Tuesday 22 October 2013

Pato la Taifa lapanda kwa 6.7%

22nd October 2013
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi NBS, Morrice Oyuke
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imesema kuwa ukuaji wa pato la taifa umeongezeka kwa asilimia 6.7 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013 kutoka asilimia 6.4 mwaka jana, pato ambalo ni sawa na Sh. trilioni 5.

Taarifa hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi NBS, Morrice Oyuke, na kueleza kuwa sababu iliyopelekea kukua kwa pato hilo ni kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa viwandani na huduma.

Alisema shughuli za kiuchumi za kilimo na uvuvi zimekuwa kwa asilimia 5.3 kutoka asilimia 5.1 kwa mwaka jana kutokana na kuwapo kwa mvua za kutosha katika mikoa inayozalisha mazao kwa wingi.

“lakini shughuli za uvivu zilikuwa kwa asilimia 2.4  ikilinganishwa na asilimia 6.5 kwa mwaka jana, kasi ya ukuaji ilipungua kutokana na kupungua kwa mavuno ya samaki kutoka kwenye maziwa, mito na mabwawa,” alisema Oyuke.

Aliongeza kuongezeka kwa shughuli za uchumi na viwanda, ujenzi na madini kwa asilimia 4.3 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013 kumepelekea kuongezeka kwa pato la taifa.

Alifafanua kuwa shughuli za uzalishaji bidhaa viwandani zilikuwa kwa asilimia 5.8 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka huu tofauti na mwaka jana iliyokuwa asilimia 8.2 utofauti huo ulitokana na kupungua kwa uzalishaji wa saruji, vyakula vilivyosindikwa na nguo.

Oyuke alieleza uzalishaji wa nishati ya umeme umekua kwa asilimia 5.6 katika kipindi cha robo ya mwaka huu ongezeko hilo limetokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa nishati ya umeme unaotokana na mafuta na gesi.
 
CHANZO: NIPASHE