Kwa ufupi
Arusha: Mashuhuda wa tukio la mlipuko wa bomu
uliotokea mwishoni mwa wiki iliyopita Jijini Arusha, wamedai kumwona na
kumtambua mtu aliyehusika na tukio hilo lakini wanasema walishidwa
kumkamata kutokana na “kushambuliwa kwa risasi na polisi”.
Mlipuko huo ulitokea katika Viwanja vya Soweto
kwenye mkutano wa kuhitimisha kampeni za udiwani jijini humo na
kusababisha vifo vya watu wanne na majeruhi zaidi ya 100.
Mashuhuda hao ambao wote walijeruhiwa kwa risasi
wanasema mlipuaji wa bomu alikuwa amevalia shati la kijivu lenye mistari
myeusi na suruali ya jeans yenye rangi ya blue na kwamba wajihi wake ni mtu wa kimo cha kati.
Mmoja wa mashuhuda hao ni mlinzi katika Kikosi cha
Ulinzi cha Chadema (Red Brigade) ambaye hakutaka jina lake litajwe
gazetini, alidai kwamba alimwona mtu aliyerusha bomu mara tu baada ya
tukio hilo.
Mlinzi huyo ambaye alipigwa risasi za mguuni na
kifuani wakati akimkimbiza mtu huyo, alisema bomu hilo lililipuka mara
tu baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kumaliza kuhutubia na
kushuka jukwaani.
“Baada ya Mwenyekiti Freeman Mbowe kushuka
jukwaani, nikawapanga walinzi kwa ajili ya kuwalinda viongozi waliokuwa
wakichangisha fedha. Ghafla nikasikia mlipuko, sikujua ni nini, lakini
kuna mama mmoja alikuwa karibu yangu akanionyesha mtu aliyelipua,
akisema yuleee…” alisema na kuongeza:
“Alikuwa amevaa shati la kijivu lenye mistari myeusi na suruali ya jeans ya blue.
Ni mtu wa kimo cha kati. Watu walianza kumkimbiza kuelekea upande wa
Magharibi wa Uwanja kwenye nyumba za NHC. Tuliruka uzio alipopita yule
mtu, mara nikasikia risasi imenipata mguuni.”
“Tulikuwa na uwezo wa kumkakata yule mtu, lakini
nikaona risasi zimezidi upande wetu nikaona nigeuze na hapo hapo
nikapigwa risasi ya kifuani, nikaishiwa nguvu, sikuweza kufahamu mtu
huyo alikoishia. Nilijikongoja na kurudi uwanjani.”
Mlinzi huyo ambaye amelazwa katika moja ya
hospitali za jijini Arusha anasema alilazimika kuhama hospitali ya
Seliani alikokuwa amelazwa awali baada ya kuandamwa na polisi. “Nilikaa
siku tatu hospitalini bila kupata huduma yoyote, lakini kila siku
madaktari walikuwa wakinihoji maswali,”alisema na kuongeza:
“Mwisho nikaambiwa kwamba nitahamishiwa ghorofa ya
chini, nilipouliza sababu wakasema eti Waziri Mkuu atakuja kuniona…
Niligoma mwisho daktari akaniambia kuwa kuna polisi waliovaa majoho ya
udaktari ndiyo waliotaka nihamishwe”.
Maelezo yake yanafanana na yaliyotolewa na
majeruhi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Abdallah Alila ambaye
alisema kuwa alimwona mtu aliyelipua bomu “akiingia kwenye gari la
polisi”.
“Baada ya mlipuko, sikujua kama nimeshapigwa
risasi, lakini niliona watu wakimkimbiza mtu baada ya mama mmoja kusema
kuwa ndiye aliyerusha bomu.
Watu waliokuwa wakimkimbiza walikuwa wakirushiwa risasi na
polisi. Baadaye nilimwona mtu huyo akipanda gari la polisi. Nashangaa
tena kusikia polisi wakimtafuta huyo mtu,” alisema Alila.
Polisi wodini
Mbali na taarifa kwamba polisi walikuwa
wakizunguka katika wodi za wagonjwa wakiwa wamevalia majoho ya
madaktari, pia mgonjwa mwingine amedai kwamba askari wamekuwa
wakimfuatilia kila kukicha.
Peter Mshanga ambaye amelazwa katika Hospitali ya
Selian hivi sasa kutokana na kujeruhiwa kwa risasi katika mguu wake wa
kushoto alisema awali alipelekwa katika hospitali ya St. Elizabeth
lakini alihama baada ya kuandamwa na askari kanzu.
“Mara baada ya bomu nilipelekwa Hospitali ya St.
Elizabeth na huko nilishangaa kuwaona askari ninaowafahamu wakizingira
kitanda changu. Hata nilipokwenda chooni askari mmoja alinifuata,
nikamuuliza anataka nini, yeye akanijibu eti anataka kunisaidia,
nikamkatalia akatoka nje,” alisema Mshanga na kuongeza:
“Waliendelea kuzingira kitanda changu kwa siku
kadhaa, siku ya tatu daktari akasema nitakiwa nihamishiwa hospitali ya
Mount Meru, nikapinga”.
Wakati huo walikuwa tayari wameandaa ambulance
(gari la wagonjwa) na gari la polisi ili wanihamishe. Ndugu zangu
walipinga ndipo nikahamishiwa hapa Seliani,”anasema.
Kuhusu kujeruhiwa kwake, Mshanga alisema baada ya mlipuko alishtukia ameshajeruhiwa mguuni na akaanguka chini.
“Nilikuwa nimeshika Sh500 mkononi nikisubiri kutoa
sadaka yangu. Mara nikaona watoto wanaanguka mbele yangu, nikasikia
kishindo kikubwa, kisha nikakimbia kubeba mmoja wa watoto, na mimi
nikaanguka, kumbe nilikuwa nimejeruhiwa,” alisema.
Jana gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas kuzungumzia suala la polisi kuwafuatilia
majeruhi lakini alipopokea simu alisema hawezi kuzungumza kwa wakati
huo kwa kuwa yuko kwenye kikao. “Niko kwenye kikao,” alisema Sabas na
kukata simu yake.
Mkanganyiko wa taarifa
Wakati Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu sera na Uratibu wa Bunge, William Lukuvi ikitoa kauli kuwa
polisi walijihami kwa kuwapiga wananchi risasi na mabomu ya machozi,
mmoja wa maofisa polisi aliyekuwa uwanjani wakati wa mlipuko ambaye pia
hakutaka jina lake litajwe gazetini amekanusha kupiga watu risasi. “Mimi
ndiyo nilikuwa pale uwanjani, baada ya bomu kulipuka wafuasi wa Chadema
walianza kutushambulia tulipojitokeza kubeba majeruhi hadi wakavunja
kioo cha gari yetu. Niliwaamuru askari warushe risasi hewani, hakuna
hata mtu mmoja aliyepigwa risasi,” alisema na kuongeza:
“Unajua wafuasi wa Chadema wamelishwa chuki na viongozi wao,
kama Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema ambaye alisema akivamiwa na
majambazi heri afe kuliko kumpigia simu RPC. Ndiyo maana watu walijawa
chuki wakaja kutushambulia.”
Aliendelea: “Baada ya kuona mashambulizi yamezidi
tukaondoka, lakini baadaye tukarudi na kukuta majeruhi wote
wameshaondolewa na wafuasi wa Chadema. Baadhi ya askari kanzu
waliwafuatilia majeruhi ili kujua majina na idadi yao ili tutoe
taarifa”.
Kama ni risasi basi wamepigwa na viongozi wa
Chadema kwani maganda mengi ya risasi yameonekana kuwa ya bastola na
viongozi wao wengi wanazo,”alisema.
Source: Mwananchi
Source: Mwananchi