NAFASI YA VIJANA WASOMI WA TANZANIA NA KATIBA MPYA
(RASIMU YA KATIBA) KWENYE MAENDELEO YA TANZANIA
Na
Mwalimu Azaveli Lwaitama
+255784432696
Ndugu Watanzania mliokusanyika hapa Oslo leo
Ndugu marafiki wa Wantanzania mlipo katika sherehe
hii,
Kwanza naomba
niwashukuru kwa kunipa mwaliko wakuhudhuria sherehe yenu bila kuchangia
chochote. Nasikitika na naomba
kusamehewa kwa kukosa kuwepo uso kwa uso ingawa hotuba hii inawaonesha nipo
nanyi kiroho. Nasikitika kukosa kuwepo
uso kwa uso maana niliambiwa kutakuwepo chakula kingi na vinyaji vya kutosha na
mimi kwa msosi ndio mwenyewe, bia na
mvinyo pia nakunywa ingawa hulewa mapema
na kuanza kusinzisinzia.
Nasikitika
kuukosa uhondo wa mapochopocho, ulaji na kinywaji. Nawashukuru Kwa dhati
kunialika hata kama nimeshindwa kufika. Nimeshindwa kufika kwa kuwa naondoka kesho Jumapili asubuhi sana na inabidi, kama mnavyojua, niwe kiwanjani walau saa 10 usiku
wa leo hii Jumamosi ( ingwa kwa Kimombo tunasema saa 10 asubuhi ya Kesho Jumapili!). Na masikini baba yake mwenyeji wangu alipata
udhuru na kushindwa kupata muda wa kuweza kunileta hadi huku jijini Oslo halafu
aniendeshe kwa gari lake binafsi kurudi karibu mwendo wa zaidi ya saa na zaidi
usiku wa manane kunipeleka uwanja wa ndege wa Gardermoen, Oslo ambao upo kati
kati ya huku jijini Oslo na huko kwao nilikokaribishwa kwenye mji mdogo wa HAMAR.
Ndugu Watanzania wenzangu ,
Ndugu marafiki wa Wantanzania,
Kwa kweli
ingebidi aondoke kwao Hamar saa 2 hivi
usiku na kunileta huku Oslo jijini ili nifike hapa kwenye saa 4 halafu anirudishe nusu mwendo wa kurudi kwao
na kuniacha uwanja wa ndege wa Gardermoen, Oslo usiku wa manane na ende kwao Hamar na kufika pia usiku wa
manane.. Hata na mimi nilikubali ingewa si uungwana kumwambia kunifanyia hisani
kiasi hicho. Yeye ni baba yake Dr
AnnaMartha van Grieken ambaye alikuwa mwanafunzi wangu wa shahada ya uzamivu (PhD)
aliyoipata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
miaka mitano iliyopita. Aliniomba nimtembelee katika shule anayofundisha ya
Sekondari ya Juu (Upper Secondary School) ambayo nimeizungumzia katika makala
yangu iliyochapishwa katika gazeti la kila siku la The Citizen Juamatano hii ya
juzi tarehe 05.06.2013.
Ni moyo wa
ukarimu wa mwanafunzi wangu wa shahada
ya uzamivu (PhD) wa zamani ulionipa fursa kutembelea shule za chekeche, msingi
na sekondari hapa Norway ili kujifunza mengi iwezekanavyo kuhusu mfumo wa elimu
katika nchi ya Norway kwa lengo la
baadaye kusambaza elimu hiyo niliyopata
kwa Watanzania wenzangu kupitia machapisho kama ile makala yangu kwenye gazeti la The Citizen juzi Juamatano. Nitaendelea
kutoa machapisho na kuzungumza juu ya niliyojifunza kuhusu Norway nikirudi
Tanzania.
Ndugu Watanzania
Kwa wale ambao
wanapenda kuendelea kuchota kutoka kwenye elimu
niliyopata hapa Norway kwa muda
wa wiki moja nawakaribisha
kufuatilia juu ya nitakachokuwa
kuandika (naandika) na kuzungumza kwa kutafuta jina langu kwenye Googles na au
kutafuta nilichoandika kwenye The
Citizen Tanzania kila Jumatano au
kusikiliza kwenye Youtube kipindi changu cha kila Ijumaa kiitwacho Hoja ya
Mwalimu Lwaitama kinachorushwa na SIBUKA
Tv na Radio ambayo inasikia kwa kingamuzi sehemu nyingi Tanzania.
Nyie pia
nawaomba mfanye bidii kwenye masomo yaliyowaleta hapa na kurudi nyumbani na
maarifa na stadi za ujuzi mbali mbali
wenye kusaidia watu wetu kule nyumbani Tanzania wafanye kazi zao za kila
siku kwa tija. Hata wale mtakaojikuta
mmezamia hapa kwa kuoa au kuolewa hapa mimi sina matatizo na nyie ili mradi
kukaa kwenu hapa kunafanywa kuwa kwa manufaa kwa ndugu zenu waliobaki nyumbani.
Muhimu kuliko chochote soma kwa bidii na jifunze yote mazuri yaliyopo mbele
yako hapa ili uwe mtu mwelevu zaidi na ambaye unapata heshima ya kujitambulisha
kama mweledi wa mambo katika fani yako yoyote ile.
Ndugu Watanzania mliokusanyika
Chonde chonde
mtu hasitoke hapa na dhana kuwa ili kujinasua na umasikini wake kama mtu binafsi sherti kujikomba kwa wana
siasa ili wakupe vyeo vya kisiasa vya kuteuliwa au kupigiwa kura na watu ulio
waonga vijikanga na na (imerudiwa) vijichumvi! Hapana jamani!!
Ndugu Watanzania wenzangu,
Toka hapa na weledi wa juu katika fani yako ili
waajiri wakutafute popote duniani ili wakuajiri katika fani yako uliyosomea.
Toka hapa na jeuri yenye unyenyekevu itokanayo na kujiamini kuwa yapo mambo
unayoyajua na watu mwisho wa siku
watakutafuta au ukiwaonesha unachoweza
watakuajiri au kukupa kazi kwa vile wewe ni mjuzi wa mambo katika fani
yako! Chonde chonde toka hapa na ujuzi fulani utakao
kukomboa na utumwa wa daima kujikomba kwa wana siasa, wawe wa chama tawala au
wa vyama vya ushindani!!!. Ukitaka kujiunga na vyama vya siasa basi jiunge huku
viongozi wao wakijua kuwa kuishi kwako hakutegemei hisani zao, ng’o!!!
Sasa ngoja nimalize salamu zangu kwenu kwa kugusia juu ya mada
niliyoelezwa mlitaka nizungumzie leo.
Tume ya Rais ya Mchakato wa Kuandika Katiba Mpya, Tume ya Jaji Warioba, imetoa Rasimu ya
Katiba hiyo Mpya na niliombwa nizunguzie juu ya nafasi ya vijana wasomi wa
Tanzania na katiba Mpya katika maendeleo ya Tanzania. Hii ni mada pana lakini nitafupisha maneno kwa kusema mambo matatu
yafuatayo.
Kwanza, kama vijana wasomi hoji kila kitu kwa kunukuu matokea ya utafiti na
ushaidi wakujenga hoja na jiepushe na
tabia ya kukubalina na kila kitu kisemwacho
na wakubwa wako kwa malengo ya
kujikomba kwao ili ujinufaishe binafsi.
Nafasi ya vijana wasomi ni kusaka elimu
na baadaye kuisambaza ili Tanzania na Bara la Afrika liondokane na kuchekwa kama watu omba
omba waliopewa baraka ya rasilimali watu
na vitu kama madini lakini
tumelala usingizi wa pono wanongojea kuvulia na kuliwa na wavuvi wenye
weledi!
Ndugu Watanzania wenzangu
Rasimu ya Katiba mpya imetoka, ina
mapendekezo mengi ya kuiondoa Tanzania
kwenye mifumo ya utawala ya miungu
mtu na polepole kutupeleka kwenye mifumo
ya utawala ya uwajibikaji na uwazi huku wengi wakishiriki katika kutoa maoni juu ya lipi lifanyike ili kuendesha shughuli zetu za
uzalishaji na usambazaji hudumu wenye ufanisi na tija. Nafasi ya vijana wasomi
ni kuhoji kila ibara iliyomo kwenye Rasimu hii kuona kama haiwezi kuboreshwa
zaidi. Si kazi ya vijana wasomi kusifia
yaliyoisha pendekezwa na kulala usingizi wa pono kungojea kuvuliwa na kuliwa na
wavuvi welevu au wezi wa matokeo ya uvuvi wa wengine lakini amabo ni wajaja wa kuvuna wasichopanda!!! Hiyo ndiyo nafsi ya vijana wasomi, tena waliosafiri
masafa marefu hadi Oslo Norway kuupata usomi wenyewe!!! Nafasi ya vijana wasomi
nikujikita kwenye tafakuri tunduizi (crititical
thinking) siyo kuwa mazezeta
wanosema “Ndiyo” kwa kila kitu au kuwa na maono na dira za muda mfupi kuhusu maswala kama ya
elimu na lugha ya
kufundishia, muundo wa Muungano wa Tanzania, na utawala
wa majimbo.
Jambo la pili ninatamani kugusia ni kuhusu nafasi ya vijana wasomi katika
kutetea uboreshaji wa sehemu ya Rasimu ya Katiba Mpya inayozungumzia juu wa
Muundo wa Muungano. Rasimu inapendekeza
kuwepo muungano wa serikali tatu: ya Shirikisho yenye kuongozwa na Rais na
Makamu Rais, na mbili kwa kila washirika
wa Muungano wawili, Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar zitakazo ongozwa na Rais pia.
Ndugu Watanzania wenzangu
Katika hili na waasa vijana wasomi wang’ag’anie kuendelea kuwepo kwa utaifa
wa TANZANIA na kutokuvunjwa kwa MUUNGANO huu pekee AFRIKA uliodumu miaka
49. Vijana wasomi wawe tayari kuboresha
mapendekezo yaliyotolewa kwa kutaka kuwepo Rais na makamu Rais MMOJA tu katika
Jamuhuri ya Muhungano ya Tanzania, RAIS
wa SHRIKISHO ya JAMUHURI YA MUNGANO
YA TANZANIA. Serikali za Washirika wa MUUNGANO huu, ya Tanzania Bara na
Tanzania Zanzibar ziongozwe na MAWAZIRI WAKUU, ili baadaye Shirikisho la Afrika
Mashariki litakapo zinduliwa siku za karibuni basi tuwe na MAWAZIRI WAKUU 6 yaani
wa ZANZIBAR, TANZANIA BARA, RWANDA, BURUNDI, UGANDA, na KENYA.
Nayasema haya kwa vile mimi ni muumini asiyekubali
kuyumbishwa, wa itikadi ya Umajumui wa Kiafrika (Pan Africanism). Mimi natoa maoni yangu lakini
najua na wengine wanaweza au kuniunga mkono au kunikatalia maana
hiyo ndiyo demokrasia. Ikiwa ninachotetea kikikataliwa na hakuna madhara
yatayotokea huko mbele ya safari itakuwa ni safi tu. Ikiwa nikishauri kitu watu
wakakikataa na baadaye wakadhurika,
walau mimi nitasema nilisema na nafsi yangu itakuwa na
amani .
Ndugu Watanzania wanzengu,
Mzee Abeid Karume aliweza kuwaongoza Wazanzibari wakakubali ushauri wa kuwa
na Muungano lakini leo wanao viongozi wengine wanaowashauri kutengana kuna masilahi
kwa Wazazibari, kazi kwao kutafakari. Pia kuna baadhi ya watanzania
wa Bara wengine wanadhani kuungana na
Zanzibar si lazima lakini mimi nafikiri itakuwa haina usalama
sana kwa Tanzania Bara kuwepo Zanzibar yenye kuwa
Kuwait ya Afrika Mashariki, yenye jeshi lake linalodhibitiwa na
Uingereza na Marekani na labda yenye kuwa na vituo vya
kijeshi vya Marekani, huku
viongozi wake wakijifanya eti Wazanzibari wote ni Waislamu kama vile
wanavyofanya viongozi wa Kuwait au
Oman...
Nakumbuka wapo Wazanzibari wengi wenye biashara zao Tanzania Bara na wenye
mahusiano ya karibu na watu wa Tanzania Bara yanayosukumwa na ufuasi
wa dini moja ya Kiislamu au kupeana mikopo ya kuanzishia biashara..Wote
hawa ni WATANZANIA na wanayo haki kumiliki ardhi Tanzania Bara na
kujisikia wako nyumbani. Mheshiwa Waziri wa Afya wa
sasa aliwahi kuwa Mbunge jimbo moja hapa Tanzania Bara na baadaye
karudi Zanzibar na kuchanguliwa
Ubunge jimbo la Zanzibar na sasa ni Wazir wa Afya kwenye serikali ya
Muungano inayoshughulikia mambo ya afya Tanzania Bara. .Mzanzibari anayedhani
kuna manufaa kwa Wazanzibari katika
kufuta utaifa wa UTANZANIA nakufufua utambulisho wa Utanganyika sina hakika amekaa na kufikiria sana juu ya madhara ya kufufua
utambulisho huo….Labda kama ni Mzanzibari anayeishi Omani au Kuwait kwa sasa
na hana mahusiano na Wazanzibari wenzake
walio na mahusiano ya karibu na Tanzania
Bara.
Vile vile, kiulinzi na usalamana mtengamano kati ya waumini wa dini mbali
mbali Tanzania Bara unasaidiwa kwa kuwepo dola moja la Tanzania. Watanzania Bara
wanaodhani ulinzi na usalama wa Tanzania Bara utakuwa wa
gharama zile zile kama za sasa ambapo
kuna uraia wa Tanzania moja, tuna
jeshi la ulinzi, usalam na polisi moja
ya dola moja la taifa moja
la UMAJUMUI wa KIAFRIKA la Tanzania, lisilo mbagua mtu kwa uzawa wake
wala nasaba yake kuhusisha nasaba za
Asia au Ulaya, Niinashaka kama
kweli hawa wanao shabikia kurudi
kwenye utambulisho wa UTANGANYIKA
tuliopachikwa na wakoloni wa
Kiingereza baada ya sisi kuitwa GERMAN EAST AFRIKA na Wagerumani hadi 1919,
wamekaa nakutafakari kwa kina juu
ya jambo ili kama alivyo kuwa amefanya Mwalimu Nyerere.
Ndugu Watanzania wanzengu,
Kinachounganisha Mzanzibari wa uzawa wa Urabuni au Uhindini ni kukubali
kuitwa MUAFRIKA, au siyo? Kinachounganisha Mhehe wa Iringa na Mhaya wa Bukoba na Muha wa Kigoma ni
kukubali kuitwa MUAFRIKA, au siyo? Hivi ukianza kushabikia kuvunja nchi ya
Tanzania iliyodumu zaidi ya miaka 49 (1964-2013) na kushabikia Utanganyika
uliodumu miaka takribani 45 ( 1919-1964) (ambayo miaka zaidi ya 42 yake ilikuwa
chini ya utawala wa kikoloni wa Waingereza na inawezekana Watanganyika wengi
HAWAKUJITAMBUA kuwa walikuwa Watanganyika!) , una huhakika gani kuwa hii
Tanganyika itakayo fufuliwa na wanasiasa wachovu wa kizazi hiki cha mafisadi waliojaa udini na ukabila
haitamegeka pia vipande vipande kwa misingi ya ukabila na udini?
Kinachoweza kutuunganisha leo na jana
hapa Tanzania ni kujitambuwa kuwa
sisi ni WAAFRIKA, na UTANZANIA ni kituo
cha kati kuelekea utambulisho ulio imara
na wenye mashiko zaidi wa UAFRIKA
MASHARIKI na UAFRIKA WA BARA ZIMA. Hayo ndiyo mawazo yangu na mimi si Napoleon au Bismark
au Musolini, kwa hiyo niko tayari kukaa kwa huzuni kwa kukataliwa maoni
yangu ninayodhani ni sahihi! NJE ya UZALENDO wa UMAJUMUI wa KIAFRIKA hakuna
uzalendo mwingine zaidi ya ushabiki wa kibaguzi wa kidini na kikabila!!! I am an Afrikan! I am an East African! I am a
Tanzania! I refuse to return to being a
Tanganyikan after 49 years of liberation!!!
Ndugu Watanzania wanzengu,
Jambo la tatu ninalotaka kugusia
ni kuhusu nafasi ya vijana wasomi katika mchayo wenyewe wa kuandika Katiba
Mpya. Tujikumbushe kuwa kutolewa Kwa Rasimu ni hatua moja muhumu lakini njia
bado ni ndefu na hatujafika kwenye Katiba Mpya. Vijana wasomi wapaze sauti zao sasa hivi,
wiki hii na mwezi huu kunadi marekebisho ya Sheria iliyoanzisha mcahakato huu
ili vifungu vinavyoaanisha nini liwe Bunge la Katiba litakalo pendekeza Rasimu
ya Mwisho itakayo pigiwa kura ya maoni liwe si ili linaloainishwa kwenye Sheria
kwa sasa ambalo litakuwa limejaa Wabunge na
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa zaidi ya dheluthi mbili.
Hivi karibuni Kamati Maalum ya Katiba
iliyondwa na Kituo cha Haki za Binadamu Tanzania yaani LHRC kimetoa taarifa
ifuatayo kwa vyombo vya habari:
“Kwa mujibu wa
Kifungu 22 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 (Sura ya 83) Bunge
la Katiba limetamkwa kuwa na wajumbe wafuatao; ambao jumla yao ni wajumbe 604:
(b)
Wajumbe
wote wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar (yaani tunaweza kuwaita wabunge wote
wa Bunge la Zanzibar) ambao jumla yao ni 81.
(c)
Wajumbe
wengine wapatao 166 ambao watateuliwa na Rais kutokana na makundi yafuatayo:
Asasi sizizo za kiserikali (NGOs), Taasisi za kidini (FBOs), Vyama vyote vya
siasa venye usajili wa kudumu, Taasisi za Elimu ya Juu, Makundi ya watu wenye
mahitaji maalum, Vyama vya wafanyakazi, Vyama vinavyowakilisha wakulima,Vyama
vinavyowakilisha wafugaji, Makundi mengine yoyote yale ya watu (yakitumia jina
lolote) ili mradi yawe na malengo ya aina moja.
Ni maoni thabiti
ya Kamati yetu kuwa uundaji wa Bunge la Katiba lenye wajumbe waliotajwa hapo
juu utakuwa ni upotezaji wa muda usiozingatia maslahi ya nchi na watu wake kwa
kuwa Bunge hilo halitakuwa tofauti na Bunge la sasa kwa kuwa wajumbe walio
wengi (zaidi ya asilimia 72) watakuwa ni wabunge wote kutoka Bunge la Muungano
na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.”
Ndugu
Watanzania wanzengu,
Mimi ni
mmoja wa wajumbe wa wajumbe wa Kamati hiyo Maalum iliyoundwa na Kituo cha Haki
za Binanadamu na ninawaasa vijana wasomi wapaze sauti kudai marekebisho ya
Sheria ya Mchakato wa Kuandika Katiba Mpya ili walau wajumbe wa Bunge la Katiba watakao tokana na Bunge la Jamhuri la sasa pamoja na
Baraza la Wawakilishi la saa , wasizidi THELUTHI
MOJA, na wajumbe wengine wa BUNGE
MAALUUM LA KATIBA , yaani theluthi mbili zilizobaki, « zitokane
na wananchi na wadau walio nje ya mfumo wa vyama vya siasa ». Vijana
wasomi walione hili na kulishupalia kama
kweli tunataka Mazuri yaliyo katika Rasimu hii yajitokeze kwenye Rasimu
itakayopigiwa kura ya maono baada ya kupitishwa na BUNGE MAALUUM LA KATIBA.
Vijana wasomi lazima wajue kuwa ni
lazima « kupata Katiba mpya ambayo
haitafuata misingi ya kiitikadi ya chama fulani na ambayo itazingatia misingi
ya upatikanaji wa Katiba yenye kuleta tija na kuipeleka nchi hii katika hatua
ya juu ya maendeleo.
Ndugu Watanzania mliokusanyika hapa Oslo leo,
Ndugu marafikiwa Wantanzania manaowasidikiza katika sherehe hii,
Natamani kusema mengi lakini
nafikiri tayari nimepunguza sana muda wenu wa kula , kunywa na kujirusha.
Nawashuru kwa kuyasikiliza maoni yangu juu nafasi ya vijana wasomi wa Tanzania kna Katiba Mpya katika
Maendeleo endelevu ya Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla. Jitaidini basi ndugu zangu mzidue Mwalimu Julius Nyerere
wa zama zenu miongoni mwenu kwa
kuzingatia ushauri wa kuwa wadadidisi na weledi.
Mungu ibariki Tanzania
Asantteni sana!!!
Mwl. Azaveli Lwaitama
Kringsjågrenda 1
Oslo, Norway,
8 Juni 2013