Wednesday, 19 June 2013

Kenya kutumia ndege zisizo na marubani kuzuia waingizaji wa silaha za magendo, al-Shabaab

Na Bosire Boniface, Garissa

Kenya inajiandaa kusambaza ndege zisizo na marubani aina ya 'drones' kama sehemu ya operesheni za usalama zilizoongezwa katika mipaka yake na Somalia na Ethiopia kufuatilia na kukomesha harakati za al-Shabaab na waingizaji wa silaha za magendo, maofisa usalama waliiambia Sabahi.

                                         drone

  • Vikosi vya usalama vya Kenya vikifanya misheni ya ukaguzi huko Liboi katika mpaka wa Kenya na Somalia mwezi Oktoba 2011 baada ya wafanyakazi wawili wa msaada wa Kihispania kutekwa katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab. [Tony Karumba/AFP] Vikosi vya usalama vya Kenya vikifanya misheni ya ukaguzi huko Liboi katika mpaka wa Kenya na Somalia mwezi Oktoba 2011 baada ya wafanyakazi wawili wa msaada wa Kihispania kutekwa katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab. [Tony Karumba/AFP]
  • Polisi wa Kenya wenye hadhi ya kijeshi jijini Nairobi wakilichoma rundo hili la silaha haramu zilizokamatwa mwezi Machi 2009. [Simon Maina/AFP] Polisi wa Kenya wenye hadhi ya kijeshi jijini Nairobi wakilichoma rundo hili la silaha haramu zilizokamatwa mwezi Machi 2009. [Simon Maina/AFP]
Ndege aina ya 'drones', au vyombo vya angani visivyo na marubani, zinahitajika kusaidia vikosi vya usalama vya Kenya kufanya doria katika mipaka ya nchi, alisema Patrick Ochieng, mkurugenzi wa Eneo Lengwa La Kitaifa la Kenya kuhusu Silaha ndogondogo na Silaha Nyepesi.
"Tunakabiliwa na changamoto za ulinzi ambazo hazijawahi kutokea," aliiambia Sabahi. "Sio tu kuwa tuna vitisho kutoka ndani ya nchi, bali pia kutoka kwa waasi wa al-Shabaab."
Uingizaji silaha kwa magendo na upenyezaji unaofanywa na al-Shabaab katika mkoa wa kaskazini-mashariki wa Kenya umeleta hali ya kutokuwa na usalama pamoja na athari mbaya, alisema, akiongeza kwamba miaka miwili iliyopita imeshuhudia ongezeko la vurugu kutokana na bunduki haramu, kwa wahalifu na wauza silaha kwa magendo kuzua njia mpya za kuuza silaha kwa magendo.
Ndege zisizo na marubani zitawekewa teknolojia ya kiwango cha juu ikiwa ni pamoja na kamera zinazoweza kuona usiku ili kuisaidia Kenya kuwashinda wahalifu na kuondoa vitisho vya usalama, Ochieng alisema.
Maofisa usalama wanapata mafunzo kuhusu ndege zisizo na marubani, ambazo zitaanza kazi mwishoni mwa mwaka huu, alisema Ochieng. Alikataa kupeana maelezo zaidi kuhusu programu hiyo, alisema kwamba kwa kufanya hivyo kutasaidia wanaoingiza silaha nchini.
Kufanya kazi ya upolisi Kenya, katika mpaka wa Kenya na Somlia wenye urefu wa zaidi ya kilometa 800 ni changamoto kubwa, alisema Mkuu wa Polisi wa mkoa wa kaskazini mashariki, Charlton Mureithi, na kutumia ndege hizo kutasaidia maofisa waliopo ardhini.
"Tunaamini teknolojia hii itaendelea kwa muda mrefu katika kushughulikia vitisho vya usalama katika mkoa kwa sababu ndege hizo zitafuatilia njia zilizo pembezoni sana zinazotumiwa na wafanya magendo," aliiambia Sabahi.

Kuwekeza katika usalama

Meja mstaafu wa jeshi Bishar Hajji Abdullahi alisema serikali inapaswa kuwekeza katika teknolojia hiyo hata kama ni ghali kwa sababu lengo la ulinzi wa nchi linapaswa kupewa kipaumbele kuliko gharama.
"Licha ya suala la ndege zisizo na marubani kuelekea kuleta utata nchini kote, katika baadhi ya matukio, serikali ina wajibu wa kuwalinda raia wake kwa gharama zozote zile," aliiambia Sabahi.
Hata hivyo, teknolojia nzuri haiwezi kuleta matokeo yanayotarajiwa pasipo mafunzo yanayofaa kwa maofisa usalama, alisema. "Serikali inapaswa kuwa makini siyo kuzamisha fedha katika teknolojia isiyo na manufaa," Abdullahi alisema.
Kadri vifaa vya usalama vinavyokuwa na gharama ya chini kuvipata, Kenya inapaswa kuwekeza kikamilifu katika kukabili vitisho vya uhalifu, hususani kutoka kwa al-Shabaab, alisema.
"Kwa mfano katika mkoa wa Kaskazini Mashariki, mahali palipo na mashambulio ya mara kwa mara ya al-Shabaab, serikali inapaswa kuwapa maofisa wa usalama magari ya deraya na fulana zisizopenyeka risasi," Abdullahi alisema.
Serikali ilitangaza bajeti yake ya mwaka wa fedha wa 2013-2014 tarehe 13 Juni, ikitenga shilingi bilioni 67 (dola milioni 784 ) kwa ajili ya usalama.
Katibu wa Hazina ya Taifa Henry Rotich alisema shilingi bilioni 4 (dola milioni 46.9) za fedha zilizotengwa zitaenda kwenye vifaa vya usalama, shilingi bilioni 4.5 (dola milioni 52.7 ) kwa operesheni zilizoimarishwa, na shilingi bilioni 1.5 (dola milioni 17.6) kwa ajili ya utafiti katika kuboresha mbinu za kuzuia uhalifu.

chanzo: Sabahionline.com