungano.
“Tunatakiwa kwenda Serikali moja na siyo kurudi
Serikali tatu ukizingatia sasa ni miaka 50 tangu Tanganyika na Zanzibar
ziungane. Hatuungi mkono suala hili kwani haliutakii mema Muungano.”
Katika siku za karibuni, joto la kuwania urais wa
Tanzania lilianza kupamba moto baada ya kuibuka habari kuwa suala la
kuwania urais lilijadiliwa wakati Rais Kikwete alipokutana na wabunge wa
CCM.
Habari za ndani kutoka katika mkutano huo
zilieleza kuwa Rais Kikwete alishauri kuwa haikuwa dhambi kujipanga
kuwania urais mwaka 2015 lakini alionya kufanya hivyo kusiathiri umoja
wa CCM.
Mtu mwingine, ambaye yuko karibu na kati ya watu
wanaotamani urais kupitia CCM, alisema: “Hii rasimu ngumu, ila tukiona
mambo siyo mazuri kwenye Muungano tutajitosa kwenye uchaguzi wa Rais wa
Tanzania Bara.”
Chadema
Rasimu pia imegusa harakati za kuwania urais kupitia Chadema
hasa ikizingatiwa kwamba mmoja wa makada wake, Zitto Kabwe alishatangaza
dhamira yake mapema.
Kama rasimu hiyo itapitishwa na kuwa Katiba, Zitto atajikuta anakwama kwani imependekezwa miaka ya kugombea urais ianzie 40.
“Ila watu wengi wanafikiri Zitto amekwama ila
jamani kuna Katiba ya Tanzania Bara inaweza kuwa tofauti na umri kuwa
chini zaidi,” alieleza mtu wa karibu na Zitto.
Bila shaka hali hiyo itakuwa heri kwa wale
wanaomuunga mkono Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa ambaye
alikuwa anatarajiwa kukabiliana na Zitto kuwania tiketi ya kugombea
urais kupitia chama hicho.
Wabunge wapinga
Mbunge Peter Serukamba, Kigoma Mjini (CCM) ameonya
kuwa kubadili muundo wa Serikali ni gharama kubwa na kuhoji kutakuwa na
marais wangapi?
“Muundo mzima ni gharama na tutatumia hadi fedha
za maendeleo ya wananchi kuendesha Serikali ya Katiba mpya. Mimi binafsi
napingana na hili, nataka Serikali mbili,” alisema.
Kwa upande wake, Maua Daftari, Viti Maalumu (CCM)
alisema mfumo wa Serikali tatu uliopendekezwa ukipita itakuwa hasara
kubwa kwa Wazanzibari.
“Kwa mtazamo wangu, kwa Zanzibar bado sana kuweza
kusimama kwa miguu yake na wakati huohuo kuchangia katika Serikali ya
Muungano,” alisema Daftari, ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa
Mawasiliano na Uchukuzi kwenye Serikali ya Muungano.
Mbunge mwingine kutoka Zanzibar, Mariam Msabaha,
Viti Maalumu, (Chadema), alisema chuki za watu na uroho wa madaraka kwa
watu wachache unaweza kuwa ndiyo sababu ya kupendekezwa kwa mfumo huo.