Kwa ufupi
Arusha/Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limetishia
kuwakamata Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema na limesema litamhoji Katibu Mwenezi wa CCM, Nape
Nnauye baada ya wanasiasa hao kudai kufahamu watu waliohusika na tukio
la kurushwa bomu mwishoni mwa wiki iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha
jana, Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul Chagonja aliwataka
wanasiasa hao kuwasilisha ushahidi wa kile wanachofahamu kuhusu
kulipuliwa kwa bomu hilo.
Juzi, Mbowe akiwa na Lema, alisema wana ushahidi
wa picha za video zikiwahusisha polisi na kulipuliwa kwa bomu hilo
katika Uwanja wa Soweto wakati wa mkutano wa kuhitimisha kampeni za
udiwani kwa Chadema, Jumamosi iliyopita.
Mkwara wa Chagonja
Kamishna Chagonja aliwataka Mbowe na Lema kupeleka ushahidi ili kusaidia uchunguzi wa tukio hilo.
“Tunamtaka Mbowe na Lema kutoa ushahidi wa askari
wetu kuhusika na tukio la bomu pale Soweto. Wasipofanya hivyo tutatumia
sheria kuwalazimisha kufanya hivyo kwani yeyote mwenye ushahidi unaoweza
kusaidia upelelezi wa kosa la jinai akikataa kuuwasilisha kwa vyombo
husika anaweza kuchukuliwa hatua,” alisema.
Nape naye kuhojiwa
Kwa upande wake, polisi limesema litamhoji Nape
ambaye alikaririwa jana akidai kuwa Chadema ndiyo waliohusika na
urushaji wa bomu kwenye mkutano wao baada ya kuhisi kushindwa kwenye
uchaguzi wa kata nne za Jiji la Arusha.
Kamishna Chagonja alisema watamhoji ili kusaidia
kazi yao ya upelelezi. Nape aliihusisha Chadema kwa kauli alizoita za
kutishia amani zilizowahi kutolewa siku za nyuma kabla ya uchaguzi wa
kata za Arusha.
Watatu wakamatwa
Kamishna Chagonja alisema watu watatu wamekamatwa wakihusishwa na tukio la kulipuliwa kwa bomu mkoani Arusha.
Alisema watuhumiwa hao wanahojiwa na polisi na
watafikishwa mahakamani muda wowote ushahidi wa kutosha utakapopatikana
au kuachiwa huru wakigundulika kutokuhusika.
Kamishna Chagonja alikataa kutaja majina ya watuhumiwa akidai kwa kufanya hivyo kunaweza kuharibu upelelezi.
Polisi wajitetea kurusha risasi
Akizungumzia madai ya polisi kutumia risasi za
moto katika tukio hilo, Kamishna Chagonja alisema walilazimika kupiga
mabomu na kurusha risasi hizo ili kuwadhibiti wafuasi wa Chadema
waliokuwa wakiwazuia kumkamata mtuhumiwa.
Hata hivyo, Mtoto Abubakar Adam, mwenye umri wa
miaka kumi na moja, ambaye ni mmoja wa majeruhi waliolazwa katika
Hospitali ya Selian alikaririwa na gazeti hili jana akiwatuhumu polisi
kumpiga risasi.
Kamishna Chagonja alisema: “Baada ya bomu kurushwa
na kulipuka, polisi walianza kukimbilia eneo la tukio lakini vijana wa
Chadema wakaanza kuwashambulia polisi ambao walilazimika kujihami.”
Tendwa awaonya Mbowe na Nape
Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa amewataka
viongozi wa Chadema na CCM kuwasilisha ushahidi wa taarifa zao za madai
ya kuwafahamu watu waliohusika na tukio hilo ili waweze kuchukuliwa
hatua za kisheria.
Kauli ya Tendwa imekuja baada ya Nape kudai
kumkariri Lema akisema kuwa uchaguzi hauwezi kufanyika, huku Mbowe
akidai kuwa wana ushahidi wa CD ambao umemwonyesha askari polisi wa
Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kuhusika na tukio la urushaji wa bomu
kwenye mkutano huo wa chama chake na kusababisha watu watatu kufariki
dunia na wengine kujeruhiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Tendwa alisema kauli za viongozi hao zinawachanganya wananchi.
Alisema kitendo cha kunyoosheana vidole bila ya
kutoa ushahidi ni kutafuta umaarufu usio na faida, jambo ambalo linaweza
kuongeza chuki na hasira.
Imeandikwa na Peter Saramba, Mussa Juma na Patricia
Kimelemeta.
chanzo: Mwananchi newpaper.
chanzo: Mwananchi newpaper.