Tuesday, 22 October 2013

Ugaidi waitesa serikali

22nd October 2013
Baadhi ya washtakiwa wa kosa la ugaidi wakishuka kutoka katika gari la polisi kuelekea Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Mtwara wakiwa chini ya ulinzi mkali kwenda kusomewa mashtaka yanayowakabili jana.
Serikali  imepata aibu ya tatu baada ya kesi ya ugaidi waliyofunguliwa watu 11 mkoani Mtwara kuondolewa mahakamani na badala yake watuhumiwa hao wamefunguliwa mashtaka mapya mawili ambayo siyo ya ugaidi.

Watuhumiwa hao ni Mohamed Matete (39), mkazi wa kata ya Sengenya; Hassan Hamli (39), mkazi wa Kijiji cha Mkumbalu; Rashid Ismail (27), mkazi wa kijiji cha Likokona; Abdalah na  Hamis (33), mkazi wa Likokona.

Wengine ni  Salum Bakari (38), Fadhili Adam (18), Ramadhan Adam (26), Ismail Chande (18), Issa abedi (23) wakazi wa kijiji cha Likokona.
Washitakiwa wengine ambao ni wakazi wa kijiji cha Nalunyu ni Abas Muhidin (32) na Saidi Mawazo (21).

Pigo la kwanza kwa serikali lilikuwa Mei mwaka huu wakati Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilipomfutia mashtaka matatu ya ugaidi, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare na mwenzake Joseph Ludovick Rwezaura.

Kesi nyingine ya ugaidi ambayo serikali ilishindwa ni Agosti mwaka huu, iliwahusu makada watano wa  Chadema ambao walifunguliwa shtaka  la ugaidi mkoani Tabora. Watu hao ni ni Henry John Kilewo, ambaye ni Katibu wa Chadema Wilaya ya Kinondoni, Evodius Justinian, Oscar Kaijage, Rajabu Daniel na Seif Magesa Kabuta.

Mahakama Kuu Kanda ya Tabora ilifutia shtaka hilo la ugaidi lililokuwa linawakabili wanachama hao wakisema kosa lao ni la jinai na halipaswi kuitwa la ugaidi. Katika uamuzi wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Simon Lukelelwa, aliwaonya waendesha mashtaka kuacha tabia ya kutumia maneno makali ya ugaidi katika kesi za jinai, hatua aliyosema inaogofya wageni wanaotarajia kuja Tanzania.

Washitakiwa wa tukio la Mtwara mara ya kwanza walipofikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nanyumbu Oktoba 3, mwaka huu na kusomewa shitaka la ugaidi.

Jeshi la Polisi mkoani Mtwara lilidai kuwakamata mwishoni mwa Septemba mwaka huu katika Wilaya ya Nanyumbu wakidaiwa kufanya mafunzo ya kigaidi. Washitakiwa hao Alhamisi iliyopita walishindwa kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mtwara, kutokana na maelezo ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Stephen Zelothe, kwamba baadhi ya taratibu za kisheria hazijakamilika.

Siku hiyo hiyo walisafirishwa na kurejeshwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nanyumbu na kufutiwa shitaka la ugaidi.

Jana washitakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mtwara  na kusomewa mashtaka mawili ya kufanya mkusanyiko usio halali na la kufanya uchochezi. Akisoma mashitaka hayo mbele ya Hakimu  Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, Dynes Lyimo, Wakili wa serikali Mfawidhi Mkoa wa Mtwara, Ladislaus Komanya, alidai kuwa  washitakiwa wameondolewa shitaka la kwanza lililokuwa likiwakabili chini ya kifungu cha 91,(1) cha mwenendo wa makosa ya jinai.

Komanya alidai kuwa Septemba 21 na 26, mwaka huu katika msitu wa Makorongo Likokona, walifanya mkusanyiko usio halali kinyume cha kifungu cha  sheria namba 74, kwa nia ya kutenda uhalifu  na kupeleka wananchi  wa eneo hilo kupata hofu, hali iliyopelekea uvunjifu wa amani.

Katika shitaka la pili la uchochezi, Komanya alidai kinyume na kifungu cha sheria namba 31 na 32, cha Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, walikutwa na kanda  za video (CD)  zenye machapisho ya uchochezi kinyume cha sheria, hivyo  kujenga hofu kwa wananchi wa maeneo hayo. Lyimo alisema dhamana za watuhumiwa hao iko wazi na kwamba endapo mtuhumiwa ana ndugu anaruhusiwa kutolewa dhamana.

Lyimo alisema kuwa dhamana kwa kila mtuhumiwa atatakiwa kuwa na wadhamini wawili, mmoja akiwa ni mtumishi wa serikali au taasisi yoyote inayotambuliwa na serikali pamoja na mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh. milioni tano. Mtuhumiwa wa kwanza, Mohamed Matete (39) alieleza kushangazwa na kitendo cha kufutiwa shitaka la kwanza la ugaidi lilokuwa likiwakabili na kufunguliwa mashitaka mengine na kudai kuwa mpaka sasa kesi waliyosomewa hawajui wanashitakiwa na nani.

“Mheshimiwa hakimu tarehe 17, mwezi huu tulifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nanyumbu, tukishitakiwa na Jeshi la Polisi, lakini kesi ile tulifutiwa, leo hii tunafikishwa katika mahakama yako na makosa mawili huku tukiwa hatuna hati ya mashitaka na hatujui tunashitakiwa na nani?” alihoji.

Mohamed alidai kuwa hati ya shitaka la kwanza walilokamatwa na kufikishwa mahakamani na Jeshi la Polisi, wamenyang’wanywa na jeshi hilo huku akidai kuwa ni haki ya mshitakiwa kuwa na hati ya shitaka linalomkabili.

Kufuatia madai hayo,, Hakimu Lyimo alimwagiza wakili wa serikali kuhakikisha washitakiwa hao wanapatiwa hati ya mashtaka ya jana kwa kuwa ni haki yao ya msingi.

“Kifungo kilichowafanya kuondolewa kosa la kwanza ndicho kifungu kinachomruhusu mlalamikaji kukukamata endapo  ataona mtuhumiwa bado ana kosa.

Kuhusu mnashitakiwa na nani, anayewashitaki ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Hakimu Lyimo.

Washitakiwa walikana mashitaka hayo na kurudishwa rumande hadi Novemba 4, mwaka huu itakapotajwa tena.  Baada ya kuwakamata na kuwafikisha mahakamani Oktoba 3, mwaka huu, Jeshi la Polisi mkoani Mtwara lilitoa taarifa kwa vyombo vya habari Oktoba 7, mwaka huu likidai kuwakamata vijana 11 wakifanya mazoezi ya kigaidi wakiwa na CD 25 za mitandao ya kigaidi ya Al Qaeda na Al Shaabab.

Kwamba liliwakamata wakiwa na vifaa mbalimbali vikiwamo vyakula.

Kamanda Stephen, alisema alidai kuwa mbali na vyakula, vijana hao pia walikutwa vijana hao walikuwa wanafanya mazoezi ya hatari ambayo yana uhusiano na makundi ya kigaidi ya Al Qaeda na Al Shaabab.

Aliongeza kwamba walitumia CD zipatazo 25 zenye mafunzo mbali mbali, baadhi zikihusu Al Shaabab, mauaji ya Osama Bin Laden, Zinduka Zanzibar, kuandaa majeshi, mauaji ya Idd Amin na Mogadishu  sniper.

Vitu vingine ni DVD player moja, Solar panel moja (Watts 30), mapanga mawili, visu viwili, tochi moja, betri moja ya pikipiki namba 12, simu tano za viganjani, vyombo mbali mbali vya chakula, jiko moja la mkaa na jiko moja la mafuta ya taa.
 
CHANZO: NIPASHE