Posted Jumanne,Juni11 2013 saa 21:32 PM
Kwa ufupi
- Mwanaye wa kwanza, Zenani Mandela-Dlamini ambaye ni Balozi wa Afrika Kusini nchini Argentina amewasili Pretoria kufuatilia hali ya baba yake aliyelazwa hospitali Jumamosi iliyopita.
Johannesburg. Wasiwasi umezidi kutanda miongoni
mwa familia na raia wa Afrika Kusini kuhusu afya ya Rais wa zamani wa
nchi hiyo, Nelson Mandela ambaye amekuwa akipatiwa matibabu kwenye
Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) kwenye Hospitali ya Mediclinic,
Pretoria, Afrika Kusini.
Tayari wanafamilia wake wameanza kurejea Afrika
Kusini kutoka maeneo mbalimbali duniani na ndani ya Afrika Kusini na
kuelekea Pretoria kufuatilia kwa karibu hali yake. Kwa mujibu wa taarifa
za kitabibu, Mzee Mandela (94) ambaye ni maarufu kwa jina la Madiba,
hajitambui. Amelazwa hospitalini kwa siku ya tano sasa ambako anaendelea
kupatiwa matibabu kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu.
Mwanaye wa kwanza, Zenani Mandela-Dlamini ambaye
ni Balozi wa Afrika Kusini nchini Argentina amewasili Pretoria
kufuatilia hali ya baba yake aliyelazwa hospitali Jumamosi iliyopita.
Mkewe, Graca Machel alilazimika kuahirisha safari
yake ya kikazi tangu Jumamosi ili kuwa karibu naye na mke wake wa zamani
ambaye walitalikiana, Winnie Mandela pia ni miongoni mwa jamaa
waliojumuika kumjulia hali Rais huyo wa Kwanza mweusi wa Afrika Kusini.
Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), lilisema
kwamba Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma jana alikutana na madaktari
wanaomtibu Mzee Mandela na baadaye kutoa taarifa fupi akisema
ameridhishwa na jitihada wanazofanya katika kumpatia matibabu.
Kijijini kwake
Huko kijijini kwake Qunu, wakazi wameendelea kukumbwa na shaka na wamekuwa wakifanya maombi ili afya ya Mandela iimarike.
Tayari baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa
vimeshaweka kambi katika eneo hilo la Qunu kwa ajili ya kuchukua matukio
mbalimbali yanayoendelea katika kipindi hiki cha shaka na wasiwasi
kuhusu kiongozi huyo.
Jana, Msemaji wa Ikulu ya Afrika Kusini, Mac Maharanji alisema hali yake haijabadilika.